RAIS Dk. John Magufuli ameshtukia mchezo unaofanywa na baadhi ya watu
wakiwamo viongozi, kuficha mabilioni ya fedha ndani na kutangaza uamuzi
mzito wa kubadili noti mpya ili wakose mahali pa kuzipeleka.
Kutokana na hali hiyo, amewataka watu hao kuzitoa mara moja fedha
walizoficha ndani ya majumba yao chini ya magodoro ziingie katika
mzunguko ili zikatumike kwenye miradi ya maendeleo iliyopangwa
kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.
Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam katika mkutano wa 14 wa mwaka
wa wahandisi (ERB), ambao uliwakutanisha wahandisi wa ndani na nje ya
nchi ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kazi zao
na kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto zao.
Dk. Magufuli alisema kuwa muda wowote anaweza akabadilisha fedha ili
wanaozificha fedha hizo za umma wapate hasara kwa kuwa wamesababisha
hasara kubwa kwa wananchi.
Alisema fedha nyingi zimepotea katika kulipa wafanyakazi hewa na
kulipia miradi hewa ambayo haitekelezeki na tayari ofisi yake imeanza
kubaini na kuwafikisha mahakamani, huku akiahidi hakuna mtu atakayeweza
kuukwepa mkono wa sheria.
“Kuna mijitu inaficha hela chini ya magodoro na mabenki, ninatamani
kubadilisha fedha ili wale wote walioficha ziwaozee huko huko. Katika
siku hizi mbili ninaweza kubadilisha fedha na waliozificha wazitoe
wenyewe ili ziweze kuingia kwenye mzunguko.
“Na wajiandae hata siku hizi hizi mbili naweza kubadilisha fedha, hii
meseji iwafikie wale wanaoficha fedha kwenye magodoro na mabenki,”
alisema Dk. Magufuli.
Alisema fedha za bure bure hazitakuwapo tena. “Kwa sasa watu watapata
fedha kwa kufanya kazi na huu ndio wakati wa kutajirika,”alisema Dk.
Magufuli.
Akizungumzia changamoto za sekta ya elimu nchini, alisema alipoahidi
kutoa elimu bure hakujua idadi ya wanafunzi ambao watapata elimu hiyo.
Alisema katika kipindi cha nyuma walikuwa wanaandikisha wanafunzi wa
darasa la kwanza milioni moja na mwaka huu wameandikisha wanafunzi
milioni mbili, hivyo ongezeko hilo ni changamoto kwa Serikali yake.
“Shule za sekondari wamefanikiwa kupata madawati kwa asilimia 98 na
kwa shule za msingi asilimia 88, zoezi la madawati tunakamilisha mwezi
huu,” alisema.
Alisema hivi sasa kuna wafanyakazi hewa na wanafunzi hewa. Kwa Mkoa wa Arusha wamebaini wanafunzi hewa 10,000 na Mwanza 8,000.
“Idadi ya wafanyakazi hewa hadi sasa wamefikia 16,500 kwa miaka yote,
nawahakikishia bado kuna wafanyakazi hewa, watafikia 20,500… hizo ndiyo
changamoto kwangu,” alisema.
Pamoja na hali hiyo alisema kuwa mapato ya Serikali yameongezeka
kutoka asilimia 26 hadi 40, na kwamba Septemba 19, wanatarajia kupokea
ndege mbili aina ya Jet ambazo zimelipiwa na fedha zilizobaki zipo
tayari. Ndege hizo zitatua kwenye viwanja vitatu.
UCHUNGUZI VIWANJA VYA NDEGE
Dk. Magufuli alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17,
alitenga Sh bilioni 100 kwa ajii ya kutengeneza na kukarabati viwanja
vya ndege kwa kiwango cha lami.
“Uwanja wa ndege Dodoma umegharimu shilingi bilioni 11. Kwa bajeti ya
bilioni 100, tulitegemea fedha hizo zitatengeneza viwanja vinane.
Uwanja wa Mwanza umegharimu shilingi bilioni 105 na upanuzi wa Uwanja wa
Dar es Salaam shilingi bilioni 600. Ni kwa nini viwanja viwili
vimetumia gharama kubwa hivyo?” alihoji Rais Magufuli.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa anataka kufanya uchunguzi ili
kuweza kubaini ukubwa huo wa gharama hali ya kuwa waliofanya tathmini ni
watu anaowaamini.
Rais Magufuli alisema hivi sasa kuna miradi mingi ya ndani ambayo
inatarajiwa kuanza ujenzi wake na kuagiza wapewe wakandarasi wa ndani
ambao kama wataamua kufanya kazi, ni wazi nchi itapiga hatua ikiwamo
kufikia kuwa na taifa la uchumi wa kati.
“Mchakato wa kutengeneza reli ya kisasa ‘Standard Gauge’ tumetenga
zaidi ya shilingi trilioni moja na kuna kutengeneza bomba la mafuta
kutoka Hoima hadi Tanga zaidi ya kilometa 14,000. Je, wahandisi wa
Tanzania tumejipanga vipi ili kuhakikisha fedha zinabaki hapa?” alihoji.
USHAURI WA WAHANDISI
Alisema hivi sasa Serikali ipo mbioni kuleta ndege na meli ambazo
zinahitaji wahandisi ambapo alihoji ushauri wa wataalamu hao kuhusu
vyombo hivyo.
“Wahandisi tujitahidi kuzuia mchanga wetu. Katika vitu vinavyoniuma
ni hicho, tumeibiwa mno na tumechezewa mno, kila mahali ni dili,
anachukua fedha anatumia anavyo taka,” alisema.
Rais Magufuli alisema Watanzania ni watu wa ajabu na wana kila kitu ikiwamo gesi inayopatikana nchini.
“Nitashangaa sana kwenye uongozi wangu wahandisi kama hamtasaidiana,
na katika uteuzi wangu nimependelea wahandisi na nimejitahidi
kuwawekaweka kwenye kila eneo. Mnataka nifanyeje wahandisi?” alisema na
kuhoji.
Aliwataka wahandisi hao wajitambue, wajipende na kwamba atafurahi siku moja ikiwa wataweza kutengeneza kampuni yao.
“Mbadilike, ‘you need to change’, kila kitu kinahitaji mhandisi au
aje malaika kutoka mbinguni ndiyo mtabadilika? Muache wivu mtajenga nchi
na msipoamua mtabaki kuwa wasindikizaji,” alisema.
Awali akitoa maelezo kwa Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wahandisi (ERB), Profesa Ninatubu Lema, alisema hadi sasa idadi ya
wahandisi 173,53 nchi nzima wamesajiliwa. Wawili walikuwapo baada ya
uhuru.
“Upungufu wa fundi mchundo unasababishwa na kutokuwapo kwa mikopo
katika vyuo wanavyosoma katika ngazi ya stashahada na kukimbilia ngazi
ya shahada kwa sababu wanapewa mikopo ya kujikimu,” alisema Profesa
Lema.
Mwenyekiti huyo wa ERB, alimuomba Rais Magufuli aelekeze miradi yote mikubwa itumike kama darasa la mafunzo kwa wahitimu.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa, alisema sekta ya miundombinu ni muhimu katika kufanya
maendeleo.
“Asilimia 59 ya barabara ni kiwango cha lami, lengo kubwa ni kuboresha usafiri wa maji na nchi kavu,” alisema Profesa Mbarawa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment