UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika,
awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda
na kutupa afya njema hadi kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa
Nne wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 6 Septemba, 2016.
2.
Nitumie fursa hii pia kukupa pole, Mheshimiwa Spika,
kwa maradhi yaliyokusibu lakini kikubwa nielezee furaha yangu kwa uponyaji
ambao Mwenyezi Mungu amekujaalia na hivi sasa tuko pamoja humu ndani.
Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uendelee kupata nguvu na afya njema.
3.
Mheshimiwa
Spika,
tangu tulipokutana mara ya mwisho, kumekuwepo majanga na matukio mbalimbali ya maradhi,
ajali, ujambazi na matukio mengine ambayo yamesababisha vifo na majeruhi kwa
Watanzania wenzetu, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, ninatoa pole kwa
wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha
na waliopo hospitali.
4.
Mheshimiwa
Spika, leo tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumekamilisha shughuli zote
zilizopangwa
kwenye Mkutano huu. Naomba nitumie fursa hii ya awali kabisa kukupongeza sana
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti na Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa ufanisi mkubwa. Kazi hizo
zilijumuisha kujadili na hatimaye kupitisha Miswada mbalimbali ya Serikali.
Napenda kukiri kwamba mijadala ya mkutano huu ilikuwa ya uwazi na hoja
zilizotolewa zililenga kuiletea maendeleo nchi yetu. Kutokana na michango
mizuri ya Waheshimiwa Wabunge na yenye tija, ilibidi mara kadhaa vikao vyetu
kuendelea hadi usiku nje ya muda wa kikanuni. Nawapongeza sana!
TUKIO LA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA MIKOA YA
KANDA YA ZIWA
5.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kuwa tarehe
13 Septemba, 2016 Serikali iliwasilisha hapa Bungeni taarifa ya masikitiko
kuhusu maafa makubwa yaliyoikumba Nchi yetu tarehe 10 Septemba, 2016 kutokana
na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera,
Geita, Mwanza na Mara. Tukio
hilo ambalo liliathiri zaidi Mkoa wa Kagera lilitokea siku ya Jumamosi majira
ya saa 9.27 alasiri, ambapo Mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, lenye
nguvu ya mtetemo wa kipimo cha 5.7, kwa kutumia skeli ya “Ritcher”. Tetemeko hilo
limesababisha vifo vya watu 17 na
majeruhi 253. Napenda nitumie nafasi
hii kwa mara nyingine kuwapa pole wafiwa wote na wale waliopata majeraha
mbalimbali. Tunaomba Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina. Kwa
wale waliopata majeraha, tunamuomba Mungu awaponye haraka.
6.
Mheshimiwa
Spika,
tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa sana wa nyumba, vituo vya afya, shule
pamoja na miundombinu ya barabara. Aidha, shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo
vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni. Nyumba 840 zimeteketea
kabisa, na nyingine 1,264 kupata nyufa.
Kwa sasa uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Kamati
ya Maafa ya Mkoa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalamu wa masuala
ya matetemeko, na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya kiasi
cha hasara iliyopatikana.
7.
Mheshimiwa Spika,
kama Bunge lako Tukufu lilivyojulishwa, Serikali kwa kushirikiana na Wadau
mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kushughulikia athari za tetemeko hilo ikiwa
ni pamoja na kufanya jitihada ya kurejesha hali ya utulivu, miundombinu
iliyoharibika ili kuirejesha katika hali ya kawaida.
8.
Mheshimiwa
Spika,
pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanyika ikiwemo viongozi kutembelea maeneo
yenye madhara, mpaka sasa Serikali imefanya mambo yafuatayo:-
(a)
Kuhusu Chakula: Wananchi wenye
mahitaji ya chakula wameendelea kupatiwa chakula kama vile, unga, mchele na
maharage, sukari na chumvi pamoja na mafuta ya kula. Tathmini ya kubaini
mahitaji halisi ya chakula inaendelea.
(b)
Kuhusu Matibabu: Serikali imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa.
Aidha, Timu ya Wataalam na Madakta 12 wamepelekwa Bukoba kutoka Hospitali ya
rufaa ya Kanda ya Bugando. Napenda kuwashukuru pia wadau mbalimbali ambao
wamechangia eneo hili wakiwemo Medecins
Sans Frontiers, Ubalozi wa China, Jhpiego
(USAID) na Chama cha Wafamasia.
(c)
Makazi: Wananchi waliokosa kabisa
hifadhi ya makazi wamepewa maturubai na mahema kwa ajili ya makazi ya muda.
Aidha, waathirika ambao nyumba zao zimebomoka kabisa, kwa kuanzia kila mmoja
ametengewa mabati 20, saruji mifuko mitano, blanketi na mikeka. Pia wapangaji
waliokuwa katika nyumba hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita
ili apate mahali pa kujihifadhi.
(d)
Kuhusu Shule
zilizoathirika:
Serikali inajenga miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa, mabweni na
vyoo hususani katika shule za sekondari za Ihungo na Nyakato zilizofungwa kwa
muda wa wiki mbili. Tathmini ya kitaalam ikikamilika, mpango wa ujenzi wa
miundombinu ya kudumu itafanyika na maandalizi yanaendelea kupata rasilimali
kwa ajili hiyo.
(e)
Mazishi: Serikali
imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa
jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha Shilingi milioni 20 za rambirambi kwa
wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa.
(f)
Barabara: Tathmini ya uharibifu wa
barabara imefanyika na barabara zilizoharibika zitarejeshwa katika hali ya
kawaida ili wananchi waendelee kupata huduma za msingi. Vilevile, Serikali
inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha miundombinu ya maji safi na maji taka
inakarabatiwa na kuhakikisha usafi unaendelea kuwa katika viwango stahiki.
Kwa ujumla,
Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa taasisi za umma ikiwemo majeshi ya ulinzi
na usalama na rasilimali zake vinatumika kutoa huduma zote muhimu kwa
waathirika katika kipindi hiki.
9.
Mheshimiwa
Spika, hivi sasa
Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalam kupitia Wizara ya Nishati na
Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kubaini chanzo
cha tukio, kiasi cha athari zilizotokea chini ya miamba na juu ya ardhi.
Tathmini hii ya kitaalamu itatupa picha na mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji
wa miundombinu iliyoharibika.
10.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie
nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na
Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyoshirikiana na Serikali katika kushughulikia
janga hili la kitaifa la tetemeko la ardhi Napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge kwa michango yenu ya hali na mali na kwa kututia moyo katika
kushughulikia tukio hili kubwa lililoathiri maisha na shughuli za wananchi pale
mkoani Kagera.
11.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, kwa niaba ya Serikali, na kipekee, nitumie fursa hii
kuishukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Waheshimiwa Mabalozi, Wawakilishi
wa Mashirika ya Umma na ya Kimataifa waliopo nchini, viongozi wa vyama vya
siasa na wananchi kwa ujumla, ambao waliitikia wito wa Serikali wa kushiriki na
kusaidia juhudi za Serikali za kuwasaidia waaathirika wa tetemeke la ardhi. Tunawashukuru
sana wote waliotuunga mkono kwa fedha na vifaa mbalimbali.
12.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na jitihada hizo zinazofanywa, Serikali imeshatoa na
inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali. Hivyo, kwa wananchi na wadau walio tayari
kuchangia wanaweza kutumia Akaunti ya Maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB
yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa
jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode:
CORUtztz kwa kutuma fedha kwa njia ya kawaida au Mobile Banking. Vilevile, michango hiyo inaweza kutumwa kwenye Namba
za simu za mkononi, 0768-196-669 (M-Pesa),
au Namba 0682-950-009 (Airtel Money) au Namba 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Nawaomba
wananchi wote, Sekta Binafsi na Jumuiya ya Kimataifa tuonyeshe mshikamano
kuungana na Serikali katika kusaidia wenzetu walioathirika na tetemeko hilo kwa
kutoa michango ya hali na mali.
13.
Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali
itaendelea kuratibu michango yote itakayotolewa na kuifikisha kwa walengwa.
Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha
uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na majanga ya aina hii na mengineyo.
SHUGHULI
ZA BUNGE
14.
Mheshimiwa
Spika, tunahitimisha
mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli
mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali na kusomwa kwa mara
ya pili na pia kusomwa mara ya tatu ni kama ifuatavyo:-
Kwanza: Muswada wa Sheria ya upatikanaji wa Habari
wa mwaka 2016; (The Access to Information
Bill, 2016);
Pili: Muswada wa Sheria ya Uthamini na
Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016; (The
Valuation and Valuers Registration Bill, 2016);
Tatu: Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016; (The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016);
Nne: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa
Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016; (The
Chemist Professionals Bill, 2016);
Tano: Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti
wa Kilimo wa Mwaka 2016; (The Tanzania
Agricultural Research Institute Bill, 2016);
Sita: Muswada wa Taasisi ya Utafiti wa
Uvuvi wa Mwaka 2016; (The Tanzania
Fisheries Research Institute Bill, 2016).
Miswada ya Sheria ya Serikali iliyosomwa kwa mara ya
kwanza ni:-
(a)
Muswada
wa Sheria ya huduma za Hbari za Mwaka 2016 (The
Media services Bill, 2016).
(b)
Muswada
wa Sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016 (The Written Laws Micellianeous Amendments)
(No.3) Bill, 2016).
15.
Mheshimiwa
Spika, katika
Bunge hili, Serikali ilitoa kauli zifuatazo:-
Kwanza: Kauli
ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini na uzalishaji kwa msimu wa mazao kwa
mwaka 2015/2016; na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017;
Pili: Kauli
ya Serikali kuhusu tukio la tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba,
2016 Mkoani Kagera na Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa.
16.
Mheshimiwa
Spika, kipekee,
naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na
Wataalam wake, kwa mchango wao mkubwa katika kuandaa miswada hiyo kwa umakini
mkubwa na hivyo kuwawezesha Waheshimiwa Mawaziri kuiwasilisha Bungeni kwa weledi
mkubwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa
michango yao mizuri. Serikali itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa
utekelezaji.
17.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 110 ya msingi na mengine 222
ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Vilevile,
jumla ya maswali matano ya msingi na ya nyongeza ya
Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ya kila Alhamisi yaliulizwa na kupata
majibu.
MWENENDO NA MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI
18.
Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa
hali ya uchumi, hususan mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa Taifa. Napenda
kutumia fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla
kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika. Aidha,
tathmini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, inaonesha kuwa Mabenki yetu bado yapo salama, na yana
mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha. Aidha,
Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya Taifa ya
Takwimu zinafuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa Hali ya Uchumi Nchini. Mathalan,
tarehe 14 Septemba, 2016 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu,
alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini ambapo
alilihakikishia Taifa na Jumuiya ya Kimataifa kwamba hali ya uchumi wetu ni
shwari kabisa na si mbaya kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
19.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo ya Benki Kuu pamoja na mambo mengine, imebainishwa
kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji
wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa wa kuridhisha. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka
2015. Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano,
utangazaji na huduma ya intaneti; kuongezeka kwa uchimbaji na madini. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya
juu katika kipindi hicho ni sekta ya
fedha kwa asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia
10.2.
20.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo huo mzuri wa viashiria vya
shughuli za uchumi, ni dhahiri kwamba mwelekeo wa uchumi katika kipindi kijacho
unatoa matumaini ya uchumi kuendelea kuimarika kama ilivyokadiriwa hapo awali
na kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka
2016. Hii inachangiwa pia na ukweli
kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi
endelevu; usimamizi thabiti wa rasilimali za umma; na ujenzi wa miundombinu
bora yenye kuimarisha lengo la kujenga
uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI KWA MWEZI JULAI NA AGOSTI,
2016
21.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuongeza na
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika
mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza
utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali
imeendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi ili kuleta tija kwa Taifa katika
ukusanyaji mapato.
22.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imelenga kukusanya mapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya
Halmashauri, ya jumla ya shilingi trilioni 18.46, sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote ya shilingi trilioni 29.5. Takwimu
za mwenendo wa ukusanyaji mapato zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia
Julai hadi Agosti, 2016, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), yalikuwa shilingi trilioni 2.168
ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113, sawa na asilimia 103 ya lengo. Aina za kodi zilizochangia
sana katika ongezeko hilo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mashine za kielektroniki katika
ukusanyaji wa mapato. Mapato yasiyo ya kodi kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi
bilioni 271.1; sawa na asilimia 60
ya lengo la kukusanya shilingi bilioni
448.4. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yalikuwa Shilingi bilioni 45.4; ikiwa ni asilimia 41 ya lengo
la kukusanya shilingi bilioni 110.9.
Napenda kutumia fursa hii kuzihimiza
Wizara na Halmashauri kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
23.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
Kwanza: Kuendelea
kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi
wa mara kwa mara katika maeneo ya biashara, viwandani, migodi, bandarini,
kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki
zinakusanywa;
Pili: Kusimamia kikamilifu matumizi ya
vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza
ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
Tatu: Kuendelea kupanua wigo
wa walipa kodi, ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze
kuingia katika mfumo wa kodi;
Nne: Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato
yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali na Halmashauri zote
nchini; na
Tano: Kuendelea
kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.
MPANGO
WA SERIKALI WA KUHAMIA DODOMA
24.
Mheshimiwa Spika, tarehe 23
Julai, 2016 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi hapa Dodoma
alieleza kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukamilisha mchakato na
ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji wa Makao Makuu – Dodoma. Aidha,
Mheshimiwa Rais alirejea kauli hiyo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa Maadhimisho
ya Siku ya Mashujaa Nchini ambayo yalifanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza katika
Viwanja vya Mashujaa, mjini Dodoma. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa anatarajia
kwamba Serikali yake yote itakuwa imehamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne
na miezi minne, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020.
25.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwamba Mpango wa sasa wa Serikali
wa kuhamia Dodoma ni mwendelezo wa utekelezaji
wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 iliyozingatia agizo
lililotolewa tarehe 1 Oktoba, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa Chama cha TANU.
Hivyo, hatua zinazochukuliwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano ni mwendelezo tu wa
utekelezaji wa mipango ya awali iliyokuwa inatekelezwa mwaka hadi mwaka na
Serikali za Awamu zilizopita, kuanzia Awamu ya Kwanza lilipotolewa tamko hilo
mwaka 1973; chini ya Uongozi wa Rais wa
Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
26.
Mheshimiwa
Spika, katika
kutekeleza azma hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya tamko la Mheshimiwa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli la tarehe 23 Julai 2016, yafuatayo yamefanyika:
Kwanza: Tarehe
26 Julai, 2016 nilikutana na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma (Viongozi wa Chama na
Serikali wa Mkoa na Wilaya, Wazee maarufu, Viongozi wa Madhehebu ya Dini na
Wadau mbalimbali) ili kuwajulisha kuhusu mkakati wa sasa wa Serikali wa kuhamia
Dodoma. Aidha, niliutaka Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuwasilisha mapendekezo ya
mpango kazi wa kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma;
Pili: Katika
kipindi cha siku 14, Uongozi wa Mkoa wa Dodoma uliwasilisha kwangu Taarifa ya
Serikali kuhamia Dodoma kama ilivyokusudiwa. Aidha, tarehe 15 Agosti, 2016 Mkoa
uliwasilisha Mpango huo katika Kikao cha Baraza la Kazi la Mawaziri pamoja na
Makatibu Wakuu na kupata ushauri na maoni yao ya kuuboresha;
Tatu: Serikali imeunda Kamati Ndogo chini
ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji
wa Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa lengo la kufanya mapitio ya upatikanaji wa
Ofisi na Makazi na miundombinu muhimu. Kamati hiyo inashirikisha Taasisi
mbalimbali za Serikali zilizopo Dodoma na Kitaifa, zikiwemo TBA, DUWASA,
TANROADS, TEMESA, TANESCO, SUMATRA, TTCL, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji;
Nne: Aidha, Serikali imeunda Kamati ya
Kitaifa ya Makatibu Wakuu ambao wanaratibu zoezi zima na utaratibu wa Serikali
kuhamia Dodoma;
Tano: Tarehe 1 Septemba, 2016, Serikali
ilikutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Fedha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na
Watendaji Wakuu wa Taasisi za Sekta Binafsi zinazohusika na ujenzi wa
miundombinu nchini. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupata mawazo ya Sekta
Binafsi, Taasisi za Fedha na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuisaidia Serikali
kuboresha mikakati ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia kuwa Serikali peke yake
haiwezi kukamilisha jambo hili. Katika kikao hiki tumekubaliana kwamba kuanzia
sasa kuwepo na vikao baina ya Makatibu Wakuu na Wadau wa Sekta Binafsi, angalau
mara moja kwa mwezi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa
Kamati hiyo akiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kikao hicho kitakuwa cha
mashauriano na kupeana mrejesho wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhamia
Dodoma kwa kuzingatia mchango wa sekta ya umma na sekta binafsi katika ujenzi
wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii, uwekezaji na uzalishaji biashara na
huduma mbalimbali;
Sita: Serikali
pia imeunda Kamati Maalum ya Wataalam Washauri itakayoshirikiana na CDA kufanya
Mapitio ya Mpango Kamambe (Master Plan)
wa Mji wa Dodoma ili kubaini mahitaji halisi ya sasa na siku zijazo katika upeo
wa miaka 50 na zaidi. Zoezi hili litahitaji ushirikishwaji mkubwa wa jamii na
sekta binafsi. Lengo la Serikali ni kuwa na mji uliopangwa vizuri na unaozingatia
vigezo mbalimbali vya Kimataifa.
27.
Mheshimiwa
Spika,
napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zilizopita
zilizoongozwa na Chama cha Mapinduzi za kuweka miundombinu mbalimbali muhimu ya
kufanikisha mpango wa Serikali kuhamia Dodoma. Tathmini iliyofanywa na OWM, Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, pamoja na wadau mbalimbali, inaonyesha kuwa kwa ujumla
miundombinu iliyopo Dodoma kwa sasa ina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya
Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2016 hadi
mwaka 2020.
RATIBA YA
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
28.
Mheshimiwa
Spika,
ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba
itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016
hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama
ifuatavyo:
Kwanza: Awamu
ya Kwanza
itakuwa kati ya mwezi Septemba, 2016 na
Februari, 2017. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu
wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza.
Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na
wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara
nyingine kuhamia Dodoma;
Pili: Awamu
ya Pili
itakuwa kati ya mwezi Machi 2017 na
Agosti 2017. Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali
kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi
wake kuja Dodoma;
Tatu: Awamu ya Tatu itakuwa kati ya
mwezi Septemba 2017 na Februari 2018;
ambapo Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya
Wizara.
Nne: Awamu
ya Nne
itakuwa kati ya mwezi Machi 2018 na
Agosti, 2018; na Awamu ya Tano
itakuwa kati ya Mwezi Septemba 2018 hadi
Februari, 2020. Katika kipindi hiki cha Awamu ya Tatu na Nne; Wizara
zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.
Tano: Awamu ya Sita, itakuwa kati ya mwezi Machi, 2020 na Juni, 2020 ambapo Ofisi ya Rais
ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.
Nazishauri Wizara zote kuanzisha
mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka
Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki.
29.
Mheshimiwa
Spika,
naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa sekta binafsi na
wadau wa maendeleo wa ndani na nje kuwekeza Dodoma ili kuboresha zaidi
miundombinu iliyopo na kuongeza majengo ya Ofisi na makazi ya Watumishi
kuwekeza katika huduma za afya na elimu, huduma za kibiashara kama mabenki,
maduka makubwa (Shopping Malls) na
masoko, mahoteli na maghala. Aidha, napenda kurejea maelekezo niliyoyatoa kwa
Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) na Mkoa wa Dodoma na
Manispaa kuhakikisha kwamba Mji Mkuu wa Dodoma unaendelezwa kwa kasi ili
kupokea watumishi wengi na familia zao pamoja na sekta binafsi watakaohamia Dodoma.
30.
Mheshimiwa
Spika, napenda
kusisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma na CDA wahakikishe kuwa pamoja na kuandaa maeneo
ya makazi na Ofisi, pia watenge maeneo maalumu ya huduma muhimu kama vile maeneo kwa ajili
ya kituo kikuu cha biashara, bustani, bandari kavu na kuendelea kuongeza eneo
la viwanda na huduma mbalimbali za kibiashara. Aidha, naagiza Mamlaka za
Mipango Miji Mkoani Dodoma na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo wa
kielektroniki wa upatikanaji wa viwanja ambao utatambua mahitaji kwa utaratibu
wa wazi, na bila urasimu usio wa lazima.
Vilevile, nashauri Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Sekta binafsi kutumia fursa hii
kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watumishi
na wageni wanapokuja Dodoma wasipate taabu kutafuta mahali pazuri pa kuishi.
SEKTA YA KILIMO:
Hali
ya Uzalishaji na Upatikanaji Chakula Nchini:
31.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya
chakula kwa mwaka 2015/16 iliyofanyika mwezi Juni 2016 inaonesha kuwa
uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa utafikia tani 16,172,841. Aidha, Mikoa 11 kati ya 26 ilibainika kuwa na
ziada ya chakula, mikoa 12 kuwa na utoshelevu wa chakula na miwili (2) uhaba wa chakula. Kutokana na mahitaji
ya chakula kwa mwaka 2016/2017 kuwa tani 13,159,326, nchi itakuwa na utoshelevu
wa chakula kwa wa asilimia 123, sawa na ziada ya tani 3,013,515
kwa mazao yote ya chakula.
32.
Mheshimiwa Spika, tathmini hii ilibaini pia
kuwa chakula kingi aina ya nafaka kilikuwa tayari kimesafirishwa nje ya nchi
kutokana na nchi jirani kutokuwa na mavuno mazuri bila kuzingatia kwanza haja
ya utoshelevu wa ndani ya nchi.
Ili kuhakikisha kuwepo kwa hali ya usalama wa
chakula Nchini na kuepuka baa la njaa hapo baadaye, Serikali imeamua kuwa
kuanzia tarehe 10 Septemba 2016 sehemu ya ziada ya nafaka ya mahindi na mchele
itasafirishwa nje ya nchi kwa vibali vitakavyotolewa kwa ya Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi pekee. Serikali itasimamia ili
kusiwe na upungufu wa chakula nchini.
33.
Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii
kuwataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kuwahamasisha wakulima na wafanyabiashara kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo hususan mahindi na mpunga kwa kuyasindika, kabla ya
kusafirisha nje ya nchi ili yapate bei nzuri zaidi,
na pia kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Utaratibu wa kutoa
ruzuku ya pembejeo za kilimo katika msimu wa 2016/2017
34.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2003/2004 hadi mwaka 2015/2016, Serikali
imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya
chakula, na hususan mahindi, mpunga na mtama. Pia, ruzuku ya pembejeo hutolewa
kwa mazao ya biashara ya korosho, pamba, chai, kahawa na alizeti. Ruzuku hiyo, imekuwa
ikitolewa kwa kutumia mfumo wa vocha na vikundi vya wakulima kukopeshwa
pembejeo hizo kupitia taasisi za fedha na makampuni ya pembejeo za kilimo.
Pamoja na juhudi hizo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika kufikia lengo
hilo.
35.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi, katika msimu wa 2016/2017, Serikali imetenga shilingi
bilioni 5 kwa ajili ya ruzuku ya
viuatilifu vya mazao ya kilimo na shilingi bilioni
25 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo nyingine za kilimo. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 20 ni za kununua tani 21,892 za mbolea kwa kaya 354,928. Aidha, Serikali italipia asilimia 30 ya bei ya mbolea kwenye
soko, sawa na shilingi 20,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kupandia; na shilingi
12,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia.
36.
Mheshimiwa
Spika, ili mbolea hizo ziweze kuwafikia walengwa kwa wakati na kwa bei
nafuu, Kampuni ya Mbolea Tanzania itasambaza mbolea katika vituo vyake 29 nchini na kuiuza kwa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo
kwa shilingi 38,000 kwa mfuko wa
kilo 50 kwa mbolea ya kupandia na shilingi 26,000
kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia. Ninaziagiza
Halmashauri zote kuhakikisha Mawakala wa Pembejeo wanauza mbolea kwa bei
itakayopangwa. Ni imani yangu kuwa wakulima wengi watatumia fursa hii ya kupata
mbolea ya ruzuku kuendeleza kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara.
SEKTA YA
USHIRIKA
Maboresho katika tasnia ya Ushirika
37.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa ushirika, kama chombo cha
kuwaunganisha, kuwapa nguvu na kuwatetea wanachama wao katika kilimo, ufugaji,
uvuvi na tasnia nyingine, unakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi mbovu,
ubadhirifu na ufujaji mali wa baadhi ya viongozi. Changamoto hizo zinawaumiza sana
wakulima na kuwafanya wakate tamaa katika uzalishaji, masoko na uendeshaji wa
shughuli zao za kiuchumi.
38.
Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na changamoto hizo, Serikali itafanya marekebisho makubwa
ndani ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika; iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakaobainika kuhusika na ubadhirifu
wa mali za ushirika. Aidha, baadhi ya
Maafisa Ushirika waliokaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu watahamishiwa
katika maeneo mengine.
39.
Mheshimiwa Spika, Serikali itafanya marekebisho makubwa kwa Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya
Ushirika (COASCO) ambalo limeshindwa kufanya kazi zake kwa weledi.
40.
Mheshimiwa Spika, katika kufufua ushirika, Serikali itahuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, na kuijengea Tume ya
Maendeleo ya ushirika uwezo wa kuajiri/kuhamishia watendaji katika ofisi za
Mikoa na Halmashauri zote ili kusimamia vyama vya ushirika; kufanya kaguzi za
mara kwa mara, kuondoa tatizo la upotevu wa rasilimali za vyama; kusimamia
upatikanaji wa viongozi wenye sifa na watendaji wenye weledi wenye kuongoza
vyama kwa ufanisi; kupanua wigo wa shughuli za ushirika katika sekta
nyingine za kiuchumi zaidi ya kilimo ili kuongeza idadi ya vyama vya ushirika
nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa kipato kwa wananchi wengi.
SEKTA YA ELIMU
Motisha
kwa Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata
41.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi
mzuri na wa karibu shuleni, Serikali imeanza kutoa posho ya madaraka kwa Walimu
Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata kila mwezi kuanzia mwezi Julai,
2016 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.09 kimetolewa. Aidha, mpango mwingine uliopo ni kuwapatia Waratibu Elimu Kata
pikipiki ili ziwawezeshe katika ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za kielimu
katika kata zao nchi nzima. Kwa kuanzia, Waratibu Elimu Kata wa Mikoa 7 ambayo ilikuwa na ufaulu wa chini katika matokeo ya kuhitimu
darasa la saba tayari wameshapatiwa jumla ya pikipiki 1,015. Mikoa iliyopatiwa
pikipiki hizi pamoja na idadi ya pikipiki ni kama ifuatavyo: - Dodoma (192); Mara (99), Simiyu (122),
Shinyanga (128), Tabora (200), Kigoma (135), Lindi (139). Mikoa iliyobakia
itapatiwa pikipiki chini ya programu ya Kukuza Stadi za Kusoma na Kuandika ya
LANES (Literacy and Numeracy Education
Support Program) pamoja na UNICEF.
Upungufu wa Walimu na Miundombinu
42.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa upungufu wa walimu, Serikali imeamua walimu wapya
watakaoajiriwa mwaka 2016 wapangwe shuleni moja kwa moja na kwenye maeneo yenye
upungufu mkubwa wa walimu.
Hali
ya Madawati
43.
Mheshimiwa
Spika, utakumbuka kuwa tarehe
16 Machi, 2016 Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania alitoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 30
Juni, 2016 kusiwepo mwanafunzi anayekaa chini kwa kukosa dawati.
44.
Mheshimiwa
Spika,
katika utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais, kufikia mwezi huu wa Septemba madawati 951,610 kwa shule za Msingi yalitengenezwa na hivyo kufikia
madawati 3,084,781 sawa na asilimia 94.4.
Kwa upande wa shule za sekondari, idadi ya madawati yaliyotengenezwa yamefikia madawati 1,490,488 sawa na asilimia 99.4 na kufanya upungufu kuwa madawati
182,864 kwa shule za Msingi na 8,380 kwa Shule za Sekondari.
Madawati hayo
yanaendelea kutengenezwa na Mikoa ambayo haijakamilisha inatakiwa iwe
imekamilisha ifikapo tarehe 30 Septemba, 2016.
MAABARA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI
45.
Mheshimiwa
Spika, mahitaji
ya Maabara kwa shule za sekondari ni 10,803.
Maabara zilizopo ni 5,756 sawa na
asilimia 53.2 ya mahitaji. Upungufu
uliopo ni maabara 5,047 ambazo
zingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2016/17,
Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imetenga jumla ya shilingi bilioni 18.876 kwa ajili ya umaliziaji
wa maabara 2,135 katika shule za sekondari
kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Serikali inaendelea na ujenzi wa jumla ya
maabara 290 kupitia mpango wa MMES
II katika shule za sekondari 528.
Upungufu utakaokuwepo baada ya kukamilika kwa maabara hizi ni maabara 4,807.
Serikali itaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuondoa upungufu
huo.
Mitihani
ya Elimu ya Msingi
46.
Mheshimiwa
Spika, mtihani wa
kumaliza darasa la saba ulifanyika tarehe 7 hadi 8 Septemba, 2016 nchini kote.
Idadi ya watahiniwa 795,761 walisajiliwa
kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2016. Aidha, taarifa za awali
zinaonesha kuwa takriban watahiniwa 789,302
walifanya mtihani huo, sawa na asilimia 99.2 ya waliosajiliwa. Taarifa rasmi
itatolewa baada ya Mikoa na Halmashauri kukamilisha kufanya mawasilisho ya
taarifa kamili ya ufanyikaji wa Mtihani huo.
47.
Mheshimiwa
Spika,
tafsiri ya idadi ya kubwa ya wanafunzi waliofanya mitihani ya darasa la saba ni
kwamba yapo matarajio kuwa idadi ya wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza katika
mwaka 2017 itakuwa kubwa kuliko nafasi zitakazo kuwepo mwanzoni mwa mwaka 2017
katika shule za Sekondari ikiwa hali ya miundombinu itaendelea kuwa kama ilivyo
sasa. Hivyo basi, natoa wito kwa
Halmashauri zote nchini zijiandae kuwawezesha wanafunzi wote watakaofaulu
kujiunga na kidato cha kwanza kwa kuongeza vyumba vya madarasa, madawati,
matundu ya vyoo na nyumba za Walimu.
UHAKIKI
WA VYETI KWA WATUMISHI
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea na zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi ingawa limeendelea kuleta
usumbufu kwa watumishi katika baadhi ya maeneo. Naagiza kwa Wakurugenzi waandae
vituo maalum vilivyo jirani na vituo vyao vya kazi badala ya kuwakusanya kituo
kimoja ili kuwapunguzia adha na gharama. Halmashauri zote zizingatie agizo hili
ili maafisa utumishi waende kwenye vituo hivyo.
JITIHADA
ZA SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI WA ANGA
49.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie
fursa hii kuzungumzia kidogo kuhusu jitihada za Serikali za kuimarisha usafiri
wa anga hapa nchini kuanzia mwaka 2016/2017 Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea
na mpango wake wa kuboresha usafiri wa anga hapa nchini. Hatua zinazochukuliwa
ni pamoja na kuendelea kuboresha viwanja vya ndege nchini. Lengo ni kuhakikisha
kuwa kila Mkoa unakuwa na kiwanja cha ndege cha kisasa, chenye ubora unaofaa
kutua ndege.
50.
Mheshimiwa Spika, ili kwenda
sambamba na azma ya Serikali kuhamia Dodoma muda mfupi ujao, kiwanja cha ndege
cha Dodoma kimefanyiwa ukarabati mkubwa ili kuweza kuhudumia ndege zenye uwezo
wa kubeba hadi abiria 90. Sambamba
na hatua hizo, Serikali imedhamiria kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania
(ATCL), ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya kuongeza ufanisi
wa huduma za usafiri wa anga kupitia ATCL.
51.
Mheshimiwa Spika, napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imenunua ndege mbili (2) aina ya Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria
76 kila moja zitakazotumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani
na nchi jirani. Ndege hizo zinatarajia
kuwasili nchini mwezi huu wa Septemba, 2016.
Aidha, taratibu za kununua ndege nyingine mbili zenye ukubwa wa kati (medium haulage aircraft) zitakazokuwa na
uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 110 zimeanza. Ndege hizo zitahudumia soko la kikanda.
52.
Mheshimiwa Spika, pamoja na
hatua hiyo Serikali imeanza kazi ya kuiunda upya ATCL. Jana tarehe 15 Septemba,
2016, Mheshimiwa Rais amefanya uteuzi wa Mtendaji Mkuu mpya wa ATCL. Aidha, mchakato wa
uteuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo unakamilishwa. Vilevile, Serikali
imegharamia mafunzo ya wataalam mbalimbali wakiwemo wahandisi watakaohudumia ndege
mpya. Hatua hizo zitasaidia sana kuboresha shirika letu la ndege na usafiri wa
aga hapa nchini katika kipindi kifupi kijacho.
HALI YA AMANI NA UTULIVU NCHINI
53.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama vimeendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo
nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi yetu. Usalama wa raia na mali zao
umeendelea kudumishwa kwa kutambua kuwa ni miongoni mwa misingi mikuu ya ukuaji
wa uchumi wa Taifa letu. Kwa namna ya pekee, napenda kutumia fursa hii
kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi.
54.
Mheshimiwa Spika, ili Jeshi la Polisi liendelee kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya
kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu Nchini, Serikali itaendelea kuwajengea
uwezo Maafisa, Wakaguzi na Askari na pia kutekeleza mambo yafuatayo:-
Kwanza: Kutabiri
mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za uhalifu
pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo korofi, wahalifu
wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na uhalifu huo.
Pili: Kuyatambua
maeneo nyeti (hotspots) yenye vivutio
vya uhalifu, na kuyapangia ulinzi, misako na doria imara.
Tatu: Kutoa
elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa
kutumia vyombo vya habari, mihadhara, mikutano, maonesho na usambazaji wa
machapisho na vipeperushi.
Nne: Kufanya
misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
mbalimbali nchini.
Tano: Kushirikiana
na wadau wote wa ulinzi na usalama kubadilishana taarifa za kiintelijensia
pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya
zamani.
55.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa suala la amani, na usalama na utulivu nchini halina
mbadala. Nawaomba tudumishe hali ya amani na usalama ili tufanikishe lengo letu
la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
MICHEZO
56.
Nchi yetu
imeendelea kuwika kimichezo hasa katika soka. Nitumie fursa hii kuwapongeza
vijana wetu wa Serengeti Boys kwa ushindi wao. Hivi sasa timu yetu inajipanga
kupambana na timu ya Congo (DRC) hapo Septemba 18.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie nafasi hii
kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa
kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote vya mkutano huu. Niwashukuru
tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru pia Watendaji wa Serikali
kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu maswali na hoja mbalimbali
za Wabunge. Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na
Watendaji wote kwa usalama kabisa. Thanx to wanahabari kwa kuihabarisha jamii
juu ya mkutano wetu. Kipekee, nimshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah
na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha shughuli zote za mkutano huu kwa
mafanikio makubwa.
58.
Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha
mkutano huu leo na kuelekea katika Majimbo yetu, sote tunatambua kuwa msimu wa
mvua za vuli na masika unakaribia.
Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuziagiza Wizara zinazohusika na
usambazaji wa pembejeo kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei
iliyopangwa. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe kwamba wanasimamia kikamilifu
shughuli za kilimo katika maeneo yao ili kila familia na kaya ianze maandalizi
ya kilimo mapema.
59.
Mheshimiwa
Spika,
napenda pia kurejea katika kusisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya kukuza
uchumi katika Taifa letu. Hivyo, nichukue fursa hii kuwahakikishia wafanyabiashara
na wenye viwanda na wawekezaji kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kuwapa ushirikiano wa dhati ili kuendeleza shughuli zao kama ambavyo
wamejipanga. Wafanye shughuli zao bila
woga au tashishi yoyote.
60.
Mheshimiwa
Spika,
mwisho, lakini si kwa umuhimu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu
awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge wote katika safari ya kurejea majumbani
kwenu.
61.
Mheshimiwa
Spika,
baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa
liahirishwe hadi tarehe 1 Novemba, 2016,
siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi
litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
62.
Mheshimiwa
Spika, naomba
kutoa hoja.
0 comments:
Post a Comment