SERIKALI imewaondoa watumishi hewa 17,201 katika utumishi wa umma,
ambapo licha ya kupokea mishahara pia mikopo mingi ilitolewa visivyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angella Kairuki alisema hayo jana mjini Dodoma wakati wa
kuapishwa kwa wakurugenzi watendaji wapya 13 walioteuliwa Septemba 10,
mwaka huu na Rais John Magufuli.
Kairuki alisema kuanzia Machi mwaka huu hadi sasa wameondoa watumishi
hewa 17,201 kwenye utumishi wa umma na zoezi hilo bado linaendelea.
“Tumegundua mikopo mingi imetolewa visivyo,” alisema Kairuki na kuongeza kuwa asilimia 80 hadi 90 ya watumishi hewa ni watoro.
“Kwenye sekta ya elimu kuna Mratibu wa elimu kata, maofisa elimu
lakini wamekuwa hawafuatilii walimu wengi wamekuwa hawapo kwenye vituo
vya kazi lakini wanapokea mishahara,” aliongeza waziri huyo na
kubainisha kwamba kumekuwa na tabia ya walimu ambao hawako kazini kwa
kipindi kirefu, lakini walimu wenzao wamekuwa wakiwaandikia kwenye
kitabu cha mahudhurio na kuwasainia ili kuonesha kuwa wapo kazini, jambo
ambalo ni kinyume cha utaratibu.
“Mwarobaini wa walimu wanaowajazia vitabu vya mahudhurio walimu ambao
hawafiki kazini dawa yao iko jikoni, tutafuatilia kituo kimoja hadi
kingine kuwabaini na tutachukua hatua,” alieleza na kuongeza kuwa
maofisa utumishi wengi wamekuwa wakijifanya ndio wakurugenzi jambo
ambalo limekuwa likisababisha tatizo la watumishi hewa kuendelea.
Alisema michakato ya maombi ya watumishi inaanza Novemba, hivyo
wakurugenzi wahakikishe wanaletewa ikama wajiridhishe ili wapate
watumishi kulingana na mahitaji. Akizungumzia suala la watumishi hewa,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
George Simbachawene alisema “Hatuwezi kuajiri wakati tuna hewa lazima
tuchambue na kujiridhisha.”
Pia alisema mitandao ya kijamii ni janga kubwa kwani kuna watu
wanatoa taarifa mitandaoni kuwa ni taarifa ya waziri kumbe uongo.
“Utakuta mtu kakataa kaandika speech ya Waziri, kila mtu anayeweza
anachapisha, wapi nilisema walimu wa sanaa hawataajiriwa?” Alihoji.
Alisema hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii watu waliweka
taarifa kuwa Tamisemi inaajiri na watu watume maombi jambo ambalo
lilileta usumbufu mkubwa.
Aidha, alisema watu wanahoji uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga aliyekuwa mtangazaji wa
Clouds Tv, lakini ukweli ni kuwa aliteuliwa kulingana na sifa na uwezo.
Rais ana mamlaka ya kuteua mtu yeyote ambaye anaamini anaweza kufanya
kazi, Wizara hii iko chini ya Rais,” alisema na kuwashangaa watu
wanaobeza uteuzi huo na kutaka wakurugenzi hao wakachape kazi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment