SERIKALI imesema mipango iko mbioni kuzifanya Manispaa za Moshi
mkoani Kilimanjaro na Dodoma kuwa Majiji. Aidha, imefafanua sababu za
kuichelewesha Moshi kuwa Jiji, ikisema haikukidhi matakwa ya kulipa
hadhi hiyo kutokana na udogo wake.
Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa jana bungeni kwa nyakati tofauti na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene na naibu
wake, Selemani Jafo.
Awali, Mbunge wa Moshi Mjini, Japgary Michael (Chadema), alitaka
kujua ni lini Serikali itaitangaza Manispaa ya Moshi kuwa Jiji, kwani
mchakato wa kupata hadhi hiyo ulianza mwaka 2012 na kupitia hatua zote
za kikanuni.
Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu, alitaka kujua mambo
yanayochelewesha mji huo wa kitalii kupewa hadhi ya Jiji. Akijibu, Jafo
alisema ni kweli vikao vyote vya kisheria vimekaa na kuridhia
mapendekezo ya Manispaa ya Moshi, kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya
Jiji.
Hata hivyo, alisema baada ya maombi hayo kuwasilishwa Tamisemi kwa
ajili ya maamuzi, yalirejeshwa ili yafanyiwe marekebisho kutokana na
mapungufu yaliyokuwa yamebainika kulingana na vigezo na taratibu
zilizopo.
Alitaja baadhi ya dosari kuwa na udogo wa Halmashauri ya Moshi, yenye
ukubwa wa kilometa za maraba 58 na kushauriwa iongezwe pia Halmashauri
ya Hai, ili kuifanya Moshi iwe na ukubwa wa kilometa za mraba 132.
Lakini pia, alisema kulipaswa kuwa na mikakati ya mipango miji kulingana
na eneo husika linalopendekezwa kuwa Jiji.
“Hivi sasa timu ya uhakiki kutoka Tamisemi ipo katika uhakiki wa
maombi ya maeneo mapya ya utawala yakiwemo kutoka Manispaa ya Moshi ili
kuhakiki vigezo vinavyozingatiwa katika kuanzisha maeneo hayo, baada ya
kukamilika kwa kazi hii nzima, waziri mwenye dhamana na Serikali za
Mitaa atashauriwa ipasavyo kuhusu maombi haya,” alisema.
Alisisitiza kuwa, vigezo vikifuatwa, hakuna shaka ya Moshi kupewa
hadhi ya Jiji kwani umuhimu wake kiuchumi unafahamika, hasa kupitia
sekta ya utalii.
Aidha, katika swali la nyongeza, Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje
(CCM) alitaka kujua kama Dodoma haikidhi kuwa na hadhi ya Jiji hasa
baada ya Serikali kutangaza uamuzi wa kuhamishia rasmi shughuli zake
mjini humo.
Alisema uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ni kigezo
tosha cha kuipa Manispaa yake hadhi ya Jiji, akiongeza kuwa, ubora wa
miundombinu umekuwa ukiongezeka kila kukicha.
Akijibu, Naibu Waziri Jafo alisema suala la Dodoma kupewa hadhi ya
Jiji, halina mashaka, kwani ni taratibu tu ndizo zinazotakiwa kufanyika
ili kuipa hadhi hiyo. Naye Waziri Simbachawene aliongeza kwa kusema
Dodoma ni lazima iwe na hadhi ya Jiji, kwani lina vigezo vyote vya
kupata hadhi hiyo, akisema mbali ya kuwa mji mkuu wa kiserikali, Dodoma
ni kubwa, ina miundombinu ya uhakika na kwamba juhudi zinafanyika
kuhakikisha inafikia sifa zote za kuwa jiji na hatimaye itangazwe rasmi.
“Kwa kuwa imeamuliwa Dodoma yawe makao makuu ya Serikali, kwa kawaida
na kiutaratibu lazima iwe na mamlaka ya Jiji…sasa unafanyika utaratibu
wa kuamua hivyo…hata kwa ukubwa, Dodoma ina eneo kubwa zaidi na linafaa
na lina sifa zote za kuwa Jiji,” alisema Simbachawene ambaye ni Mbunge
wa Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment