WAKATI vifo vya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera
vikiongezeka na kufikia 17, uongozi wa mkoa huo umesema zinahitajika
zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya waathirika,
na tayari serikali jana imehamasisha na kupatikana zaidi ya Sh bilioni
1.4.
Kati ya fedha hizo zilizopatikana, Sh milioni 700 zilikuwa ahadi,
fedha taslimu Sh milioni 646, Dola za Marekani 10,000, Euro 10,000 na
mifuko 2,800 ya saruji.
Kampuni za mafuta ya Oilcom, GBP na Moil, zimejitolea kujenga shule
mbili za sekondari zilizoathiriwa na tetemeko hilo. Shule hizo
zimefungwa. Jumamosi iliyopita, saa 9.27 alasiri mji wa Bukoba ulikumbwa
na tetemeko la ardhi, ambalo nguvu ya mtetemo wake ulikuwa ni 5.7 kwa
kutumia skeli ya “Ritcher”.
Ukubwa huo ni wa juu kiasi cha kuleta madhara makubwa ikiwemo
kuanguka nyumba, nyingine zimepata nyufa, watu 17 wamekufa, na mamia
wawamejeruhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema, baada ya Kamati ya Maafa
ya Mkoa na Kamati ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wamefanya tathmini ya haraka na kubaini
mahitaji kwa wananchi walioathirika.
Kijuu aliwaomba wananchi, wadau na marafiki walioguswa na janga hilo
katika mkoa na nje ya mkoa, wachangie michango yao kupitia akaunti ya
maafa iliyopo katika benki ya CRDB yenye namba 0152225617300 na kwa
walioko nje watumie Swift code:CORUtztz, huku akiomba watakaowiwa kutoa
wawasiliane na ofisi yake kwa maelezo zaidi.
Alitaja mahitaji ya muhimu ambayo yanahitaji kwa haraka ni dawa, tiba
na vifaa tiba, vifaa vya ujenzi mabati 90,000 yenye gharama ya Sh
bilioni 1.7, saruji mifuko 9,000 yenye thamani ya Sh milioni 162, mbao
zenye thamani ya Sh milioni 450 na misumari yenye thamani ya Sh milioni
12 ambapo jumla ni Sh bilioni 2.3. Majaliwa achangisha bil 1.4/- Wakati
Kijuu akisema hayo, Majaliwa amehamasisha wafanyabiashara pamoja na
mabalozi, kuchangia na kuchangisha zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri
Mkuu Majaliwa alieleza kuwa kutokana na tetemeko hilo kubwa, imelazimu
serikali kuzifunga shule mbili za sekondari zilizoharibiwa vibaya za
Nyakato na Ihungo. Waziri Mkuu alisema tetemeko hilo ni kubwa ambalo
halijawahi kutokea nchini, hivyo haikutarajiwa na wala hakukuwa na
maandalizi ya kukabiliana na hali kama hiyo.
Alisema mpaka jana watu 17 walikuwa wamefariki dunia huku 253
wakijeruhiwa na 145 walikuwa wako katika hospitali huku vitu vingi
pamoja na miundombinu vikiharibika.
Katika miundombinu ya shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na
Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na
mabweni yameharibika kabisa pamoja na hospitali na vituo vya afya navyo
vimeharibika.
Alisema kuna baadhi ya sehemu hali ni mbaya na wanahitaji msaada
ambapo nyumba 840 zimeanguka kabisa chini huku nyumba na majengo 1,264
yakiwa na nyufa na kamati ya maafa katika mkoa pamoja na viongozi wake
wanaendelea kufanya tathmini ya kiasi cha hasara iliyopatikana.
Alisema serikali imefanya juhudi katika kukwamua maisha ya wananchi
wake na mawaziri watatu wako mkoani humo kuangalia namna ya kukabiliana
na majanga hayo ambao ni Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa, Elimu
Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista
Mhagama.
Alisema kupitia kitengo cha maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu
wamefungua akaunti hiyo katika benki ya CRDB huku wakiendelea na
maandalizi ya kupata namba za kuchangia kwa simu ya mkononi huku
akiwashukuru wabunge walioamua kuchangia maafa hayo kwa kutochukua posho
zao za siku ya jana.
Mabalozi, Wafanyabiashara Mkuu wa Jumuiya ya Mabalozi, Balozi wa
Zimbabwe nchini, Edzai Chimonyo alisema kutokana na tarifa hiyo kuwa ya
ghafla na wako sehemu mbalimbali duniani watakusanyika na kuwasilisha
michango yao. Lakini, hata hivyo, balozi mbalimbali zilijitokeza
kuwasilisha michango yao ikiwemo Ubalozi wa China, uliotoa Sh milioni
100, wafanyabiashara wa Kichina walitoa Sh milioni 100 na Ubalozi wa
Kuwait Sh milioni 50.
Pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilitoa
mchango wa wafanyakazi wake Sh milioni 10 huku ikiandaa matembezi ya
kuchangisha fedha zaidi kwa waathirika wa tetemeko hilo yatakayofanyika
Jumamosi wiki hii. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Azizi Mlima alisema
wameanza kwa kukabidhi fedha hizo ambazo ni mchango wa wafanyakazi,
lakini Jumamosi wamealika wadau mbalimbali katika matembezi hayo
watakayochangia zaidi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald
Mengi alisema wafanyabiashara wako pamoja katika kuhakikisha
wanakabiliana na tatizo hilo na kuipongeza serikali kwa hatua za haraka
walizochukua kukabili majanga hayo.
Mengi alichangia Sh milioni 110, Kampuni ya Mohammed Enterprises
(MeTL) kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Mohamed Dewji ilitoa Sh
milioni 100, Kampuni ya Bia (TBL) Sh milioni 100, Chama cha Wauzaji
Mafuta kwa Rejareja Sh milioni 250 huku Umoja wa Waagizaji Mafuta
ukiahidi kuchangia baada ya kikao watakachokaa leo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage alishukuru kwa wafanyabiashara na mabalozi
kwa michango hiyo na kuomba ipatikane kwa haraka ili kusaidia wananchi
wa mkoa huo kurejea katika maisha yao ya kawaida.
RC afafanua zaidi
Kijuu alisema shule za sekondari Ihungo na Nyakato zimefungwa kwa
muda wa wiki mbili kutokana na miundombinu yake kuharibika, ambayo ni
madarasa, vyoo na mabweni baada ya kuta kuanguka au kupata nyufa kubwa
na kuonekana haifai kutumika tena, huku wanafunzi wakiruhusiwa kurudi
katika familia zao baada ya kuonekana kuathirika kisaikolojia.
Alisema Kamati ya Maafa kuanzia sasa, inajenga miundombinu hiyo ndani
ya muda wa wiki mbili ili irudi katika hali yake ya kawaida na
wanafunzi warudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida.
Pia serikali imefanya juhudi za kuleta wataalamu wa afya ambao ni
madaktari bingwa sita kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando
iliyoko jijini Mwanza ili kutoa msaada kwa wagonjwa wanaohitaji msaada
zaidi wa kitabibu huku Ubalozi wa nchi ya China ukileta waganga wa
kusaidia matibabu kwa waathirika hao.
Aidha, katika uchunguzi uliofanywa na wataalamu kutoka Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST) kuhusu tetemeko hilo, walibainisha sababu kuwa
ni kitovu cha tetemeko hilo kuwa kiko chini sana ya ardhi kwa kutafsiri
umbile la tetemeko hilo lililonakiliwa na vituo vya kupima matetemeko ya
ardhi ambapo inaonekana kuwa limetokana na misuguano ya mapande makubwa
ya ardhi iliyopasuliwa mithili ya mipasuko kwenye Bonde la Ufa.
Pia Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hasa
wataalamu kutoka GST wameandaa vituo mbalimbali katika mkoa ili kutoa
elimu jinsi ya kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari kabla ya tetemeko,
wakati wa tetemeko na baada ya kutokea ili kujizoesha kwani mara nyingi
wakati wa matukio kama ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua
uamuzi wa haraka kujinusuru kwamba wafanye nini. Taarifa ya serikali
bungeni
Akisoma taarifa ya serikali bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi), George Simbachawene
kwa niaba ya Waziri Mkuu, alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.7
katika vipimo cha “Ritcher”, kufikia jana lilisababisha vifo vya watu 17
na kujeruhi watu 252, kati yao 169 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Alisema nyumba za makazi zilizoanguka ni 840 huku nyumba za makazi
zenye nyufa zikiwa 1,264 na majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka
ama kupata nyufa ni 44. Kutokana na athari hizo, serikali imetangaza
kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo ya kuokoa na kuwapeleka hospitalini
waathirika kwa ajili ya matibabu.
Imewapatia pia makazi ya muda baadhi ya wananchi ambao nyumba zao
zimeathirika. Serikali pia imeongeza nguvu ya madaktari bingwa 15 kutoka
mkoani Mwanza ili wasaidie kutoa huduma za haraka kwa waathirika, huku
ikiwahamasisha wananchi wasaidiane kila inapowezekana.
Alisema serikali pia imeelekeza wanajiolojia kutoa maelekezo ya kisayansi ili kuwatoa hofu wananchi kuhusu hali hiyo.
Taarifa hiyo imesema Serikali inaendelea kuhakikisha hatua za dharura
zinachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa hatua
za muda mfupi na muda mrefu zinatambuliwa na kutekelezwa ili kuwasaidia
waathirika.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya
athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi. Kutokana na janga hilo,
serikali imewaomba wadau wa ndani na nje wanaotaka kuchangia waathirika,
wawasiliane moja kwa moja na Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Maafa ya
Mkoa wa Kagera, huku ikionya watu kuacha kutumia maafa hayo
kujinufaisha.
“Wananchi mnaombwa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na
Serikali katika kutatua tatizo ambalo limeipata nchi ili wananchi
waendelee kupata huduma kulingana na athari za tetemeko,” alisema
Simbachawene.
Wabunge waunga mkono
Kutokana na kuguswa na tukio hilo, wabunge jana waliunga mkono juhudi
za Serikali na wameridhia kwa kauli moja kukatwa posho yao ya siku
moja, sawa na Sh 220,00 kila mmoja ili kuchangia maafa hayo.
Bunge lina wabunge 389.
Uamuzi huo ulitokana na hoja ya Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi
(CCM) aliyeomba Bunge liahirishe mjadala uliokuwa mezani wa Muswada wa
Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 na Muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Wataalamu wa Kemia 2016 ili kujadili tukio la tetemeko la
ardhi Kagera ambalo ni la dharura.
Alipendekeza pia wabunge wajadili kwa muda wa nusu saa suala hilo
pamoja na kuchangia posho yao ya siku moja. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
alipokea ombi la Shangazi na kusema kuwa ataruhusu mjadala huo kwani
kanuni zinaruhusu.
Hata hivyo, alisema kitakachojadiliwa ni hoja ya dharura na mchango
wa wabunge, lakini sio kujadili Kauli ya Serikali kuhusu tetemeko hilo
iliyotolewa na Waziri Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
(Chadema) alionesha utovu wa nidhamu mbele ya Bunge na Naibu Spika kwa
kumnyooshea kidole Dk Tulia jambo lililofanya avunje Kanuni ya 74
inayomtaka mbunge kutoonesha dharau yoyote kwa aliyekalia kiti cha
uongozi bungeni.
Mdee atia doa Naibu Spika alimkanya Mdee, akisema, “Mheshimiwa Halima
Mdee acha kuninyooshea kidole, acha kunyoosha vidole, huo ni utovu wa
nidhamu kwa kiti… hebu Halima Mdee uwe na heshima kidogo, hebu kuwa na
heshima kidogo.”
Baada ya kauli hiyo ya onyo, Halima alionekana kususa na kutoka nje
ya Bunge wakati wabunge wakianza kujadili hoja ya dharura iliyoletwa
mezani na Shangazi. Akichangia Shangazi alianza kwa kupendekeza wabunge
kuchangia posho yao ya siku hiyo ambayo ni Sh 220,000 ili kuwafariji
wananchi waliopatwa na tatizo la tetemeko hasa manispaa ya Bukoba.
“Tunamshukuru Mungu tukio limetokea mchana, kama ingekuwa usiku
huenda maafa yangekuwa makubwa zaidi. Tukio hili litufunze kuweka kanda
maalumu zinazoshughulikia maafa ili tatizo linapotokea litatuliwe
haraka,” alisema.
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alisema tukio hilo la
tetemeko liwaunganishe wabunge wa kambi zote, kwani Bunge ni chombo cha
wananchi na kutaka wabunge bila kujali itikadi kusaidia kuielekeza
serikali nini cha kufanya kukabiliana na maafa hayo.
Aliunga mkono hoja kuchangia posho ya siku ya jana, ingawa alisema
tayari kwa upande wao wapinzani walishachangishana Sh 100,000 kila mmoja
kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tukio hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu (CCM) naye aliunga mkono hoja ya
kuchangia posho yao ya siku na kuongeza suala hilo limegusa hisia za
watu na kuonya wanasiasa kutotumia maafa hayo kujiinua kisiasa.
Vullu aliipongeza serikali kwa juhudi zake tangu kutokea kwa tukio
hilo, lakini alisisitiza haja ya kutolewa elimu zaidi ya kukabiliana na
maafa na njia za kuokoa watu yanapotokea matukio ya dharura kama hilo la
tetemeko la ardhi.
Mbunge wa Muleba, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) alisema ametoka Bukoba
na kwamba ameshuhudia hali ilivyo mbaya katika maeneo yaliyoathirika na
tetemeko hilo na kuongeza kuwa ni mkono wa Mungu tu ndio umeepusha
maafa kuwa makubwa zaidi.
Alisema suala hilo sio la kisiasa na kwamba wananchi wanahitaji
faraja na kutaka kama taifa Watanzania wawe wamoja bila kujali itikadi
zao na kutaka tathmini ifanywe kitaalamu zaidi.
Alitaja baadhi ya maeneo aliyotembelea na kujionea athari kubwa
ikiwemo Manispaa ya Bukoba, ambapo alisema kati ya nyumba 10 tatu
zimeharibika kabisa, hivyo inahitajika tathmini ya kitaalamu sana ili
kubaini iwapo eneo husika linafaa tena kujenga au watu wanatakiwa
kuhama.
Mbunge wa Buchosa ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk
Charles Tizeba alisema tetemeko limeleta uharibifu mkubwa katika mkoa
wa Kagera ingawa maeneo mengine yameguswa ikiwemo Mwanza, Geita na
Shinyanga.
Mara baada ya wabunge hao kumaliza kuchangia, Naibu Spika Dk Tulia
alilihoji Bunge ambalo kwa pamoja liliunga mkono kutoa posho kwa ajili
ya kuchangia waathirika wa tetemeko Bukoba.
Akishukuru kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwashukuru wabunge kwa kutoa mkono
wa faraja na kuungwa mkono na Bunge zima.
“Hili ni jambo letu sote, kwani ni utamaduni wa Watanzania kusaidiana
na kuchangiana yanapotokea majanga kama haya. Serikali inaahidi mchango
wenu utawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali inalichukulia suala hilo kwa ukubwa wake na
ndio maana, Rais John Magufuli aliahirisha safari ya kikazi Lusaka,
Zambia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yuko Dar es Salaam akikutana na
wataalamu na wadau wa ndani na kimataifa kuona namna gani walikabiliana
na maafa ya tukio hilo.
Athari Bukoba
Alisema Manispaa ya Bukoba ndiyo iliyoathiriwa zaidi, kwani imepoteza
watu 15 waliokufa kutokana na tetemeko hilo, huku majeruhi wakiwa 142
kati ya 252. Aidha, nyumba 753 zimeanguka katika Manispaa ya Bukoba
pekee, huku nyumba 1,037 zikipata nyufa.
Kwa upande wa taasisi alisema, shule kongwe ya Sekondari Ihungo
imelazimika kufungwa kutokana na uharibifu mkubwa, kwani tetemeko
limeangusha ukumbi wa shule, bweni moja huku mengine sita yakitajwa
kuharibika vibaya na kutofaa kukaliwa na wanafunzi.
Aidha, madarasa 16 yamebomoka, huku vyoo 25 vikiharibiwa sambamba na
mabafu mawili. Nyumba tatu za walimu zimeanguka na nyingine 17 zikipata
nyufa.
Taarifa hiyo imeeleza kanisa na msikiti shuleni hapo vimebomoka,
wakati maabara tatu zimepata nyufa ilhali mtego wa Radi moja umeanguka.
Shule nyingine iliyofungwa ni Nyakato ambayo mabweni yake sita
yameharibika na hayawezi kukaliwa huku mengine manane yakipata nyufa.
Aidha, vyumba vitano vya madarasa vimeharibika na vingine 15 vikipata
nyufa. Pia tetemeko limeharibu jengo moja la utawala, nyumba nane za
walimu ambazo hazifai kutumia wakati nyingine 17 zimepata nyufa. Athari
za tetemeko zimezikumba pia halmashauri za wilaya ya Bukoba, Missenyi,
Muleba, Karagwe na Kyerwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment