MBUNGE wa Manonga mkoani Tabora,
Seif Gulamali (CCM), ametoboa siri jinsi wabunge wanavyojikuta wakiingia
katika mtego wa rushwa ili kushawishi kupitishwa kwa baadhi ya hoja
bungeni.
Ingawa katika miaka ya karibuni, wabunge wamekuwa wakihusishwa na tuhuma za kupokea rushwa kwa nia ya kufanikisha au kuficha jambo wanalolisimamia, Gulamali ndiye mbunge pekee aliyeripoti bungeni viashiria vya rushwa kwa watunga sheria hao katika siku zote 73 za Bunge la Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 lililoanza Aprili 19 na kumalizika Juni 30, mwaka huu.
Mei 20, mwaka huu, wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, mbunge huyo alidai baadhi ya wabunge walikuwa wamehongwa kuutetea bungeni mfumo wa vinasaba unaotumika katika upimaji wa mafuta.
Akichangia mjadala huo, Gulamali alieleza kushangazwa na baadhi ya wabunge waliokuwa wanatetea vipimo hivyo, huku akiweka wazi kuwa alikuta karatasi kwenye meza yake bungeni zikiwa na maelezo ya kutetea vipimo hivyo.
Wakati uongozi wa Bunge bado haujatoa taarifa yoyote kuhusu tuhuma za rushwa kwa wabunge zilizotolewa na Gulamali takribani miezi minne iliyopita, mbunge huyo katika mahojiano maalum na Nipashe mjini hapa juzi alieleza jinsi alivyoshtukia kuingizwa kwenye kadhia ya rushwa na kutetea vitu bungeni bila kuvijua kiundani.
Katika miaka ya karibuni tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge zimekuwa zikiibuka mara kwa mara.
Mathalani katika Bunge la 10, Spika Anne Makinda, kuna wakati alilazimika kuvunja baadhi ya kamati za bunge baada ya kuibuka kwa madai hayo.
Swali: Katika Bunge la Bajeti mwaka huu, ulilalamika kwa Naibu Spika kwamba baadhi ya wabunge walikuwa wanakushawishi kushupalia suala la vinasaba katika upimaji wa mafuta na ukaweka wazi kwamba baadhi yao walikuwa wamehongwa. Ulipataje utashi huu?
Jibu: Unajua, sisi ni wabunge. Jukumu letu kwanza ni kuwakilisha wananchi. Pili, kuisimamia serikali. Kwa hiyo, unapokuwa mbunge, unatakiwa kuisaidia serikali. Usipotekeleza hicho maana yake hufanyi kazi yako ipasavyo.
Utekelezaji wa usimamizi wa mbunge unakuwa na manufaa kwa mbunge, diwani na hata kwa Rais.
Na Rais amekuwa akituomba sana wabunge tumsaidie. Anasema tumuombee. Sasa anapofanyiwa `figisufigisu’, wa kumsaidia ni sisi wabunge.
Kuna wakati mwingine unaweza kuletewa taarifa za udanganyifu na wewe ukafanya uamuzi kupitia taarifa hizo. Mwisho wa siku, unapotoka na kupotosha taifa.
Niliamua kusema vile bungeni kwa sababu suala hilo linatetea na baadhi ya wabunge wa CCM, hata wabunge wa upinzani walikuwa hawajui chochote kilichokuwa kinaendelea.
Nikaona nitimize wajibu wangu wa kuisaidia serikali bila kuegemea upande wowote. Niliona kuna watu wanafaidika, watu wanapokea rushwa kwa sababu leo nikija nikakwambia ulipe faini ya Sh. milioni tano, kisha unasema huna kiasi hicho cha fedha, unaamua kunipa Sh. milioni mbili, na ninaichukua bila kulipa risiti. Hapo serikali imepata hela?
Sasa wenye maslahi hayo, walitaka kutumia mwanya huo, kuwatumia wabunge kupenyeza mambo yao kwenye bajeti ya serikali ili waendelea kupiga dili. Kwa hiyo, nikamwomba waziri (Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sosper Muhongo).
Kilichonishtua zaidi, hata waliokuwa wanaunga mkono suala hilo, nilipowafuata nje ya ukumbi wa bunge kunipa ufafanuzi, walisema hawajui chochote.
Kwa hiyo, baadhi wanatumwa kuja bungeni kuzungumza vitu ambavyo hawavijui. Sasa unajiuliza huyu mbona amezungumza hapa bungeni, unapomuuliza akupe ufafanuzi zaidi, hajui? Wabunge wanakaririshwa vitu ambavyo hawajui maana yake.
Waziri alienda kukaa na Ewura pamoja na wafanyabiashara na kubaini tatizo, kumbe nilichokizungumza bungeni ni kweli. Wameyachakata huko na kuyamaliza wenyewe.
Nilipata utashi wa kulisema suala hilo bungeni kwa sababu mimi ni mtu mwenye msimamo. Napinga rushwa, nimeipiga vita rushwa nikiwa shule, chuo ambako nilikuwa rais wa wanafunzi.
Nimeongoza mapambano dhidi ya watu wanaokandamiza elimu ya juu. Misimamo yangu kote nilikopita inajulikana. Sipendi kukandamiza haki za watu. Napenda walio wengi wanufaike.
Swali: Huu ni muhula wako wa kwanza bungeni, kesi za kuomba upokee kitu kidogo ili ushupalie jambo fulani zimekukumba mara ngapi hapa bungeni?
Jibu: Tangu kipindi kile cha Bunge la Bajeti sijawahi kukutana tena na tukio la aina hiyo. Pengine kwa sababu msimamo wangu umeshajulikana. Watakuwa wanahofu pengine kwamba wakinishirikisha nitawaumbua hadharani.
Mimi ninataka nikichangia jambo, lazima niwe nalijua kwa kina. Ni heri wasinishirikishe kabisa kwenye masuala hayo.
Swali: Ni watu wapi hasa wanaotumika kupenyeza kitu kidogo kwa wabunge ili kushupalia baadhi ya hoja? Je, ni mawaziri, wabunge, makatibu wakuu wa wizara au wapi hasa?
Jibu: Unaweza kuona wabunge wenyewe wanapasiana (wanapeana) vitu, lakini kwenye Bunge la Bajeti sikuona sana tabia hiyo tofauti na zile karatasi.
Hata hivyo, wabunge hasa wale wakongwe hapa bungeni walinifuata na kuniambia nimekuja bungeni katika kipindi kibaya sana, nimekosa mengi.
Sasa najiuliza hayo mengi sijui ni yapi. Na sisi tunaendelea kukosa mengi hivyo hivyo.
Nilikabidhi zile karatasi kwa Naibu Spika, wao ndiyo wanajua nani alipenyeza kitu hicho kwa wabunge. Kama walifuatilia, watakuwa wanajua kilichokuwa kimelengwa na wahusika.
CHANGAMOTO WABUNGE WA MAJIMBO
Swali: Kuna changamoto zipi ambazo ninyi wabunge wa majimbo ya vijijini mmekuwa mkikumbana nazo katika utekelezaji wa shughuli zenu?
Jibu: Kuna dhana imejengeka miongoni mwa wabunge kwamba unapotembelea jimbo la kijijini lazima uende na furushi la fedha, lakini ukweli ni kwamba wananchi wa maeneo hayo wanahitaji msaada mkubwa zaidi tofauti na fedha za mbunge.
Kuna eneo lilitembelea nikakuta mwenyekiti wa kijiji amejigeuza mfalme. Kile kijiji kilikuwa hakijawahi kutembelewa na mbunge wala kiongozi yeyote wa juu serikalini. Yule mwenyekiti alikuwa anafukuza mtu yeyote. Anatoza faini anazoona yeye inafaa na wanamuogopa.
Kibaya zaidi, akauza hadi eneo la shule. Mwalimu Mkuu alipombishia kuuza eneo hilo, naye akapewa siku saba aondoke katika kijiji hicho akafanye kazi sehemu nyingine. Wananchi wanaonewa sana kule vijijini. Kuna kijiji nilikuta mtu amenyang'anywa shamba lake halali na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani. Yaani, shamba lake, lakini anafungwa jela. Ni uonevu mkubwa.
Swali: Kitaaluma wewe umesomea masuala ya uchukuzi. Una mtazamo upi kuhusu hali ya sekta hii ilivyo nchini kwa sasa?
Jibu: Usafirishaji ndicho kiini cha uchumi wa nchi yoyote duniani. Huwezi kukuza uchumi bila kuwa na sekta hii. Hata mtalii hawezi kuja Tanzania bila usafiri. Ukizungumzia dhahabu, lazima uguse usafirishaji. Sekta hii ni muhimu mno, ndiyo uti wa mgongo na roho ya uchumi wa nchi yoyote duniani.
Sekta hii ikiyumba, uchumi wa nchi pia lazima uyumbe. Tayari tumeanza kuona kitu kama hicho hapa kwetu (Tanzania). Wakati tunaanza awamu hii ya tano, ilionekana bandarini kukiwa na mizigo feki mingi ambayo ilikuwa hailipiwi ushuru.
Sasa ukidhibiti mianya, wale waliokuwa wanaifanya, wanaathirika kisaikolojia. Na inabidi waanze kujiuliza, maana yake hapo wanaacha kuleta mizigo.
Kwa hiyo, sekta yetu imeshuka lakini naamini Rais wetu ameliona hilo. Tunawaomba wadau wa bandari kwa maana ya wafanyabiashara, bandari na TRA wakae kutatua changamoto zilizopo. Wafanyabiashara wanalalamikia kuongezeka kwa kodi. Hakuna nchi ambayo inaweza kuendesha uchumi wake bila wafanyabiashara.
Swali: Ndege ya kwanza kati ya nne ambazo serikali ya awamu ya tano imepanga kuzinunua itatua nchini Septemba 19, lakini baadhi ya mashirika yaliyowekeza kwenye sekta hiyo yameanza kupunguza wafanyakazi na hata kuleta ndege za kubeba watu wachache zaidi. Je, tutaweza kushindana na mashirika haya na kufufua shirika letu la ndege?
Jibu: Nimezungumza hapo awali kuhusu kutokea kwa mtikisiko wa sekta ya usafirishaji nchini. Watu bado hawajazoea na kujua serikali mpya inataka nini. Naamini ndege zinazoletwa na serikali kwa ajili ya usafiri wa ndani zitakuwa za abiria wachache na zitatumia gharama kidogo kuzisimamia, hivyo kuhimili ushindani dhidi ya mashirika yaliyopo.
HALI YA TABORA
Swali: Mkoa wa Tabora ulikuwa unasifika kwa uzalishaji wa pamba,lakini sasa hausikiki tena. Kulikoni Mheshimiwa Mbunge?
Jibu: Kwanza tulikuwa na kiwanda kikubwa cha Manonga ambacho kilikuwa kinasaidia masuala ya pamba, mafuta, mbegu.
Kiwanda kikongwe katika nchi hii. Baada ya serikali kukibinafsisha kwenda kwa Rajan na Igembesabho, walikiendesha kwa miaka minne, mitano hivi lakini kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao la pamba kukasababisha gharama za kukiendesha kuwa kubwa, ikabidi kifungwe.
Sasa kufufua kiwanda hicho ni ahadi yangu. Pia ni ahadi ya Rais. Tumewatafuta Rajan na Igembesabho na kukaa nao. Rajan wako tayari kukiachia kile kiwanda kwa kukiuza kwa Sh. bilioni 1.5, lakini Igembesabho bado ana nia ya kukiendesha.
Tumemuomba waziri mwenye dhamana aingilie kwa kuzikutanisha pande husika kwa sababu Igembesabho wako tayari kuwapa Rajan Sh. milioni 700, lakini Rajan naye anataka faida maana kimekaa muda mrefu na alitoa Sh. milioni 700 kukinunua kipindi kile.
Niombe waziri alichukulie hili suala hili kufufua kilimo cha pamba katika mkoa wa Tabora maana kimeshuka sana kutokana na ujanjaujanja mwingi.
Swali: Takwimu za Benki ya Dunia zilizotolewa mwanzoni mwa mwaka huu, zinaonyesha katika kila saa moja, kunatokea vifo viwili vitokanavyo na uzazi nchini. Hali ya huduma za afya ikoje jimboni kwako?
Jibu: Ni kweli, bado kuna changamoto ya vifo vya uzazi nchini, lakini vingine vinatokea kwa sababu ya uzembe tu wa watumishi wa sekta ya afya. Kuna siku nilitembelea kituo chetu cha afya pale Chama cha Nkola.
Kuna kina mama niliwakuta walikuwa wametoka maeneo ya mbali sana na nilipowauliza waliniambia walifukuzwa kwenye zahanati za maeneo yao. Kuna baadhi ya watumishi wa afya ni wazembe tu.
Manonga tumejitahidi sana kutekeleza ahadi ya kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati. Tuna vijiji 65, vijiji 40 tayari tumeshajenga majengo kwa ajili ya zahanati, lakini changamoto iliyopo ni uhaba wa wataalamu na nyumba za kuishi wataalamu hao.
Tuna uhaba mkubwa wa madaktari na halmashauri imesema ajira zao zinatoka serikalini.
Kila kijiji nimetumia mfuko wa jimbo kuhakikisha kinapata mabati, simenti na nondo. Zahanati 15 tumezipatia umeme wa jua na tumejipangia mwaka mmoja tu zahanati zote zinazofanya kazi lazima ziwe na umeme.
Pia tumepata vifaa vya upasuaji kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, badala ya kwenda Igunga sasa upasuaji unafanyika kwenye kituo chetu cha Choma cha Nkola. Tunachokifanya sasa ni kuboresha kituo kwa kuongeza wodi na wataalamu.
Swali: Tabora ni miongoni mwa mikoa muhimu nchini katika uzalishaji wa mpunga. Katika jimbo lako kuna mradi wa kilimo cha umwagiliaji kwenye eneo lote linalopitiwa na Mto Manonga, lakini kuna kipindi ulikwama. Hali ya mradi huo ikoje kwa sasa?
Jibu: Tulikuwa na miradi miwili ya umwagiliaji, mmoja uko Choma cha Nkola na nyingine ipo pale Buhekela, lakini katika mvua za mwaka jana miradi hii ilikumbwa na uharibifu mkubwa kiasi cha kunilazimu kuingia mfukoni kutoa fedha za kuitengeneza.
Tulitengeneza lakini si katika kiwango kinachotakiwa, tulifanya mradi tu maji yale hayapotei na kutuacha na njaa kali. Mvua ilikuwa kubwa, ikabomoa tena upande mwingine.
Bajeti ya mradi wa Choma ilikuwa Sh. milioni 100 na ile ya Buhekela ilikuwa Sh. milioni 60. Tuliliweka suala hilo kwenye bajeti ya halmashauri, lakini mpaka sasa pesa hazijatoka. Masika yanakaribia, nimeongea na mkurugenzi ili tusake mzabuni ili atengeneze kwa deni, tutamlipa zitakapotoka. Waziri wa Maji na Umwagiliaji pia amekubaliana na pendekezo hili la mzabuni.
Mbuga ile inategemewa na watu zaidi ya 2,000. Sasa tuna mpunga mwingi ambao umekosa soko kutokana na serikali kuzuia kuuza mazao nje ya nchi.
Swali: Vipi kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama jimboni kwako?
Jibu: Hali si nzuri na hili ni tatizo la karibu kila jimbo maana kila mbunge anasema maji, maji, maji! Tunashukuru kuna mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria unapita Tabora ambao ni wa fedha za mkopo kutoka India zaidi ya Dola milioni 265 na ujenzi wake unaanza mwaka huu. Baadhi ya maeneo ya jimbo letu yatapitiwa na mradi huo, hivyo kunufaisha wananchi ambao wanaishi maeneo ya karibu na bomba litakapopita.
Kuna kata zangu tatu za Ziba, Ibologelo na Nyandekwa zitapata maji katika mradi huu wa miaka miwili. Utaratibu uliopo ni kwamba watu wanaoishi kilomita 12 kutoka kwenye bomba katika pande zote, wanapatiwa maji. Tuna ahadi ya Makamu wa Rais ya kutupatia majisafi na salama ambayo pia tunaisubiri.
KAULI UONGOZI WA BUNGE
Alipoulizwa na Nipashe nje ya ukumbi wa Bunge mjini hapa jana mchana hatua walizochukua kuhusu madai ya Mbunge Gulamali, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alidai suala hilo alilitolea ufafanuzi siku hiyo hiyo (Mei 20, mwaka huu).
"Ni kweli nilimwagiza (Gulamali) akabidhi katarasi kwenye Kiti cha Spika na alifanya hivyo na suala hilo nililitolea ufafanuzi siku hiyo hiyo," alisema Dk. Tulia.
Hata hivyo, Nipashe inafahamu kuwa hapakuwa na maelezo mengine yaliyotolewa bungeni siku hiyo zaidi ya kauli ya Profesa Muhongo kukutana na wafanyabiashara wa mafuta na Ewura jijini Dar es Salaam wiki lililokuwa linafuata.
Nipashe.
0 comments:
Post a Comment