Katika
kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa shuleni na hatimaye kumaliza masomo
yao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) limetenga Dola 1,605,000 ambazo ni zaidi ya Bilioni 3 za
Kitanzania ambayo zitatumika kuwasaidia watoto wa kike nchini kurejea
katika shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo.
Akizungumzia mradi
huo, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodriguez
alisema kuwa Tanzania bado inaonekana kuwa na tatizo la watoto wa kike
kuachishwa masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kupata mimba
za utoto na ndoa za utotoni hivyo kupitia mradi huo wataweza kuwasaidia
watoto hao kuendelea na masomo.
Bi. Rodriguez alisema UNESCO imeamua
kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuwasaidia watoto wa kike
kurejea masomoni na utafanyika kwa uhakika bila kumwacha mtoto yoyote na
wana matumaini utaweza kusaidia watoto wa kike ambao wamekatishwa ndoto
zao kimaisha kutokana na kukatishwa masomo.
"Tanzania kuna tatizo la
watoto wa kike kusahaulika katika elimu na UNESCO imejitoa kushirikiana
na serikali ya Tanzania ili kusaidia kukuza elimu ya watoto wa kike,
"Baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuchangia ni pamoja na mambo ya
asili, wamekuwa wakiwaozesha ndoa za utotoni na na watoto wengine
wamekuwa wakipata mimba za utoto na hivyo kuacha masomo … mradi huu ni
wa uhakika na utasaidia kukuza elimu," alisema Bi. Rodriguez.
Kwa
upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi.
Maimuna Tarishi alisema serikali inafahamu kuwepo kwa changamoto hizo na
imekuwa ikifanya jitihada ili kuhakikisha kuwa matatizo ya watoto wa
kike kukatishwa masomo yakimalizika.
Alisema kuwa makabila mengi ya
Tanzania yamekuwa yakiwaona watoto wa kike kama watu wa kukaa nyumbani
na kulea watoto lakini kama jamii ikiwa na mtizamo tofauti na
kuwawezesha watoto wa kike basi wanaweza kusaidia nchi kukuza uchumi.
"Tumeona
kazi ambayo wameifanya UNESCO hata machifu huko Ngorongoro wameanza
kuelewa umuhimu wa watoto wa kike kuwa shuleni na kwa mpango huu
matarajio ya serikali ni kumaliza changamoto iliyokuwepo awali,
"Serikali
inafahamu kuna changamoto nyingi ambazo zinawakuta watoto wa kike na
sio katika elimu pekee bali ni maeneo mengi … serikali inataka kukuza
thamani ya elimu kwa watoto wa kike ambao wengi wao wanakatishwa kwa
sababu ya mimba na ndoa za utotoni," alisema Bi. Tarishi.
Nae Afisa
Mradi wa Maswala ya Afya ya Uzazi kwa Vijana (UNFPA), Fatina Kiruviya
alisema mradi una malengo ya kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa shuleni
na kwa kuanza wanataraji kufanya mradi Ngorongoro, Pemba, Geita na
Sengerema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment