Wanachama
wa Chama cha Wananchi (CUF) wamesema wapo tayari kugharamia matibabu
ya Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim Seif Sharif Hamad.
Tamko hilo
limetolewa siku chache baada ya kuibuka taarifa kuwa kiongozi huyo
amesusa gharama za matibabu zinazotolewa na Serikali ingawa ni haki yake
kwa mujibu wa sheria kama kiongozi mstaafu.
Akizungumza kwa niaba
ya wanachama wenzake kisiwani Unguja jana, mmoja wa wanachama wa CUF,
Ali Abdallah Issa, alisema wanashangazwa na baadhi ya watu kumpiga na
kumsema kiongozi huyo ambaye alidai ni kiungo muhimu katika
kuwaunganisha Wazanzibari.
“Maaalim ana haki zote za kuhudumiwa na
Serikali na si vinginevyo. Lakini kwa manyanyaso na kusimangwa kila
kukicha sisi wanachama wa CUF tupo tayari kugharamia matibabu ya
kiongozi wetu.
“Na hili si jambo geni, Maalim alikamatwa na kuwekwa
kuzuizini. Je, alipotoka alikuwa akitibiwa na SMZ? Jibu ni hapana ni
fedha zake mwenyewe binafsi pamoja na wana CUF ambao walikuwa mstari wa
mbele kumhudumia kiongozi wetu nasi sasa tutafaya hivyo ikiwa SMZ
imeshindwa,” alisema Ali.
Alisema kitendo cha Maalim Seif kusafiri nje ya nchi kwa matibabu bila ya huduma za Serikali hakileti picha nzuri.
Kuna hatari visiwa vya Zanzibar vikaingia katika mgogoro na kujengeka chuki hasa kati ya CUF na CCM, alisema.
‘’Iwapo
Maalim Seif amekwenda kwenye matibabu kwa gharama zake binafsi basi
inasikitisha sana kuona ni jinsi gani Katiba inavyoanza kukiukwa na kwa
kweli si jambo jema na halifai,” alisema.
Naye Is-hak Said Makame,
alisema Zanzibar imepita katika wakati mgumu hasa baada ya kutokea
migogoro ya siasa iliyotokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka
jana na ule wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.
“Maalim
hawezi kusemwa na hata kuonekana ni kiongozi anayetibiwa kwa fadhila
kama alivyotaka Rais Magufuli alipokuja hapa Unguja kwenye mikutano
yake. Sasa tunasema sisi CUF tutamlinda kiongozi wetu kwa hali na
mali,”alisema Makame.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Biman kujua Maalim Seif amepata wapi
fedha kwa ajili ya safari ya nje ya nchi kutibiwa.
Alisema hajui ni wapi kiongozi huyo alipopata fedha za matibabu.
“Katibu
Mkuu amekwenda India kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake
lakini nasi hatujui ni wapi amepata fedha. Ila atakaporejea nchini
itatolewa taarifa kwa kina kuhusu suala hili,” alisema Biman.
Maalim Seif yuko India na anatarajiwa kujerea nchini siku chache zijazo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment