WANAWAKE 12,581 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi
mkoani Mbeya katika kipindi cha kuanzia mwaka 2012 hadi Juni 2016.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Seif Mhina, kati ya
wanawake hao waliofanyiwa uchunguzi, 1,483 walibainika kuwa na dalili za
awali za ugonjwa huo na kati yao 803 walipatiwa tiba mgando na wengine
246 walioonekana kuwa na dalili za saratani na walipewa rufaa kwenda
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
matibabu.
Alibainisha hayo jana alipofungua mkutano wa siku tatu wa
uraghibishaji kuhusu saratani ya shingo ya kizazi unaofanyika mkoani
Mbeya unaohudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya ya uzazi mkoani humo
ukiwa umeandaliwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Chama
cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA).
Alisema huduma zilizofanyika katika kipindi hicho zimetokana na
ushiriki wa karibu wa wadau mbalimbali, likiwemo Shirika la Watu wa
Marekani linalojishughulisha na Mapambano dhidi ya Ukimwi la Watereed
lililofadhili katika kufundisha watumishi na kununua vifaa.
Alisema kutokana na ufadhili wa Watereed hadi sasa mkoani Mbeya vituo
18 vinatoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na mwezi
uliopita vituo 36 vimefundishwa na sasa watumishi wanasubiri kupewa
vifaa mapema mwezi ujao ili waanze kutoa huduma.
Mratibu wa Mradi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi kutoka Wama, Dk
Sarah Maongezi alisema lengo ni kuhamasisha timu za afya za mikoa ya
Mbeya, Mwanza, Iringa, Mbeya na Mara na wilaya zake na kuona mafanikio
yaliyopatikana kutokana na mikakati iliyowekwa mwaka 2014.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment