Ni Mpambano. Ndivyo unaweza kusema hasa baada ya Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kutarajiwa kuripoti
ofisini kwake Buguruni Dar es Salaam huku Mwenyekiti wa chama hicho
aliyerejeshwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba,
akitangaza kumpokea kiongozi huyo.
Hatua hiyo inatokana na maswahiba hao wa miaka mingi kugeuka
maadui ambao kwa sasa ‘hawapikwi chungu’ kimoja hata kufikia kufukuzana
ndani ya chama hicho.
Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Uhusiano wa Umma, Mbarara Maharagande, alisema kesho 30 Septemba 2016 Maalim
Seif ataripoti ofisini kwake Buguruni akisindikizwa na wanachama na
viongozi wa chama hicho.
Alisema mapokezi hayo yatawajumuisha wanachama wa CUF wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na wabunge.
Katika mapokezi hayo watawakaribisha wajumbe wa Baraza Kuu Ofisi Kuu
ya CUF Buguruni baada ya kumaliza kazi kubwa ya kutengeneza mustakabali
wa chama.
“Wanachama wa CUF wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na
wabunge wote wa CUF, wameandaa mapokezi haya makubwa yatakayofanyika
kesho Ijumaa Septemba 30 kuanzia saa 2.00 asubuhi.
“Watawakaribisha wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa katika Ofisi Kuu za CUF Buguruni.
“Wajumbe hao watakuwa wanatoka Zanzibar kwenye kikao maalumu
kilichotengeneza mustakabali muhimu wa chama na mameya wa CUF,
madiwani, Kamati ya Uongozi ya chama, Katibu Mkuu (Maalim Seif) wote
watakuwapo.
“Mbali na hao pia watakuwapo wakurugenzi, wajumbe wa Bodi ya
Wadhamini ya chama na watu muhimu ambao kwa pamoja watafika Buguruni
na kuanza kazi,” alisema Maharagande
Kauli ya Lipumba
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa
Lipumba alisema atampokea Maalim Seif siku yoyote atakayofika na
pamoja na mambo mengine atapanga naye mikakati ya ujenzi wa chama.
Alisema CUF inamtambua Maalim Seif kama Katibu Mkuu, hivyo basi
hawezi kumtenga atakapofika kwenye ofisi hizo zilizopo Buguruni kwa
sababu kuna ofisi yake ya kufanyia kazi.
“Namsubiri Maalim Seif aje kwenye ofisi zetu za Buguruni ili tukae na
kukijenge chama kwa sababu anatambua kuwa mimi ni mwenyekiti halali kwa
mujibu wa Katiba yetu. Kinachojitokeza sasa ni migongano ya siasa
ambayo inaweza kumalizika wakati wowote.
“Naamini siku atakayokuja tutampokea na kumpeleka ofisini kwake kwa
ajili ya kuchapa kazi, lakini pia nitampa mwongozo wa namna ya kukijenga
chama ikiwa ni pamoja na kumwambia kuwa fedha zisitutenganishe,”alisema
Prof. Lipumba.
Akizungumzia kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika Visiwani Zanzibar
ambacho pamoja na mambo mengi kilitangaza kumvua uanachama, a alisema
kikao hicho ni batili na kimekiuka katiba ya chama hicho.
Alisema kikao chenye wajibu wa kumfukuza uanachama ni Mkutano Mkuu
pekee ambao unawashirikisha wajumbe wote kutoka kila upande wa Bara
na Zanzibar.
“Kifungu cha 79(2)(a) cha Katiba ya chama hicho kinasema kuwa,
Mkutano Mkuu unaweza kuchukua hatua za nidhamu zozote zile zikiwamo
kumuachisha au kumfukuza uongozi au uanachama au yote mawili, mwenyekiti
wa chama hicho.
“Mimi navuliwa uanachama na Mkutano Mkuu, siyo baraza la uongozi
ambalo na lenyewe halijakidhi matakwa ya katiba ya chama… kilichofanyika
Zanzibar ni sawa na kikao cha harusi,” alisema.
Alisema licha ya kufanyika kikao hicho, pia idadi ya wajumbe
waliohudhuria kutoka upande wa bara ni tisa kati ya 22 na wajumbe watatu
ni wakurugenzi huku wanachama wa kawaida walikuwa sita.
Profesa Lipumba alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF, kikao cha Baraza
Kuu huitishwa na mwenyekiti na hutakiwa kukutana kila baada ya miezi
minne isipokuwa kama kuna dharura. Linakutana chini ya mwenyekiti na
si vinginevyo, alisisitiza.
“Kifungu cha 83(1) ambacho kinalipa mamlaka Baraza Kuu kuwasimamisha
uongozi na siyo kuwavua uanachama viongozi wakuu wa chama ambao ni
Mwenyekiti, Makamu na Katibu Mkuu. Hivyo baraza halina uwezo wa kunivua
uanachama,” alisema.
Alisema katiba hiyo, kifungu cha 83(5) kinasema, baraza hilo linaweza
kuchukua hatua za nidhamu ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kwa maandishi
na karipio kali.
Alisema hakuna hatua zilizofuatwa katika Baraza Kuu hasa kwa kumvua
uanachama ila kuna fitina zinazochochewa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(Chadema).
“Mimi sifukuziki ndani ya chama hiki, wala sisusi, nimelipia kadi
yangu hadi mwaka 2020, nitaendelea kukipigania chama hiki hadi mwisho,
sihami, siondoki…wala siendi mahakamani, nipo ngangari, wakija Buguruni
watanikuta kama mwenyekiti wa chama,” alisema.
Juzi, Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilitangaza kumvua uanachama
Profesa Lipumba kwa kile kilichoelezwa kukaidi wito wa kwenda kujieleza
kwa kuvamia ofisi za CUF za Buguruni na kufanya uharibifu wa mali za
chama.
Septemba 23, Msajili wa vyama Jaji, Francis Mutungi, alimrejesha
katika nafasi yake ya uenyekiti na siku iliyofuta kiongozi huyo
alikwenda ofisini kwake Buguruni na kuzuka tafrani hiyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment