Zungu alimuomba radhi Mbowe jana baada
ya wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mwita
Waitara wa Ukonga na Paschal Haonga wa Mbozi, kusimama na kuomba
mwongozo kwa nyakati tofauti.
Aliyeanzakumlalamikia Zungu ni Waitara
ambaye katika maelezo yake, alisema anashangazwa na utaratibu uliotumiwa
na mwenyekiti huyo wa Bunge kwa kushindwa kutambua mchango uliotolewa
na Mbowe baada ya kutokea tetemeko hilo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, hivi punde
umewataja na kuwashukuru viongozi mbalimbali wa Serikali walioshiriki
kwa karibu kuwapa pole wananchi waliopatwa na matatizo kule Kagera
kutokana na tetemeko la ardhi.
“Umewataja waziri mkuu na mawaziri
wengine walioshiriki tukio hilo, lakini hukumtaja kabisa kiongozi wa
upinzani bungeni wakati naye alikwenda Bukoba kutoa pole.
“Hata sisi wabunge wa Chadema kabla ya
Bunge kukubali kukatwa posho ya siku moja ili kuwachangia waathirika,
tulikuwa tumekwisha kuchangishana fedha na kumkabidhi mwenyekiti wetu
azipeleke, lakini hukututaja.
“Kwa hiyo, mheshimiwa mwenyekiti, naomba
mwongozo wako juu ya tukio hili kwa vile imekuwa ni kawaida kwa
viongozi wa Serikali kutowatambua viongozi wa upinzani katika matukio
mbalimbali,” alisema Waitara.
Hoja hiyo ya Waitara, iliungwa mkono na Haonga ambaye naye alionyesha kumshangaa Zungu kwa kutomtaja Mbowe.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mwongozo wangu
hautofautiani na mwongozo wa Mheshimiwa Waitara kwa sababu umewataja
viongozi wengine na kushindwa kumtaja Mbowe wakati ni kiongozi mkubwa
hapa bungeni.
“Kwa hiyo na mimi naomba mwongozo wako katika jambo hilo,” alisema Haonga baada ya kutumia kanuni ya 68 (7).
Akijibu miongozo hiyo, Zungu alikiri
kosa kwa kutomtaja Mbowe kwa kuwa naye alishiriki kwa karibu kuwapa pole
waathirika wa tetemeko hilo.
“Ni kweli sikumtaja Mbowe, namuomba
radhi kwa kosa hilo. Hili suala lisitugawe, tuwe wamoja tuweze
kuwasaidia ndugu zetu waliopata matatizo,” alisema Zungu.
Awali, mwenyekiti huyo wa Bunge
aliishukuru Serikali kwa jinsi ilivyoshiriki kwa karibu kukabiliana na
madhara ya tukio hilo na kuitaka iendelee
na utaratibu huo kila majanga yanapotokea.
Septemba 10 mwaka huu, tetemeko la ardhi
lenye ukubwa wa 5.7 katika vipimo vya richter lilitokea mkoani Kagera
na kusababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi wengine zaidi ya 200.
Pia, tetemeko hilo lilisababisha majengo na nyumba kadhaa kuharibiwa zikiwamo taasisi za umma na za binafsi.
Wakati huo huo serikali imewasilisha miswada miwili bungeni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uvuvi na kilimo nchini.
Miswada hiyo ya Sheria ya Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo Tanzania ya Mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Taasisi
ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania
wa Mwaka 2016, iliwasilishwa jana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba.
Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania ya Mwaka 2016, Dk. Tizeba alisema
sheria inayopendekezwa inakusudia kuweka mfumo wa utafiti unaolenga
kuimarisha shughuli za utafiti wa kilimo kulingana na mahitaji.
0 comments:
Post a Comment