BABA
mmoja mkazi wa Kijiji cha Maji ya Moto, Wilaya ya Arumeru mkoani hapa,
Wilfred Kivuyo amemuua mtoto wake baada ya kumchoma kisu tumboni, kwa
kosa la kufungulia redio kwa sauti ya juu.
Kabla ya tukio hilo
inadaiwa yalitokea mabishano ya kugombea kupunguza sauti ya redio kati
ya baba na mtoto, ambapo baba aliamua kumchoma kisu tumboni mtoto wake
na utumbo kutoka nje.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles
Mkumbo alisema, tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu saa tatu usiku
katika Kijiji cha Maji Moto na kumtaja marehemu kuwa ni Abraham Wilfred
(22), ambaye kabla ya mauti alikuwa nyumbani akiendelea na shughuli
zake huku akiwa amefungulia redio.
Alisema siku ya tukio mtuhumiwa
huyo alifika nyumbani akiwa amelewa na kumkuta mtoto wake amefungulia
redio kwa sauti ya juu, ambapo alimtaka kupunguza sauti hiyo lakini
mtoto huyo aligoma.
“Baada ya hapo mabishano na kutoelewana
kulijitokeza baina yao wakaanza kupigana, baba alipozidiwa nguvu na
mtoto wake alichomoa kisu cha kukunja kwenye mfuko wa suruali kisha
akamchoma tumboni na kumsababisha utumbo kutoka nje.
“Mara baada ya
tukio hilo mtoto huyo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya
Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu, lakini hata hivyo alifariki
wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake,” alisema Kamanda
Mkumbo.
Kamanda Mkumbo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka
mtuhumiwa huyo ambaye baada ya tukio alikimbia ili hatua zaidi za
kisheria zisichukuliwe dhidi yake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment