WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa muda wa miezi
miwili kwa wafanyabiashara wanaotumia majina ya biashara pasipo
kusajiliwa, wafanye hivyo haraka.
Baada ya muda huo kupita, patakuwa na msako nchi nzima ili kuwabaini
wale wote wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajili na kuwafikisha
katika vyombo vya sheria au kuwatoza faini.
Akizungumza na waandishi wa jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi alisema katika kazi hiyo ya kutoa elimu na
kurasimisha majina ya biashara na kampuni inayoendelea katika mikoa
mbalimbali, imebainika kuwa wafanyabiashara wengi wanatumia majina ya
biashara pasipo kuyasajili.
“Sheria ya Majina ya Biashara inamtaka mfanyabiashara kusajili jina
la biashara yake ndani ya siku 28 toka aanze kulitumia,” alisema Kanyusi
na kuongezea kuwa kinyume cha hapo atakuwa amevunja sheria ya majina ya
biashara.
Alisema sasa usajili wa majina ya biashara umerahisishwa, kwani
unafanywa kwa njia ya mtandao kwa kutembelea tovuti ya wakala huo ambayo
ni www.brela.go.tz ili kupata maelezo yote ya namna ya kusajili jina la
biashara.
Aliwataka wafanyabiashara wasiishie kusajili tu jina la biashara,
bali pia waende katika Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa ajili ya kupata Namba
ya Mlipa Kodi (TIN), pia waendelee katika halmashauri zao kupata leseni
ya biashara.
“Kwa kurasimisha biashara serikali itapata mapato kwani wigo wa
walipa kodi utaongezeka na pia itakuwa faida kwa wafanyabiashara katika
kujengewa mazingira bora ya kufanya biashara,” alisisitiza Kanyusi.
Alisema Brela imejipanga kuzunguka mikoa yote nchini ili kutoa elimu
juu ya urasimishaji wa majina ya biashara na kampuni kwani imeonekana
wananchi hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa urasimishaji.
Hadi sasa Brela imefanya ziara katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na
Simiyu na wiki hii watakuwa mkoani Shinyanga kwa wiki moja katika
kuhamasisha wafanyabiashara kurasimisha biashara zao.
Alisisitiza kuwa ni lazima kuhakikisha kuwa biashara zinarasimishwa
ili serikali iwatambue walipa kodi wake ambao watachangia Pato la Taifa
na kuiwezesha Tanzania kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment