RAIS John Magufuli amewataka watanzania kuwa mstari wa mbele, kutunza
amani yao kwa kuhakikisha wanawafichua wale wote wenye lengo ya
kuivuruga amani hiyo.
Pia, ametoa changamoto kwa vyombo vya habari nchini kuweka zaidi
uzalendo mbele na kuandika habari za maendeleo ya nchi zinazoonekana,
badala ya kung’ang’ania kuandika habari zenye mlengo wa kuiponda
serikali pekee.
Rais alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati akizindua kiwanda cha
kusindika matunda kinachomilikiwa na kampuni ya Food Products ya
Bakhresa kilichopo katika Kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga mkoani
Pwani.
Alisema endapo Watanzania wataichezea amani iliyopo iliyodumu kwa
muda mrefu, jitihada za serikali za kuijenga nchi kiuchumi na
kimaendeleo ikiwemo uchumi wa viwanda, kamwe hazitazaa matunda.
“Navipongeza vyombo vya dola kwa jitihada zake za kuhakikisha nchi
inadumu kwenye amani, nawahakikishia serikali haitovumilia mtu yeyote
mwenye nia ya kuivuruga amani hii,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zinazozungumziwa kuwa
uchumi wake kuwa unakua kwa kasi barani Afrika; huku uchumi wake katika
robo ya pili ya mwaka pekee ukifikia asilimia 7.9.
“Lengo la serikali yangu ni kuhakikisha uchumi unakua na kufikia
asilimia 7.2 lakini hadi robo ya pili ya mwaka tumefikia asilimia 7.9
tumevuka lengo. Hii ina maana kuwa mpaka tufikie robo tatu hata kama
hapo katikati kutatokea mgogoro kidogo wa kiuchumi tutaweza kufikia
lengo la asilimia 7.2,” alisema.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema pamoja na mafanikio hayo
yanayosifiwa hadi na vyombo vya nje, hali ni tofauti hapa nchini kwani
vyombo vingi vya habari vimekuwa vikiona habari za maendeleo ya nchi si
habari ya kuripoti.
“Tatizo kuna Watanzania hawapendi kusifia kitu cha kwao, leo hii Dar
es Salaam kuna wageni wapatao 30,000 wa madhehebu ya Bohora, sherehe yao
duniani inafanyikia Tanzania, lakini huwezi kusikia vyombo vyetu vya
habari zinatangaza suala hilo,” alisema Rais Magufuli.
Alisema sherehe hiyo kufanyikia nchini, ina faida kubwa kiuchumi kwa
Tanzania, si tu kitaifa, bali hata kwa mtu mmoja mmoja ikiwemo
kuliingizia taifa fedha za kigeni, lakini kwa kuwa suala hilo linahusu
maendeleo si habari ya kuandikwa.
Pamoja na hayo, Magufuli alipongeza mwekezaji mzalendo, Said Salim
Bakhresa kwa kuamua kuanzisha usafiri wa majini kutoka Dar es Salaam
kwenda Mkuranga na kumhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inampa
baraka zote.
Aidha, Rais alitangaza rasmi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina
mpango wa kupiga marufuku matumizi ya plastiki kwa kuwa zimekuwa
zikiharibu mazingira.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment