STAA wa muziki wa RnB kutoka nchini Marekani, Chris Brown ameweka
historia baada ya kufanya shoo yenye ujazo wa juu katika onesho
lililopewa jina la Mombasa Rocks Music Festival iliyofanyika juzi
Jumamosi jijini hapa.
Onesho hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Mombasa Rocks Music
lilifanyika katika Viwanja vya Nyali Mombasa Golf Club na kuhudhuriwa na
mamia ya mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Mombasa.
Chris Brown maarufu Breezy alijua namna ya kutumia vyema jukwaa hilo
na kupagawisha mashabiki ambao walikuwa wakimshangilia muda wote
aliokuwa akifanya vitu vyake jukwaani.
Msanii huyo alipanda jukwaani mishale ya saa 6:30 usiku na kufanya
kazi ya kuwaburudisha mashabiki mpaka saa 9 kasoro za usiku ambapo
shangwe ilitawala viwanjani hapo.
Mbali na msanii huyo kuonyesha ufundi mkubwa katika kuimba na
kucheza, madansa wake wawili waliokuwa naye beneti muda wote,
walinogesha onesho hilo kwa staili yao ya kucheza huku kivutio kikubwa
kikiwa ni kupiga muziki live.
Kwa zaidi ya dakika 90, Brown alipiga shoo mfululizo ingawa alitumia
dakika tatu katikati ya shoo kwa ajili ya kubadilisha mavazi.
Kabla ya Brown kupanda, alisafishiwa njia na wasanii wengine wa
Afrika huku wa mwisho kabla ya yeye kupanda akiwa ni mkali wa Bongo
Fleva, Ali Kiba.
Wa kwanza kupanda jukwaani alikuwa ni mkongwe wa Dancehall nchini
Kenya, Naazizi Hirji ambaye alipagawisha mashabiki kwa nyimbo zake za
zamani kama Let’s Get Down na Kenyan Girl Kenyan Boy zilizoamsha shangwe
kwa mashabiki.
Baada ya Nazizi kushuka jukwaani, msanii Nadio kutoka Uganda alipanda
kufanya yake kabla ya kupokelewa na mtoto mzuri kutoka Bongo Fleva,
Vanessa Mdee ‘V – Money’ ambaye alipiga shoo matata.
Vanessa hakufanya makosa, aliamsha mashabiki pale alipoimba nyimbo zake maarufu Nobody But Me, Niroge na Siri.
Wa mwisho kupanda jukwaani kabla ya Ali Kiba kumpisha Breezy alikuwa
ni mkali kutoka Nigeria, Wiz Kid ambaye alitumia muda mwingi kucheza juu
ya spika zilipokuwa pande mbili za jukwaa kuu.
Hii ni mara ya tano sasa, Wiz Kid anapata shavu la kupafomu jukwaa
moja na mkali huyo kutoka Marekani na hivyo kuweka rekodi ya peke yake
kuwa mwenye bahati ya kupiga naye kazi jukwaani mara nyingi.
Mapema Juni, mwaka huu Breezy alimpa Wiz Kid mchongo wa kushiriki
kwenye Tamasha la One Hell of a Nite lililofanyika mjini Amsterdam,
Uholanzi.
Kabla ya hapo walishakutana kwa nyakati tofauti kwenye shoo nyingine tatu zilizofanyika nchini Nigeria na nyingine Ghana.
ALI KIBA
Mbali na Chris Brown, staa aliyekuwa na mvuto mkubwa zaidi katika
onesho hilo ni Ali Kiba ambaye alipanda jukwaani na kuimba kwa ustadi wa
hali ya juu.
Kiba aliimba nyimbo zake Aje na Mwana ambazo aliimba na mashabiki huku wakimshangilia.
Mishale ya saa 6 usiku, baada ya kuimba nyimbo hizo mbili pekee, Kiba
aliaga mashabiki ambao wengi waliamini alikuwa akitania, maana wasanii
wote waliotangulia waliimba zaidi ya nyimbo tatu.
“Thank you and goodbye (nawashukuru sana, kwaherini),” alisema Kiba kisha zikafuata kelele za mashabiki.
Tofauti na matarajio ya wengi, Kiba alikuwa hatanii, alirudi hadi
mwisho wa jukwaa, kisha akafuata njia ya kushuka akiongozana na madensa
wake.
“Kibaaa arudiiii, Kiba aje… Kiba, Kiba….,” kelele hizo kutoka kwa mashabiki zilisika.
CHRIS BROWN HESHIMA
Breezy hakufanya makosa, katika muda wote aliokuwa jukwaani alitumia vizuri kila sekunde yake kwa kuangusha shoo ya nguvu.
Akiwa na madensa wake, Breezy aliimba nyimbo zake maarufu kama With
You, Kiss Kiss, Don’t Wake Me Up, Next To You, Internation Love na Love
More zilizowainua mashabiki pande zote za viwanja hivyo.
Mashabiki wa kike walichanganyikiwa na kupiga kelele pale msanii huyo
alipovua tisheti yake na kubaki kifua wazi, ambacho sehemu kubwa
alikuwa amechora tattoo.
TAMASHA LA BEI MBAYA
Tamasha la juzi mjini hapa, licha ya kuwa na kiingilio kikubwa sana,
wahudhuriaji walikuwa wengi kiasi katika eneo la kawaida, lakini upande
wa VIP na VVIP eneo lote lilifurika watu.
Kiingilio cha chini katika onesho hilo kilikuwa ni Shilingi 10,000 za
Kenya (karibu 220,000 za Tanzania), VIP Shilingi 20,000 (karibu
440,000) huku wale wa VVIP wakilipa Shilingi 50,000 (karibu 1,100,000).
Siku mbili kabla ya onesho hilo, watayarishaji wa shoo hiyo walitoa
ofa kwa wateja kununua tiketi kwa elekroniki kwa punguzo la Shilingi
5,000 (karibu 110,000 za Tanzania) lakini baada ya muda mfupi sana
ziliisha.
Wakazi wa hapa Mombasa wanaeleza kuwa, ilikuwa miongoni mwa maonesho
machache yenye viingilio vikubwa kupata kufanyika mjini hapa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment