WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ameahidi kuzungumza na mwenzake wa Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ili kuhakikisha halmashauri
zote nchini zinapanga bajeti ya kununua viuadudu katika kupambana na
malaria.
Akizungumza baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Mesa
kutembelea kiwanda cha kutengeneza viuadudu, Kibaha mkoani Pwani jana,
Ummy alisema hatua ya kuzungumza na Waziri wa Tamisemi ni katika
kuhakikisha halmashauri zinunue dawa hiyo kwa lengo la kupambana na
ugonjwa wa malaria nchini.
“Tunataka halmashauri zote zitenge bajeti ya kununua viuadudu ili
kila wiki ipulizwe kwenye maeneo yao, kwani na kuhakikisha tunatokomeza
malaria na kuifanya nchi isiyo na malaria kama ilivyo Cuba,” alisema.
Aliongeza kuwa malaria ni ugonjwa unaosumbua watu wengi na unaifanya
serikali kutumia rasilimali fedha nyingi. Alisema takwimu za sasa
zinaonesha kuwa takribani Watanzania 14 kati ya 100, wanaugua malaria
wakati uwezo ni kutengeneza lita milioni sita kwa mwaka.
Akizungumza kabla ya kukagua kiwanda hicho na kuzungumza na
wafanyakazi kutoka Cuba, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mesa
aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujenga kiwanda hicho ambacho
kitasaidia katika kupambana na malaria nchini na nchi zingine za Bara la
Afrika.
“Kiwanda hiki kina umuhimu mkubwa kwa Tanzania si katika nyanja ya
afya pekee, bali hata katika kuongeza ajira kwani zaidi ya wafanyakazi
zaidi ya 100 wataajiriwa,” alisema Makamu wa Rais aliyekuwa katika ziara
ya siku tatu nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk Samwel
Nyantahe alisema kiwanda hicho ni cha kipekee Afrika na kina uwezo wa
kuzalisha viuadudu kwa ajili ya soko la ndani, Afrika Mashariki na nchi
zingine za Afrika. "Faraja iliyopo ni kuwa wenzetu wa Cuba wako tayari
kutusaidia katika masoko mengine kwa ajili ya kuuza bidhaa zetu,"
alisema.
Kiwanda hicho kilichofunguliwa mwaka jana, kinatarajia kuanza
uzalishaji mwishoni mwa wiki hii, ikiwa ni siku kadhaa tangu kupata
mkopo wa Sh bilioni nne zikizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF).
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment