KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,
amemdhibiti mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kuandika barua kwa benki zote ili
kudhibiti ruzuku ya chama isipite kwenye mikono ya kiongozi huyo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
kumtambulisha Prof. Lipumba Benki ya NMB Tawi la Ilala akitaka apewe
ushirikiano wa kufungua akaunti mpya ya chama.
Taarifa kutoka ndani ya CUF zililiambia MTANZANIA kuwa juzi Maalim
Seif, aliandika barua kwa benki zote kuzui hatua hiyo kwa kuweka zuio la
mtu yeyote kufungua akaunti ya chama.
“Unajua hii vita si ya kitoto ni mapambano yaliyopo ndani ya CUF
lakini yana nguvu kubwa kutoka katika kila pembe ya watu wanaochukia
upinzani. Na pia wapo hata viongozi wakubwa wa dola ambao kila siku
wamekuwa wakifanya kazi ya kuivuruga CUF.
“Walitegemea lakini tangu jana (juzi) Katibu Mkuu ameziandikia barua
benki zote nchini kuzuia mpango wa Msajili kutaka kuchepusha ruzuku ya
chama na kwenda katika mikono ya Lipumba na sasa nakala yake imepelekwa
kwa Msajili wa Vyama,” alisema mtoa habari wetu.
Hatua ya Profesa Lipumba kufungua akaunti inatokana na barua
aliyopewa na Msajili wa Vyama vya Siasa ya Oktoba 6, mwaka huu
iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kwenda
kwa Meneja wa Benki NMB Tawi la Ilala.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba HA.322/362/14/104 ambayo
inamtambulisha Profesa Lipumba kutakiwa kufungua akaunti mpya ya The
Civic United Front (CUF).
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Kaimu Naibu Mkurugenzi wa
Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Mbarara Maharagande ambaye
alithibitisha kuandikwa kwa barua hiyo kwa benki zote nchini.
Siri ya Profesa Lipumba kutaka kufungua akaunti mpya yenye jina la
Chama cha Wananchi CUF inadaiwa kutolewa na watumishi wa benki wa tawi
hilo.
Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa Vyama Vya Siasa, huku chama chake kikiwa tayari kimemfukuza
uanachama.
Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kupitia Sisty Nyahoza ilinukuliwa
na vyombo mbalimbali vya habari ikikiri kumtambulisha Profesa Lipumba
kwa Benki ya NMB ili aweze kufungua akaunti hiyo, hata hivyo ikikana
kujua matumizi ya akaunti hiyo.
Taarifa za kufunguliwa kwa akaunti mpya yenye jina la CUF kwa malengo
yanayodaiwa ni kuchukua ruzuku za chama hicho zilianza kusambaa katika
mitandao ya kijamii wiki iliyopita.
Hatua ya Profesa Lipumba ambaye kwa sasa yupo katika ziara kwenye
mikoa ya kusini kutaka kufungua akaunti hiyo ilipingwa vikali na wana
CUF akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVCUF), Hamidu
Bobali ambaye alitangaza kwa kuwataka wanachama wao kutompa ushirikiano
kiongozi huyo katika ziara zake.
Maalim na Msajili tena
Katika hatua nyingine Maalim Seif amemwandikia tena barua Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, akimtaarifa kuhusu maamuzi
ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi liloketi Septemba 27, mwaka huu.
Barua hiyo ya Oktoba 4, mwaka huu yenye kumbukumbu namba
CUF/HQ/KM/2016/21, ambapo Maalim Seif alisema wamebaini kwamba pamoja na
kuandikia mara kadhaa kwamba Ofsi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina
mamlaka, uwezo wala wajibu wa kuingilia maamuzi ya vikao halali vya
chama.
“Pamoja na hali hiyo bado umekuwa ukituandikia na kututaka tujibu
malalamiko ya watu waliowasilisha malalamiko kwako kuhusiana na maamuzi
ya vikao halali vya chama.
“Uzoefu tulioupata kupitia barua yako Kumb. Nam. HA.322/362/14/85 ya
tarehe 23 Septemba, 2016 iliyokuwa na kichwa cha maneno, “MSIMAMO NA
USHAURI WA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU UONGOZI WA KITAIFA WA CHAMA
CHA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF)”. alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment