WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa mabati 100 yenye thamani ya
zaidi ya sh. milioni mbili kutoka kwa Mbunge wa Viti maalum mkoa wa
Lindi Mhe. Hamida Abdallah.
Msaada huo umetolewa leo (Jumatano,
Oktoba 19, 2016) katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara
ya Waziri Mkuu hospitalini hapo.
Mbunge huyo amesema amekabidhi
msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwezi Aprili mwaka
huu wakati Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Hospitali hiyo.
“Ulipofanya
ziara ya mwezi wanne hospitalini hapa nilikuahidi kukupa mabati 100
kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanawake. Nilitoa ahadi hii baada ya
kuona jitihada kubwa unazozifanya katika kuimarisha hospitali hii,”
amesema.
Akipokea msaada huo Waziri Mkuu amemshukuru Mhe. Hamida kwa
kutekeleza ahadi yake na kumuomba aendelee kuisaidia hospitali hiyo
pindi anapopata nafasi.” Nashukuru sana kwa msaada wako tunajua kutoa ni
moyo na si utajiri,”.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema mkakati
wake kwa sasa ni kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kila kijiji
kinakuwa na zahanati ili kuwawezesha wananchi kupata matibabu karibu na
makazi yao.
“Nataka sekta ya afya inapata mafanikio makubwa.
Nitashirikiana na wananchi kuhakikisha kunakuwa na zahanati katika kila
kijiji na vituo vya afya kwenye kata zote,” amesema.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea
Chezue alimshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kuboresha huduma
hospitalini hapo.
Amesema hivi karibuni walipokea sh. milioni 100
kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi kwa ajili ya ukarabati wa wodi
mbili ambazo tayari ukarabati huo umekamilika na zitaanza kutumika
kuanzia Novemba 15 mwaka huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 19, 2016
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment