WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itachukua hatua
kuhakikisha kuwa waliohusika na mauaji ya watafiti wa Kituo cha Utafiti
wa Kilimo cha Selian Arusha (SARI) wanakamatwa na kufikishwa kwenye
mikono ya sheria.
Amebainisha kwamba watafiti hao waliouawa jioni ya Jumamosi iliyopita
katika Kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino katika Mkoa wa Dodoma,
walifika Dodoma kutokana na agizo la serikali la kufanya uchunguzi wa
matetemeko ya ardhi kama yatakuwa endelevu nchini. Mbali ya hayo,
amewatoa hofu wale wanaokuja Dodoma kwa ajili ya kikazi au kuwekeza
kwani Dodoma ni shwari.
Waliouawa kwa kucharangwa kwa silaha kama mapanga na shoka na kisha
kuchomwa moto ni Nicas Magazine aliyekuwa de reva, mtafiti Theresia
Nguma (43) na kijana aliyekuwa akianza kazi ya utafiti, Jaffari Mafuru,
wote kutoka SARI jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa jana,
Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imesikitishwa sana na tukio hilo
la watumishi wa serikali kuuawa wakati wakiendelea na majukumu yao ya
kazi.
Asikitishwa na vifo
“Ni jambo la kusikitisha sana tunawaombea roho zao zipumzike kwa
amani, kama serikali tutachukua hatua kwa kuhakikisha waliohusika
wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema na kuongeza
kuwa watafiti hao walitumwa na serikali kutokana na tetemeko la ardhi
lililotokea mkoani Kagera.
“Walikuja Dodoma kutoka Arusha kufuatia agizo la serikali la kufanya
uchunguzi wa matetemeko ili ijulikane kama tetemeko ni endelevu,”
alibainisha na kuongeza kuwa kufanyika kwa utafiti huo, serikali iliomba
Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
kufanyika utafiti huo, hivyo serikali kupita kwa taasisi zake iliamua
kufanya uchunguzi kuhusu matetemeko hayo kama yataendelea ama la.
“Waliweka mpango kazi wapite mkoa wa kati kwenye Bonde la Ufa,
walifanya kazi zao kwa siku tano siku ya sita ndipo wakakumbana na
umauti. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi,” alieleza Waziri Mkuu
na kufafanua kuwa jukumu la serikali ni kuhakikisha wanaokuja Dodoma
wajue Dodoma ni salama, historia ya Dodoma haioneshi kama ina matukio ya
ajabu kama haya.
“Jukumu la Serikali ni kuhakikisha Dodoma ni salama, wanaokuja
wataikuta Dodoma ni salama,” alisema Majaliwa ambaye alihamia mjini hapa
mwishoni mwa wiki iliyopita kuanza utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya
Tano kuhamia Dodoma kuanza sasa hadi ifikapo mwaka 2020.
Makamu wa Rais alaani
Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amelaani mauaji ya watafiti
wawili wa Seliani na dereva waliokuwa kazini katika Kijiji cha Iringa
Mvumi, Chamwino.
Akifungua Kongamano ya 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa
na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwenye
Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
jana, Samia alisema tukio hilo ni baya na amewahakikishia watafiti
wanaoshiriki kongamano hilo kuwa serikali itachukua hatua stahiki kwa
watu waliofanya kitendo hicho cha kinyama ili kukomesha tabia hiyo.
“Haiwezekani hata kidogo watu kufanya mauaji hayo ya kikatili na
waachwe bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisisitiza Makamu wa
Rais.
Akizungumzia masuala ya utafiti, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
amesema serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na watafiti hao hivyo
serikali itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali ili kuhakikisha
watafiti hao wanafanya kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.
Waziri ashiriki maziko Arusha Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, William ole Nasha akitoa salamu za serikali wakati wa maziko
ya Nguma, jana Olasit jijini Arusha, alisema msiba huu ni msiba mzito
kwa serikali kwani imepoteza watafiti wake waliokuwa wakichukua sampuli
za udongo kwenye maeneo mbalimbali na hatimaye wakakutana na mauti.
Alisema serikali haipo tayari kuvumilia tukio hilo na ndio maana
inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo kuwashikilia watu zaidi ya
43 hadi jana.
Ole Nasha alisema serikali haijawahi kupata tukio la unyonyaji damu
na wala hakuna matukio hayo Tanzania na hakuna ukweli wowote juu ya
tukio hilo na kutoa rai kwa wananchi kuacha tabia yakujichukulia sheria
mkononi.
Alisisitiza kuwa kama wananchi au wanakijiji wana hofu ya jambo
fulani ni bora kwenda polisi au uongozi wa kijiji ili kulitatua badala
ya kujichukulia sheria mkononi.
“Acheni kujichukulia sheria mkononi kama mna hofu na watu nendeni
sehemu husika badala ya kuwaua watu wasio na hatia na hizi tuhuma za
kunyonya damu zinatoka wapi wakati katika nchi yetu hakuna mambo kama
haya,” alieleza naibu waziri.
Mtoto wa marehemu kusomeshwa
Aidha, alibainisha kuwa wanaendelea kuzungumza na familia za Magazine
na Mafuru kufahamu nini cha kufanya, lakini kwa familia ya Theresia,
serikali itamsomesha mtoto wake wa kiume Gabriel kwa kumlipia ada katika
Chuo cha Uhasibu Njiro jijini Arusha huku mtoto mwingine wa kike, Lisa
serikali ikiendelea na mazungumzo na familia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti Makao Makuu ya wizara, Dk Hussein
Mansuri alisema Theresia na Magazine anawafahamu kwa kuwa ni watumishi
wa Seliani na wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Alisema Theresia aliomba kupata safari hiyo ili apate ada ya
kuwalipia watoto wake, lakini amekufa akiwa kazini hivyo kituo hicho
kimepoteza watu muhimu waliojitolea kwa ajili ya kusaidia wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqro alisisitiza serikali
haitawavumilia watu wanaojichukulia sheria mkononi na kutoa rai kwa
wananchi wa Arusha kutii sheria, kanuni na taratibu na endapo kuna
taarifa za mashaka miongoni mwa jamii inayowazunguka vipelekwe sehemu
husika ili kudhibiti mauaji au uharibifu wa mali.
Paroko: Tusilipize kisasi, tusamehe
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yoseph Mfanyakazi
Olasiti, Boniface Mbite amewasihi waumini wa madhehebu mbalimbali
kuwasamehe wale wote waliohusika na tukio la kuwaua na kuwachoma moto
watafiti wa Selian.
Akizungumza katika misa ya kumuaga Theresia aliyezaliwa Oktoba 10,
1973, Paroko Mbite alisema msiba huo ni msiba mzito, lakini ni lazima
kumshukuru Mungu kwa kila jambo na tukio hilo lililotokea ni la
kusikitisha, lakini ikumbukwe kuwa wanadamu bila kujali tofauti za dini,
kabila jinsi na vinginevyo, wote ni wanawali wa Mungu.
“Lakini licha ya kuwa wanawali wa Mungu, miongoni mwetu wapo
wapumbavu na wenye busara na kila mmoja amepewa taa yake ambayo ili
iwake ni lazima usali na kukubali kusamehe hata katika jambo linaloudhi
kama hili lililotokea kwa wenzetu,” alisema Paroko Mbite na kuongeza:
“Msilipize kisasi, serikali ipo na inafanya kazi yake tuiache ifanye
kazi yake.
Tujifunze kusamehe waliohusika na tukio hili vyombo vya dola
zitawachukulia sheria na lazima tutambue ya kuwa sisi wote tunapita
hatuna haja ya kuhuzunika, bali tushukuru Mungu kwa hili lililotendeka
hakika bwana atatenda.
” Alisisitiza kuwasamehe wote walifanya mauaji hayo ingawa ni ngumu,
lakini alisema Mungu alitoa neno kuwa ni “lazima tusamehe wale
wanaofanya mambo mabaya kama haya yaliyotokea.”
Marehemu Theresia amezikwa eneo la nyumbani kwake ambako ni karibu na
kanisa hilo huku watu mbalimbali wakihudhuria maziko yake wakiwemo
watafiti kutoka vituo mbalimbali mikoani, wafanyakazi wenzake, ndugu
jamaa na marafiki.
Polisi: Acheni kujichukulia sheria mkononi
Nalo Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kwa wote wenye tabia ya
kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja huku ikibainisha kuwa
kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, kumekuwapo na matukio 705 ya
kujichukulia sheria mkononi.
“Katika siku za hivi karibuni kumeendelea kuwepo kwa vitendo na tabia
ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga,
kuwachoma moto na kuwaua baadhi ya watu wasio na hatia pamoja na
wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu jambo ambalo ni kinyume
cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Mpaka sasa takwimu za makosa ya kujichukulia sheria mkononi
yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi katika kipindi cha Januari hadi
Agosti mwaka 2016 ni matukio 705.Katika matukio hayo yaliyoripotiwa,
Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani
watuhumiwa 393,” ilieleza taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi
Makao Makuu, Advera Bulimba.
“Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali kwa
wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja. Aidha,
kwa kuzipuuza sheria za nchi zilizopo na wakati mwingine kuzikiuka kwa
makusudi na mbaya zaidi baadhi yao kufikia hatua ya kuwaua watu wasio na
hatia kwa hisia. Mwananchi yeyote anapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya
dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mhalifu au mtu
yeyote wanayemtilia mashaka katika maeneo yao,” alisema Bulimba.
“Aidha, Jeshi la Polisi nchini litaendelea kuchukua hatua kali za
kisheria kwa kufuatilia na kuwakamata watu wote wanaojihusisha na tabia
za kujichukulia sheria mkononi. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watu
wote wakiwemo wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuendelea kukemea na
kutoa elimu juu ya madhara ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake
wananchi kuendelea kutii na kufuata sheria za nchi zilizopo,” iliongeza
taarifa ya Bulimba.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment