MWISHONI mwa wiki, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe
ameuhakikishia umma wa Tanzania kupitia vyombo vya habari kwamba wizara
yake inaweka mkakati wa kupunguza msongamano gerezani kwa kurekebisha
sheria zinazowafunga watu waliotenda makosa madogo.
Sisi tunaunga mkono kauli hiyo aliyoitoa Waziri Mwakyembe wakati
akizungumza na Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Chris Kourakis
aliyetembelea nchini na kujadiliana na watendaji wa idara ya mahakama
kushirikiana katika mambo mbalimbali, yakiwamo ya kufanya marejeo ya
sheria mbalimbali, ikiwamo ya adhabu ya kifungo cha chini na kutoa
mafunzo na kuwajengea uwezo watumishi wa mahakama.
Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome anasema
urekebishaji wa sheria hiyo utawasaidia mahakimu kutoa adhabu ya
kifungo cha chini cha adhabu hiyo, jambo ambalo litapunguza vifungo kwa
wafungwa, hivyo kuondoa msongamano gerezeni.
Ukweli ni kwamba, kumekuwapo na utitiri wa mashauri ya kesi ndogo
ambayo yamejaza watuhumiwa wengi gerezani na kesi zao nyingi zinachelewa
kumalizika mapema, kunakochangia kuongeza msongamano gerezani.
Kurekebisha sheria za mashauri ya kesi ndogo kwa ushirikiano na
huduma nyingine, kutapunguza msongamano na gharama za kuwatunza wafungwa
hao gerezani. Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema anasema
nusu ya wafungwa waliopo kwenye magereza yaliyoanzishwa rasmi mwaka 1931
na wakoloni, wametengenezewa kesi na wenye fedha, kutokana na baadhi ya
askari ambao wasio waaminifu wamekuwa wakicheza ‘dili’ na kuwatia
hatiani watu wasiohusika na wengine wapo kutokana na kesi ndogo.
Mrema ameweka mkakati wa kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu,
atakuwa amepunguza wafungwa 10,000 gerezani, jambo ambalo litasaidia
kupunguza idadi ya wafungwa na kuondoa msongamano gerezani. Lakini pia
wakitokea wasamaria wengi kama Mchungaji Getrude Lwakatare, watachangia
kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani.
Mchungaji huyo ametumia Sh milioni 25 kuwalipia wafungwa 50 wa awamu
ya kwanza na awamu ya pili 28, faini walizokuwa wakidaiwa kutokana na
kutenda makosa madogo ya faini ya pungufu ya Sh milioni moja. Mchungaji
amepunguza msongamano wa wafungwa. Njia nyingine za kupunguza ni
kuachiwa kwa masharti, kupewa muda wa matazamio kwa kupewa kifungo cha
nje, kutoa huduma kwa jamii na parole.
Njia zote hizo zikitumika huku Wizara ya Sheria na Katiba ikairejea
na kuirekebisha sheria za mashauri ya kesi ndogo, hakika msongamano wa
wafungwa gerezani utakuwa historia au tutabaki na wafungwa 21,000 ambao
ndio uwezo wa magereza yote nchini.
Hakika, msongamano wa wafungwa utapungua kwa kasi zaidi, kuliko idadi
aliyoisema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni,
Septemba 8, mwaka huu, bungeni Dodoma kwamba wafungwa wamepungua kutoka
38,000 hadi 34, 000 kutokana na kupewa adhabu mbadala ya parole.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment