LICHA ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika utoaji huduma wa
magari yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (DART), Kampuni inayoendesha
mradi huo, UDART imepiga marufuku usafiri wa bure kwa makundi
mbalimbali wakiwemo askari polisi, walemavu, viongozi wa dini na hata
walimu.
Imesema mageti yaliyokuwa wakiyatumia yafungwe na kila mmoja alipe.
Udart imetoa taarifa hiyo katika waraka uliobandikwa katika kila kituo
mwishoni mwa wiki na kufafanua kuwa kumekuwepo na ongezeko la makundi
hayo, wakipita katika mageti hayo bila kulipa na pia kupokea simu kutoka
katika makundi mbalimbali, yakiomba kupatiwa huduma hiyo.
Hilo limo katika waraka uliosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UDART,
David Mgwassa na nakala kwenda kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
NMB, Msajili wa Hazina na kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa
Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Katika taarifa hiyo, Mgassa alitaka waraka huo ufike kwa watumishi
wote wa usafiri huo na hatua zichukuliwe haraka. Alisema watumishi
waliopo katika vituo wanapaswa kuhakikisha mageti yanakuwa yamefungwa
kwa ufunguo na hakuna anayeruhusiwa kupita bila kulipa.
Makundi hayo yalikuwa yakisafiri bila kulipa nauli katika mradi huo
unaofanya kazi katika Barabara ya Morogoro na ile ya Morocco jijini Dar
es Salaam.
Changamoto nyingine
Aidha, kumekuwapo na changamoto kadhaa ambazo zimeonekana kuwa sugu
kwa sasa katika mradi huo ulioanza mapema mwaka huu; ambazo ni magari
kuchelewa kufika vituoni kwa zaidi ya nusu saa, jambo linalosababisha
abiria kupoteza muda mwingi na mengine yafikapo kutosimama vituoni.
Changamoto nyingine ni ya abiria ambao wanatumia kadi wanapoweka
fedha, hutumika kwa safari chache, ikilinganisha na kiasi cha fedha
kilichowekwa.
Kutokana na hali hiyo, watumiaji wake wamekuwa wakilalamikia mradi
huo siku hadi siku kwamba tangu ulipoanza umekuwa tofauti na matarajio
ya abiria kwa kadri siku zinavyokwenda, kwani umekuwa ni wa kupotezea
abiria muda badala ya kuuokoa.
Mbali na hilo, mashine za kukagua tiketi na kadi zinazotumika katika
usafiri huo, nazo zimekuwa na kero mbalimbali, nyingine zikichelewesha
na nyingine zikigoma, jambo linalosababisha kuwepo kwa msururu wakati wa
kuingia kwa abiria na kutoka.
Mtendaji Mkuu wa Mradi huo, Ronald Lwakatare alikiri kuwepo kwa
changamoto hizo na kueleza kuwa wanapopata malalamiko huyatafutia
ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Lwakatare alisema kuchelewa kwa magari vituoni hilo ni kosa na kwamba
madereva wanapoulizwa wanasema kuwa tatizo ni uwepo wa askari wa
usalama barabarani wanaoongoza magari, jambo ambalo huchelewesha
kuyaruhusu magari hayo, jambo ambalo hubadili mfumo mzima wa usafiri
huo.
“Ni kweli kwamba mradi huu umeanza mapema mwaka huu, lakini mpaka
sasa haujatengemaa. Magari yanatakiwa kufika kituoni kila baada ya
dakika tano zaidi ya hapo hilo ni tatizo,” alisema Lwakatare na kuongeza
kuwa mfumo wa barabara pia huchangia mabasi kuchelewa kufika kituoni.
Alifafanua kuwa magari hayatakiwi kufika kituoni zaidi ya matano kwa
wakati mmoja na hali hiyo husababishwa na askari ambao wanaongoza magari
ama kuwepo kwa msafara wa aina yoyote ile. Alisema wamekuwa
wakishirikiana na askari kuhakikisha magari hayo, yanapewa kipaumbele
ili yawe na maana kwa watumiaji kama yanavyoitwa.
Lwakatare alisisitiza magari yaliyopo ni 120 na kwamba sio magari
yote hayo yanafanya safari kwa siku moja, kwa kile alichoeleza kuwa
yanapishana kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo kwa kadri
yanavyoharibika.
Vilevile aliongeza kuwa kuna wakati magari yanakuwa yamesimama
vituoni, bila ya kwenda mahali kwa kuwa madereva wake wanakwenda msalani
au kula.
“Lengo la kufanya magari hayo yawe yanafika kituoni kila baada ya
dakika tano ni kurahisisha usafiri, lakini abiria wanaposubiri magari
zaidi ya nusu saa bila kupata huduma hilo ni kosa, tutalifanyia kazi,”
alieleza Lwakatare, na kufafanua kuwa magari hayo huanza kazi saa 12
asubuhi.
Alieleza kuwa baadhi ya njia ikiwemo Kivukoni na Gerezani Kariakoo,
zimepewa kipaumbele kwa kuwa na magari mengi kuliko njia ya Morocco.
Alisisitiza kuwa safari za asubuhi na jioni ni tofauti na ya mchana
kwamba wanatoa magari mengi kuwapeleka watu kazini na kwa mchana
hupunguza magari kutegemeana na siku kwani hutofautiana siku hadi siku.
Akizungumzia magari yanayoanzia Mbezi, Lwakatare alisema yapo magari
26 kwa ajili ya kuwatoa abiria walio nje ya Dar es Salaam kwenda Kimara
ambapo ndio kituo kikuu na utaratibu wanaoutumia wa kupanga foleni ndipo
abiria waingie kwenye gari, ndio utaratibu mzuri unaofundisha ustaarabu
badala ya kugombania magari hayo.
Aidha, alisema wanategemewa na watumiaji wa usafiri kwa kuwa asilimia
kubwa ya daladala zilizokuwa zinaenda Kariakoo na Posta kupitia
Barabara ya Morogoro zimepungua. “Tutazifanyia kazi changamoto zote
zinazojitokeza kwa lengo la kuboresha usafiri huu. Tunawaomba abiria
wavumilie tunapozifanyia kazi changamoto hizi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, msemaji wa UDART, Deus Bugaywa alisema takriban
asilimia 30 ya mabasi hayo hupunguzwa katika kutoa huduma hususani
nyakati za mchana kutokana na muda huo kuonekana kutokuwa na abiria
walio wengi ikilinganishwa na asubuhi ama jioni wakati wengi wakielekea
majumbani.
Bugaywa alisema magari hayo yamegawanywa katika hatua mbalimbali
wakati wa kutoa huduma ambao huanza kutoa huduma kuanzia alfajiri saa 11
hadi saa nne ikiwa ni muda ambao abiria ni wengi vituoni na saa nane
mchana hadi saa tatu usiku.
“Hata hivyo, muda mwingine magari hayo huendelea kutoa huduma hadi
saa sita usiku na mpishano wa basi kwa basi ni dakika tano, na katika
siku za Jumamosi na Jumapili magari hupunguzwa ili kutoa muda wa
matengenezo,” alisema na kuongeza kuwa matengenezo mengine makubwa
hufanyika kuanzia saa tano usiku hadi asubuhi.
Alikiri ni kweli kuwa changamoto katika huduma hiyo zipo
zikitofautiana, lakini zikiendelea kufanyiwa kazi siku hadi siku, lengo
likiwa ni kuifanya huduma hiyo kuwa bora yenye kufanikisha kiu ya
watumiaji.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment