UFAULU kwa watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2016
umepanda kwa asilimia 2.52 kutoka asilimia 67.84 mwaka jana hadi
asilimia 70.36, huku wavulana waking’ara katika matokeo hayo ambao wengi
wametoka shule za Kanda ya Ziwa.
Aidha, watahiniwa 238 kutoka shule sita wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika wamefanya udanganyifu katika mtihani huo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa 27 Octoba 2016 na Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Charles Msonde ambaye alisema kati ya
wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mtihani huo, msichana ni
mmoja tu, Justina Gerald wa Shule ya Msingi ya Tusiime ya jijini Dar es
Salaam.
Kati ya wanafunzi hao 10, watahiniwa saba wanatoka Shule ya Msingi
Kwema iliyopo mkoani Shinyanga, wawili Tusiime na mmoja kutoka Kaizirege
ya Bukoba mkoani Kagera. Dk Msonde alisema jumla ya watahiniwa 555,291
kati ya 789,479 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata jumla ya
alama 100 na zaidi kati ya alama 250.
“Idadi hii ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 70.36, kati
ya hao wasichana ni 283,751 na wavulana 271,540. Mwaka 2015 ufaulu
ulikuwa ni asilimia 67.84 kuwapo ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.52,”
alisema Dk Msonde.
Watahiniwa 16,929 wamepata daraja A, watahiniwa 141,616 wamepata
Daraja B, watahiniwa 396,746 wamepata daraja C, watahiniwa 212,072
wakipata daraja D na 21,872 wakipata daraja E . Dk Msonde alisema ufaulu
katika masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii umepanda kwa asilimia kati
ya 4.06 na 14.76 ikilinganishwa na mwaka 2015 huku masomo ya Kiswahili,
Hisabati na Kiingereza ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 0.39 na
12.51 ukilinganisha na mwaka jana.
“Watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili ambalo ufaulu
wake ni asilimia 76.81 na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini ni
Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 36.05,” alifafanua Dk Msonde. Matokeo ya Shule ya Kavazungu Wilaya ya Mwanga Kilimanjaro haya Hapa.->http://necta.go.tz/matokeo/2016/psle/psle.htm
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment