MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya
udalali ya Yono Action Mart jana iliibuka tena kwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), na kuzua tafrani kubwa kwa kutaka kufunga ofisi hizo
kutokana na kudaiwa deni la Sh bilioni 1.6.
Maofisa hao wa TRA wakiongozana na lundo la madalali wa Yono
walitinga ofisi hizo za TFF zilizopo Karume, Ilala saa nane mchana
kuanza kufunga mageti na baadhi ya magari yaliyokuwa yameegeshwa kwenye
ofisi za shirikisho hilo huku wahusika wa magari hayo wakitakiwa kutoka
kwa kitambulisho ili kujua magari yanayomilikiwa na TFF.
HabariLeo ilikuwepo kwenye ofisi hizo na kushuhudia kila kilichoendelea.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliwaomba maofisa
hao wa TRA kuzungumza na baada ya mazungumzo ya muda mrefu kidogo TRA na
Yono wakaondoka kwa makubaliano kuwa TFF watamalizana nao leo hadi
kufikia saa nne asubuhi.
Meneja Operesheni wa Yono, Kasimir Mwandema alisema kuwa wanachofanya
wao ni kutekeleza agizo la TRA kwa kukamata mali za TFF ili kufidia
deni la Sh bilioni 1.6.
“Walitakiwa wawe wameshamaliza kulipa deni kwa mujibu wa makubaliano
ya awali waliyoomba, lakini mpaka sasa hakuna kilicholipwa," alisema
Mwandema huku madalali hao wa Yono wakizingira ofisi hiyo wengine wakiwa
ndani na wengine wakiwa nje na kuzuia magari ya watu ambao walifika kwa
ajili ya huduma mbalimbali.
Hata hivyo, baada ya tafrani iliyodumu takribani nusu saa na kuzua
taharuki kwa wafanyakazi wa shirikisho hilo, hatimaye TFF waliahidi
kumalizana na TRA leo.
“TFF wameomba wakae na TRA wamalizane, tumewapa leo (jana) mpaka
kesho (leo) saa tatu asubuhi, kufanya hivyo, kuanzia saa nne tupo hapa
kama hawatamalizana hatutakuwa na jinsi zaidi ya kutekeleza agizo
tulilopewa,” alisema.
Alisema TRA imekuwa ikiwadai Sh bilioni 1.118 ambayo ni kodi
mchanganyiko kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, kodi hizo VAT, Kodi ya
Mapato, SBL na kwamba hapo nyuma walikamata akaunti zao kwa sababu deni
lilikuwa ni Sh bilioni 1.6 na wakapunguza sehemu ya deni lakini
halijaisha ndio sababu wanataka kukamata tena mali za TFF.
Hii ni mara ya tatu kwa mwaka huu TRA kuvamia ofisi za TFF na
kukamata mali zake, Machi ilizuia fedha za TFF kwenye akaunti zake na
baadaye ikakamata magari matano ya shirikisho hilo ikiwemo basi la timu
ya taifa, Taifa Stars.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa hakuwa tayari kuzungumzia
suala hilo, na baada ya maofisa hao wa TRA na Yono kuondoka, aliitisha
kikao cha dharura kwa baadhi ya watendaji ikiwemo Idara ya Uhasibu
kujadili suala hilo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment