KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Projestus Rwegasira
amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge ya kuhakikisha
mfumo wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole unafungwa katika wilaya
za kipolisi 108 nchi nzima kwa muda wa miezi mitatu.
Zabuni ya kufunga na kusambaza mashine hizo za utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka,
aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa ripoti hiyo
tayari imekabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kaboyoka alisema ripoti hiyo baada ya kukabidhiwa kwa Spika Ndugai ataipitia na baadaye kuiwasilisha kwa kamati hiyo ya PAC.
Juni 30, mwaka huu, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya
kuahirisha Bunge la Bajeti aliiagiza serikali kuhakikisha mfumo huo
unafanya kazi kwa ajili ya kuwadhibiti wahalifu na kuitaka Kamati ya PAC
ifuatilie suala hilo.
Dk Tulia alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa yenye utata ya
kuhusu zabuni yenye thamani ya Sh bilioni 37 ya kufunga mashine hizo
katika vituo vyote vya Polisi baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya
Lugumi Enterprises Limited iliyotolewa mwaka 2011.
“Ninashauri serikali ihakikishe mradi huu unakamilika ndani ya
kipindi cha miezi mitatu kuanzia leo…, mradi huu utasaidia Jeshi la
Polisi kuwatambua kwa haraka watu waliohusika katika matukio ya uhalifu
mbalimbali,” alisema.
Katika mkataba huo, Lugumi inatakiwa kusambaza na kufunga mashine
hizo za utambuzi wa vidole katika wilaya 108 za kipolisi nchi nzima.
Hata hivyo, mashine hizo zilifungwa kwenye vituo 14 pekee wakati
tayari kampuni hiyo ilishapokea kiasi cha asilimia 99 za malipo yake.
Katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
ya mwaka wa fedha 2013/14 ilionesha kuwa pamoja na kampuni hiyo ya
Lugumi kulipwa asilimia 99 ya malipo sawa na Sh bilioni 34, bado
haijakamilisha mradi huo kwa muda wa miaka mitano sasa.
Aprili, mwaka huu, PAC iliunda kamati ndogo kwa ajili ya kuchunguza
mkataba huo wa utata baina ya Kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment