KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema wameumia kuondoka kwa
Kocha Mkuu, Hans van Pluijm lakini hawana budi kusonga mbele na
kuhakikisha wanaendeleza ushindi katika michezo iliyoko mbele yao ili
kutetea taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Pluijm alijiuzulu kuifundisha Yanga juzi baada ya uongozi wa timu
hiyo kufanya mazungumzo na Kocha mwingine kutoka Zambia, George
Lwandamina ili kuchukua nafasi yake pasipo kumshirikisha. Kufuatia
kujiuzulu huko, timu hiyo kwa sasa iko chini ya Mwambusi na wasaidizi
wengine waliokuwemo tangu mwanzo hadi uongozi huo utakapoamua hatma yao.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya mchezo dhidi ya JKT
Ruvu Mwambusi alisema walimzoea Pluijm kwani walifanya kazi vizuri na
kwamba ushindi walioupata wa mabao 4-0 walitoa kama zawadi kwake ya
kumuaga.
“Tulimzoea sana kwa sababu tulifanya naye kazi vizuri, ‘tutammis’ na
niseme tu kwamba ushindi wa leo (juzi) tunampa zawadi kwake na kumtakia
kila la heri huko aendako,” alisema.
Mwambusi alisema kuondoka kwa Pluijm hakutawafanya kurudi nyuma,
tayari wamezungumza na wachezaji na kuangalia namna ya kuendelea na
mapambano.
Akizungumzia mchezo dhidi ya JKT Ruvu Mwambusi alisema anashukuru kwa kupata matokeo kwani timu hiyo siku zote huwa ngumu.
Aliomba mashabiki wa Yanga kuendelea kuwaunga mkono ili kutimiza
malengo waliyojiwekea. Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City alisema
wataendelea kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao kuendelea kushinda.
Ushindi wa Yanga umeendelea kuiweka timu hiyo katika nafasi ya pili
ikijivunia pointi 24 katika mechi 11 ilizocheza.
Kwa upande wa Kocha wa JKT Ruvu, Malale Hamsini alisema timu yake
ilikuwa na udhaifu kiasi cha kukubali kufungwa na kwamba wataendelea
kurekebisha mapungufu yao kufanya vizuri.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment