BAADA ya uamuzi wa kuwafukuza vyuo walimu wanne waliokuwa kwenye
mafunzo ya vitendo katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya (Mbeya
Day), serikali imesema vyuo husika vinaweza kushauri adhabu mbadala
iwapo vitajiridhisha kuwepo kwa mazingira tofauti na yaliyozingatiwa
kwenye uamuzi wa kuwafukuza vyuo.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari
mkoani Mbeya alikokuwa katika ziara kwenye shule mbalimbali mkoani humo.
Profesa Ndalichako alisema uamuzi uliochukuliwa na ofisi yake
ulizingatia sheria ndogo zilizotungwa katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (Udsm) zinazoainisha makosa yanayoweza kumfukuzisha chuo
mwanafunzi.
Hata hivyo, alisema uamuzi uliochukuliwa unaweza kutazamwa upya na
vyuo husika iwapo uzito uliochukuliwa na wizara utaonekana kuwa katika
mazingira na uhalisia wa tukio husika.
Walimu wanne waliokuwa kwa vitendo katika shule ya Mbeya Day
walifukuzwa vyuo baada ya uamuzi wa serikali kutokana na kuhusika
kumpiga mwanafunzi Sebastain Chinguku vibao, mateke na fimbo kwa ukatili
Septemba 28 mwaka huu shuleni humo.
Walimu hao walibainika baada ya kipande cha video kusambazwa katika
mitandao ya kijamii hivi karibuni. Waliohusika na vyuo walivyokuwa
wakisoma ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi makofi
kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa DUCE-UDSM, na Evans Sanga
wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Akijibu swali la idadi ipi ya viboko inastahili kutolewa kama adhabu
kwa mwanafunzi anayekwenda kinyume na maelekezo ya shule yake, Profesa
Ndalichako alisema binafsi asingependa mwanafunzi achapwe hata kiboko
kimoja lakini hilo linawezekana pale wanafunzi watakapozingatia maadili.
“Adhabu yoyote kwa mwanafunzi inatolewa pale anapokuwa amekwenda
kinyume na maadili ya shule yake. Kama wanafunzi wote watazingatia
maadili sidhani kama kuna mwalimu atakayempiga mwanafunzi hata kiboko
kimoja. Haya yote yanatokea kutokana na wanafunzi kukosa nidhamu,”
alisisitiza Ndalichako.
Aliwasihi wanafunzi kuzingatia maadili ya shule yao, akisema ndiyo
njia pekee ya kuwawezesha kuishi vyema na walimu wao na pia kufanya
vyema kitaaluma na kuwasihi wazazi kuwafundisha watoto wao nidhamu ya
kuwaheshimu watu wote, akisema malezi hayo yatawapunguzia walimu adha ya
kuishi na wanafunzi watukutu ambao kimsingi wanazorotesha utendaji kazi
wao.
Katika hatua nyingine, wizara hiyo imesema Waraka wa Elimu wa mwaka
2002 namba 24 unaelekeza utoaji wa adhabu ya viboko kwa wanafunzi kuwa
ni lazima kuidhinishwa na mwalimu mkuu kwa maandishi huku kukiwa na
daftari linaloonesha idadi ya viboko alivyopigwa mwanafunzi na mwalimu
aliyemchapa.
Wizara hiyo imeweka bayana utoaji wa adhabu hiyo, lakini imewataka
wanafunzi kujiepusha kufanya makosa mbalimbali yatakayosababisha kupigwa
viboko kwani shuleni wameenda kwa ajili ya kusoma.
Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicholaus Buretta alisema hayo juzi
alipozungumza na gazeti hili kuhusu adhabu anayopaswa kupewa mwanafunzi
na suala zima la maadili kwa wanafunzi na walimu.
Alisema adhabu hiyo ya viboko hutolewa kwa kuangalia ukubwa wa kosa,
jinsi ya mwanafunzi, afya yake pamoja na kuhakikisha viboko hivyo
havizidi vinne kwa mwanafunzi tena hutolewa na mwalimu mkuu au mwalimu
aliyethibitishwa na mwalimu mkuu kwa maandishi.
“Katika adhabu hiyo ni lazima mtoto wa kike apigwe viboko na mwalimu
wa kike labda kama shule hiyo haina mwalimu wa jinsia hiyo, hivyo
mwalimu mkuu atatoa maelekezo ya jinsi ya kumuadhibu. “Hatuhamasishi
adhabu hii kwa wanafunzi, bali wanafunzi wanatakiwa kujua kuwa wamekuja
shuleni kusoma na hawajaja kuchapwa viboko, hivyo lazima wajiepushe
kufanya makosa yatakayosababisha kuchapwa, huku tukihamasisha mahusiano
bora kati ya mwalimu na mwanafunzi ambayo ni yale ya kama mzazi,”
alisema Buretta.
Buretta alisema katika kuboresha uhusiano baina ya walimu na
wanafunzi, wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) itahakikisha wanafikia wastani wa darasa
moja kuwa na wanafunzi 1:40 hadi 45.
Kwa upande wao, Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo
binafsi Tanzania (Tamongsco) limetaka walimu kufuata waraka maalumu wa
serikali katika kuadhibu wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuwa karibu na
wanafunzi mara wanapokosea.
Imeandikwa na Joachim Nyambo, Mbeya na Theopista Nsanzugwanko, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment