MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), ameiambia Mahakama Kuu
Kanda ya Mwanza, kwamba alishinda uchaguzi wa ubunge uliofanyika mwaka
jana.
Bulaya aliyasema hayo mahakamani hapo jana mjini Musoma kupitia kwa
wakili wake, Tundu Lissu, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Sumbawanga, Noel Chocha, anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo yake
iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen Wassira.
Katika utetezi wake baada ya kuapa, Bulaya alisema alitangazwa na
msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo baada ya taratibu zote ikiwamo
kuhesabu kura, kukamilika.
Baada ya utetezi huo, malumbano ya sheria baina ya mawakili wa upande
wa waleta maombi na wajibu maombi yaliibuka na kudumu kwa zaidi ya saa
tatu.
Malumbano hayo yalianza baada ya Wakili wa Waleta maombi, Costantine
Mutalemwa, kuiomba mahakama hiyo iondoe aya saba kati ya 11 zilizokuwa
kwenye utetezi wa Bulaya kwa kile alichodai hazimo kwenye utaratibu wa
awali uliowasilishwa mahakamani hapo.
Aya ya saba ya utetezi wa Bulaya inadai kasoro ya kura 164,794
zilizotangazwa awali na msimamizi wa uchaguzi badala ya kura 69,369 za
wapiga kura halali, hazikuathiri matokeo.
Wakili Mutalemwa alidai kwamba, madai yaliyotokea kwenye utetezi wa
mbunge huyo ni mapya na suala la idadi ya wapiga kura ni moja ya
kipengele ambacho wateja wake wanakipinga.
“Naomba mheshimiwa jaji aya ya pili, tatu, nne, tano, sita, saba na
nane, ziondolewe kwenye utetezi wa Bulaya na zibaki aya ya kwanza, ya
tisa, ya 10 na aya ya 11.
“Naomba aya hizo ziondolewe kwa sababu ni mpya na hazipo kwenye utaratibu wa awali,” alidai Wakili Mutalemwa.
Kutokana na maombi hayo, Lissu alisema hakubaliani na pingamizi la wakili huyo.
Alisema amekumbuka kauli ya aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Mahakama ya
Afrika Mashariki, Sir Charz Nyubon aliyewataka mawakili wasiweke
mapingamizi yasiyo na msingi.
“Kitendo cha mawakili kuweka mapingamizi yasiyo na msingi ni kupoteza
muda wa mahakama kwa mujibu wa kauli ya rais huyo na nakuomba
mheshimiwa jaji uendelee na ushahidi wa mtoa ushahidi kwa kuwa muda wa
kupoteza kwenye ushahidi haupo,” alisema Lissu.
Naye Wakili wa Serikali, Angela Lushagamba, alisema hana pingamizi
lolote kwenye kiapo cha utetezi wa Bulaya uliotolewa mahakamani hapo na
kuiomba mahakama iendelee kusikiliza ushahidi.
Akitoa uamuzi juu ya hoja zilizoibuka mahakamani hapo, Jaji Chocha,
alisema anaona dalili za shauri hilo kusikilizwa kwa muda mrefu kutokana
na hoja mpya zilizoibuka mahakamani.
“Kuna vitu vipya ambavyo vimeibuka kwa siku ya leo na nahitaji nipate
muda zaidi ya saa tano kuvifanyia kazi,” alisema Jaji Chocha huku
akiahirisha kesi hiyo hadi leo saa saba mchana.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment