ALIYEKUWA Meya wa Jiji la Dar es Salaam Dk. Didas Masaburi amefariki dunia.
Masaburi ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki
(EALA), alifariki jana saa 3:30 usiku katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii kuanzia saa 4 usiku na baadaye kuthibitishwa na wanafamilia.
Akizungumza na MTANZANIA ndugu wa marehemu, Dk. Makongoro Mahanga,
alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na yupo kwenye maandalizi ya
kuelekea nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya vikao.
“Taarifa za kifo ni za kweli ingawa kwa jioni hii sijakwenda
hospitali, ninafanya mawasiliano na familia ila taarifa kamili kuhusu
msiba zitakuwa zikitolewa na msemaji wa familia ambaye usiku huu
tutamteua na kesho (leo) tutaeleza kwa undani,”alisema Dk. Mahanga
Naye Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge (CCM), alisema
kifo cha Masaburi ni pigo kwa chama pamoja na wakazi wa jijini Dar es
Salaam.
“Ni kweli kaka Masaburi ametotoka (amefariki) usiku huu wa leo (jana)
saa 3:30 na alikuwa Muhimbili kwa siku kama tano pale ICU (wodi ya
wagonjwa mahututi) na tunamumbea mwenzetu ambaye ametangulia mbele ya
haki,” alisema Mnyonge
Wasifu wake
Mwaka 1995, Dk. Masaburi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar e Salaam .
Mbali na hilo pia alibahatika kuwa na Shahada ya Juu ya Masuala ya
Ugavi iliyotolewa na Bodi ya Uhasibu ya Taifa (NBAA), huku kwa miaka
kadhaa akifanikiwa kuwa mfanyakazi wa Kiwanda cha vinywaji cha Chibuku.
Pia amefanyakazi Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo kupitia mradi
maalumu wa Benki ya Dunia (WB) na amekuwa akimiliki Shule ya Sekondari
ya Dk. Didas Masaburi iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam pamoja na
anamiliki Chuo cha Ugavi na Manunuzi kilichopo Chanika.
Dk. Masaburi alikuwa akiishi na figo moja kwa tangu mwanzoni mwa miaka 2000 hadi mauti yanamkuta.
Safari ya siasa
Mwaka 2015, marehemu Dk. Didas Masaburi, alijitosa katika
kunyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambapo alishindwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Saed
Kubenea ambaye alitangazwa kuwa mbunge hilo kwa kura 87,666 huku
Masaburi akipata kura 59,514.
Mwaka 2010, Dk. Masaburi alichanguliwa kuwa Diwaniwa wa Kata ya
Kivukoni na Desemba 23, akachaguliwa kwa Meya mpya wa Jiji la Dar es
Salaam, kwa kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi
uliofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo
aliwashinda wapinzani wake, Diwani wa Kata ya Tandale, Amir Mbunju
(CUF).
Meya huyo wa zamani alichaguliwa kwa kura 125 huku wajumbe wanne kati yao hawakupiga kura na 9 ziliharibika.
Kauli tata za kukumbukwa
Agosti 6, mwaka 2011, Dk. Masaburi aliingia katika malumbano ya
wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao walimtaka ajiuzulu kutokana na
kukiuka taratibu katika uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam
(UDA).
Kutokana na hali hiyo meya huyo wa zamani alijibu mapigo dhidi ya
wabunge hao ambapo alisema baadhi yao wanashindwa kufikiri kwa kutumia
vichwa na badala yake wanafikiri kwa kutumia ‘makalio’.
Alisema wabunge katika kuchangia hoja ya suala la UDA wamegawanyika
katika mafungu matatu ambao alisema katika mafungu hayo moja halijui
lolote kuhusiana na sakata hilo na limedandia tu hoja.
Alitaja kundi la pili kuwa ni la wabunge wa jiji la Dar es Salaam
ambao ni Mbunge wa Ubungo wa wakati huo, John Mnyika, na Mbunge wa Kawe,
Halima Mdee, ambao alisema wanatafuta umaarufu wa kisiasa kupitia
sakata la UDA.
Alisema Mnyika aliweza kuhoji hata katika vikao rasmi, lakini Mdee hajui
chochote kwa kuwa hajawahi kuhudhuria vikao vya jiji mpaka sasa.
Aidha, kundi la tatu ambalo ndilo alilituhumu zaidi kufikiri kwa
kutumia “makalio” badala ya kichwa ni la wabunge Abasi Mtemvu aliyekuwa
(Temeke), Mussa Azzan ‘Zungu'(Ilala) na Dk. Makongoro Mahanga aliyekuwa
(Segerea) ambao alidai kuwa wanajua ukweli wa jambo hilo lakini
wanapotosha ili kuficha madhambi yao ambayo alisema yataibuliwa muda si
mrefu ya ufisadi ndani ya jiji hilo.
Escrow yamuibua
Kutokana na sakata hilo ambalo liliitikisa Serikali ya awamu ya nne
chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Dk. Masaburi alijitokeza hadhani
baada ya makombora kutoka kwa wabunge na kutaka kiongozi huyo wa nchi
kutobebeshwa mzigo huo.
Alisema Rais Kikwete amefanyakazi kubwa ya kuhakikisha anawashughulikia waliohusika hivyo hastahili kuingizwa kwenye kapu hilo.
Tukio la mwisho
Kabla ya kufikiwa na mauti Dk. Masaburi alipelekwa nchini India mara
mbili kwa ajili ya matibabu na kwa mara ya mwisho alionekana hadharani
Serena Hoteli ambapo alikwenda kutoa mada kuhusu masuala ya manunuzi.
Baada ya kutoa mada akiwa njiani anarejea nyumbani kwake alijisikia
vibaya na shinikizo la damu kushuka ambapo alikwenda hospitali kwa
matibabu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment