MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali maombi
yaliyowasilishwa na Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi(CUF) ya
kutaka kuwasilisha maombi katika kesi ya msingi ya kufuta uamuzi wa
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wakumtambua Mwenyekiti
wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Katika kesi hiyo, Bodi ya Wadhamini ambayo iliwakilishwa na Wakili
Juma Nassoro, aliitaka mahakama hiyo kuweka zuio maalumu kwa Msajili wa
Vyama vya Siasa kuacha kufanya kazi nje ya mipaka yake na kuingilia
maswala ya chama hicho kinyume cha taratibu.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaama, Ama –Isario Munisi alisema mahakama hiyo imeridhia kuwasilishwa
kwa maombi ya kesi ya msingi ndani ya siku saba ili ianze kusikilizwa.
“Mahakama imeridhia hoja ya mleta maombi ya kutaka kuwasilisha maombi
ya kesi ya msingi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa
Chama cha Wananchi, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama wengine 12
waliomo kwenye kesi hii,”alisema Jaji Munisi.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, Wakili Nassoro alidai sasa wanakwenda
kujipanga ili ndani ya siku saba waweze kuwasilisha maombi hayo.
“Tunashukuru mahakama imekubali maombi yetu, kilichobaki ni kwenda
kujipanga ili tuweze kuwasilisha maombi katika kesi ya msingi dhidi ya
walalamikiwa wetu,”alidai.
Katika kesi hiyo, Wakili Nassoro alidai mahakamani hapo, kuwa mbali
na kuweka zuio hilo kwa msajili, pia kesi hiyo imelenga waliokuwa
wanachama 12 wa chama hicho wakiongozwa na Profesa Lipumba.
Alidai hoja nyingine katika kesi hiyo, ni pamoja na kumtaka msajili
kutengua uamuzi wa kumrudisha Profesa Lipumba kwenye nafasi yake kwa
madai alishavuliwa uanachama.
Alidai kitendo cha kiongozi huyo kuvamia ofisi za chama hicho na
kuikalia kinyume cha sheria pamoja na kuharibu baadhi ya mali za chama
hicho hakikubaliki.
Akizungumza nje ya mahakama, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF,
Julius Mtatiro alisema kitendo cha msajili kuziandikia barua Benki za
NMB na Exim ili Profesa Lipumba aweze kufungua akaunti na kumpa ruzuku
kinapaswa kupingwa.
Alisema mwenye mamlaka ya kuandika barua kwenda katika benki hizo, ni
bodi ya wadhamini ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia mali za
chama.
Alisema bodi hiyo ambayo imesajiliwa na Wakala wa Ufilisi na
Udhamini(RITA) ambayo inawajibika chini ya Baraz aKuu la Uongozi la
Taifa na sio msajili au mwanachama aliyefukuzwa.
“Tunamshangaa Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kumwandikia barua
Lipumba, huku akijua kufanya hivyo ni kosa, kwa sababu wenye mamlaka ni
bodi ya wadhamini,”alisema Mtatiro.
Alisema katika mchakato huo, bodi ya wadhamini kwa kushirikiana na
Katibu wa Bodi wanapaswa kuandaa vikao kwa ajili ya kujadili suala hilo
kabla ya kufikia uamuzi huo.
Alisema mpaka sasa bodi hiyo imeshangazwa na uamuzi wa Profesa
Lipumba wa kufungua akaunti hiyo, huku ikihoji mahala alipozitoa nyaraka
muhimu.
“Tunaamini Lipumba ameghushi nyaraka za kufungulia akaunti katika
Benki ya Exim, kwa sababu wenye nyaraka hizo ni bodi ya wadhamini na si
yeye kwa sababu ndiyo wanaosimamia masuala ya fedha na mali za chama
chini ya Katibu Mkuu wa chama, Maalim Seif Sharif Hamad,”alisema.
Alimtaka Msajili kuacha kuingilia mausla ya chama hicho kwa madai
kuwa kipindi hiki siyo cha Chama Cha TLP au NCCR-Mageuzi, bali ni zama
za CUF ambao wamesimama imara kwa ajili ya kuhakikisha haki inatendeka.
Alisema kutokana na hali hiyo, chama hicho kimejipanga ili
kuhakikisha kuwa suala hilo linamalizika kwa haki katika mahakama hiyo.
Hata hivyo, Msajili Msaidizi waVyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema
barua aliyopewa Profesa Lipumba kwa ajili ya kufungua akaunti ni sawa
na barua ya serikali za mitaa.
“Lipumba amepewa barua ya utambulisho kama zilivyo barua za Serikali
za mitaa kwa sababu kila chama kinapopata mwenyekiti mpya kinapaswa
kuwasilisha barua ya kumtambua mwenyekiti huyo ndani ya ofisi hizo,
lakini mpaka sasa Ofisi ya Msajili haijapokea barua yoyote ya
kutomtambua Lipumba kama si mwenyekiti wa chama,”alisema Nyahoza.
Alisema taarifa za kuwapo baadhi ya viongozi wa chama hicho kuonana
na msajili hazijafika kwenye ofisi hiyo kwa sababu vikao vyote
vinavyofanyika vina utaratibu wake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment