POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imefanya operesheni katika
maeneo ya katikati na pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam na kuwakamata
watuhumiwa 87 wa makosa mbalimbali, wakiwemo waliokuwa kwenye mtandao wa
uhalifu wa mkazi wa Machimbo Yombo jijini Dar es Salaam, Salum Njwele
(34) maarufu kama ‘Scorpion’.
Njwele alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mwishoni mwa
wiki, kujibu mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa
macho yote mawili Said Mrisho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda
wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi Simon Sirro alisema watuhumiwa
wengine wanadaiwa kuvunja nyumba na kuiba na wengine walipatikana na
gongo lita 148, bangi kete 95 na puli 48.
Alisema watuhumiwa hao, wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo
ya Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana,
Kunduchi, Keko, Kawe.
“Watuhumiwa hao walipatikana na makosa mbalimbali yakiwemo kuvunja
nyumba usiku na kuiba maarufu 10 ndani 10 nje, kuvuta na kuuza bhangi,
kuuza na kunywa gongo, kupiga debe, uzembe na uzururaji,” alisema
Kamanda Sirro.
Katika tukio lingine, watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi
wamekamatwa wakiwa na silaha aina ya MARK IV ikiwa imekatwa kitako
chake.
Watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 10 mwaka huu saa 3:30 asubuhi huko
maeneo ya Vingunguti wakiwa na pikipiki yenye namba MC 787 BEP aina ya
Boxer ikiwa kwenye jaribio la kufanya tukio la ujambazi katika eneo la
viwandani.
Alisema Kikosi Maalumu cha Kupambana na ujambazi wa kutumia silaha
kiliwafuatilia na watuhumiwa hao baada ya kuona hivyo walianza kufyatua
risasi hovyo kuelekea kwa askari na ndipo askari walijibu mashambulizi
na kuwajeruhi wote wawili na kuchukua silaha hiyo, ikiwa na risasi tano
kwenye magazine moja tayari kwa kufyatuliwa.
Alisema taarifa za awali zimebaini kwamba watuhumiwa hao ambao majina
yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, walikuwa wamejipanga
kuvamia kiwanda kimojawapo maeneo ya Vingunguti. Alisema watuhumiwa hao
walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu
hali zao zikiwa mbaya kutokana na majeraha ya risasi.
Alisema upelelezi zaidi wa tukio hilo unaendelea.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment