MENEJA
wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Dodoma,
Mhandisi Zakayo Temu amesema ni vema mkoa huo ukapewa hadhi ya mkoa
maalum ili uweze kukabiliana na changamoto za ujio wa Serikali Dodoma.
Ametoa
ombi hilo jana jioni (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati akitoa taarifa
ya utendaji wa TANESCO Mkoa wa Dodoma mbele ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa ambaye alifika kwenye kituo cha kupozea umeme cha Zuzu nje
kidogo ya mji wa Dodoma, kukagua mahitaji halisi ya umeme ikilinganishwa
na ujio wa watumishi mkoani humo.
Mhandisi Temu alisema: “Tunaomba
mkoa wetu wa Dodoma ambao ni Makao Makuu uangaliwe kwa jicho la pekee na
kupewa hadhi ya mkoa maalum kama ilivyo kwa Dar es Salaam ambako kuna
mikoa minne ya ki-TANESCO.”
“Dar es Salaam ina mikoa minne ya Ilala,
Kinondoni, Temeke na Mikocheni. Mkoa wetu unatakiwa kubeba majukumu yote
ya Serikali kama yanavyofanyika hivi sasa katika Jiji la Dar es Salaam.
Hivyo, tunaomba tupewe kipaumbele kwenye rasilmali watu, usafiri na
vitendea kazi,” alisema.
Alisema TANESCO inabidi iende kwa kasi zaidi ili kumudu wimbi la wafanyakazi wanaohamia Dodoma.
Akifafanua
kuhusu uboreshaji wa miundombinu iliyopo, Mhandisi Temu alisema
kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Iringa
mpaka Shinyanga kupitia Dodoma, kumeboresha upatikanaji wa umeme kwenye
mji wa Dodoma.
“Umeme unapatikana ukiwa na voltage nzuri na
hauchezichezi na hivi sasa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara
limepungua kwa kiasi kikubwa. Kukamilika kwa njia hii kunaleta uwezekano
wa kufanya matengenezo kwenye njia moja ya umeme bila kuathiri
upatikanaji wa umeme kama ilivyokuwa awali,” alisema.
Alisema kazi
inayoendelea hivi sasa ni kubadilisha nguzo za umeme zilizochakaa;
kubadilisha njia za msongo wa kilovolti 11 kwenda kilovolti 33 zenye
urefu wa km. 85 na transforma 74 ili kupunguza upotevu wa umeme na
kuingiza njia hizo kwenye njia mpya ya 132/33kV katika maeneo ya
manispaa ambayo yanapata umeme kupitia njia za 11kV.
Alisema mbali
ya kusambaza umeme kwa njia ya mzunguko wa mji (ring circuit),
wataongeza vituo vikubwa viwili vya kupozea umeme katika maeneo ya
Msalato na Kikombo.
Mhandisi Temu alisema wameanza kuboresha
miundombinu ya umeme ili kuwezesha baadhi ya wilaya za mipakani zipate
umeme kutoka mikoa ya jirani wakati wa matengenezo au kukiwa na hitilafu
za umeme.
“Tunapanga wilaya ya Gairo ipate umeme kutoka Morogoro;
Bahi ipate umeme kutoka Manyoni; Mpwapwa hasa maeneo ya Chipogolo yapate
umeme kutoka Ruaha Mbuyuni ambako ni karibu zaidi. Pia tunataka wilaya
ya Kiteto ipate umeme kutoka Dodoma badala ya Babati kama ilivyo hivi
sasa,” alisema.
Alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba umeme unaozalishwa
na kituo cha Zuzu unatosha mahitaji ya sasa na hata baadaye kwani
wanazalisha megawati 48 wakati mahitaji ya juu ni megawati 25 na hivyo
kubakiwa na ziada ya megawati 23.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa aliwaagiza viongozi wa TANESCO mkoa wa Dodoma wahakikishe
wanapeleka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili
wanaonunua wakute huduma hiyo ipo tayari.
“Nimeongea na watu wa idara
ya maji, nimewaambia wapeleke miundombinu yao katika maeneo yanayopimwa
viwanja. Na ninyi pia mfanye hivyo kama ambavyo watu wa TAMISEMI
walijenga barabara za lami katika viwanja vipya vya makazi ili watu
wakienda kununua wakute huduma hiyo ipo tayari,” alisema.
“Nimefarijika
kukuta kwamba Dodoma hatuna shida ya umeme, hatuna mgao, kwa hiyo
endelezeni kazi hii nzuri mnayoifanya,” alisema Waziri Mkuu.
Home
News
Slider
Tanesco yaomba kupewa hadhi ya mkoa maalum katika kukabiliana na ujio wa Serikali Dodoma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment