WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu
wa taasisi zote za serikali mkoani Dodoma ambao wamelimbikiza deni la Sh
bilioni 1.4 zikiwa ni ankara zao za maji.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi na
viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (Duwasa), baada ya
kukagua utendaji kazi wa chanzo cha maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji
wa Dodoma.
“Niletee haraka orodha ya wadaiwa wote wa Ofisi za serikali na
taasisi za umma ambao hawajalipa ankara zao. Madeni yote ni lazima
yalipwe,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua
maandalizi ya serikali kuhamia Dodoma, anatembelea sehemu mbalimbali za
kutolea huduma za jamii pamoja na kukagua miundombinu ya mkoa huo.
Aliutaka uongozi wa Duwasa na watumishi wote wahakikishe wanaboresha
huduma za upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili
wananchi au wawekezaji wanaponunua viwanja wakute huduma hiyo ipo na
waanze ujenzi mara moja.
“Tumealika wawekezaji, nataka wajenge viwanda na mahoteli hapa
Dodoma, sasa wakikuta maji na umeme kwenye maeneo yao, itakuwa ni
kichocheo cha kuharakisha kazi za ujenzi,” alisema na kumwagiza Mkuu wa
Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme ahakikishe eneo lililo jirani na
chanzo hicho cha maji halikaliwi na mtu yeyote na linalindwa dhidi ya
uchomaji moto.
“Uchomaji moto uoto wa asili umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni
tatizo kubwa hapa nchini na halina budi kusimamiwa hadi liishe,”
alisisitiza.
Alifikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Duwasa, David Pallangyo kwamba kuna wananchi wameanza
kujenga na kufanya shughuli za kijamii jirani na chanzo hicho licha ya
kuwa walikwishaondolewa zamani.
Kuhusu wadaiwa sugu, Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za serikali ndiyo wanaongoza kwa kulimbikiza madeni.
“Wananchi wa kawaida wapo wanaodaiwa lakini deni lao siyo kubwa na
hao tunawamudu,” alisema wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii.
Alisema tatizo lingine linalowakabili ni uchomaji moto ambapo hivi
karibuni uliwashwa moto na kuunguza baadhi ya nguzo za umeme ambazo
zinapeleka umeme kwenye chanzo hicho. Alisema askari wa JKT Makutupora
walisaidia kuzima moto huo ili usifike kwenye mitambo mingine ya chanzo
hicho cha maji.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment