NI vilio kila kona sekta ya afya nchini kutokana na wagonjwa wanaofika katika hospitali mbalimbali kwa matibabu kukosa dawa.
MTANZANIA imefanya utafiti katika hospitali mbalimbali nchini na kubaini hali hiyo, huku mamlaka husika zikitupiana lawama.
Hatua ya kukosekana kwa dawa na vifaa tiba muhimu katika vituo vya
kutolea huduma vya umma nchini, kumeelezwa kuathiri zaidi wananchi wasio
na bima za afya na wale wenye bima zenye wigo mdogo.
Ukosefu huo wa dawa kwa sasa umekuwa mkubwa, hali inayotishia kutokuwapo uhakika wa huduma kwa wagonjwa katika vituo vya afya.
Kwa mujibu wa takwimu, inaelezwa kuwa asilimia 80 ya wananchi hawamo
katika mfumo wowote wa bima za afya, na inapotokea uhaba wa dawa na
vifaa tiba, hujikuta wakiathirika zaidi kwani hulazimika kutumia gharama
kubwa kupata huduma, na wakati mwingine hukosa kabisa.
Imeripotiwa kuwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imefikia hatua ya kutoagiza
dawa kama njia ya kulinda mtaji wake ambao umekuwa ukizidi kutetereka
kutokana na madeni yanayozidi kulimbikizwa serikalini pamoja na vituo
vya kutolea huduma.
HOSPITALI ZILIZOKUMBWA
Baadhi ya hospitali zilizokumbwa na kadhia ya kukosa huduma MSD, ni
pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean
Road, hospitali za wilaya za Kiteto, Mpwapwa na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa uchunguzi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa na MSD zaidi ya Sh bilioni 90.
Baadhi ya hospitali zinazodaiwa na MSD ni Muhimbili (Sh bilioni 8) na Hospitali ya Wilaya ya Kiteto (Sh milioni 38).
HALI MIKOANI
Baadhi ya wagonjwa mkoani Songwe wameilalamikia hatua ya Serikali
kushindwa kupeleka dawa hospitalini hali inayowalazimu kwenda kununua
katika maduka binafsi.
Akizungumza na MTANZANIA katika Hospitali ya Wilaya ya Vwawa, mmoja
wa wagonjwa hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Jackson, alisema
hatua ya kukosa dawa imekuwa ni mateso kwa wagonjwa hasa wanaotoka
maeneo ya vijijini kwa lengo la kupata huduma kwenye hospitali ya
Serikali.
“Nimeandikiwa dawa na daktari na kwenda katika dirisha la dawa,
lakini nimekwama, nimefika pale nimeambiwa hakuna dawa. Kwa hali hii
tupo kwenye mateso sisi Watanzania maskini.
“Dawa hakuna na sasa nimeambiwa niende katika duka la Flashlight
ambalo lipo nje ya hospitali, haya ni mateso makubwa sana kwetu ndugu
yangu,” alisema Jackson.
Hata hivyo, baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo ambao hawakutaka
kuandikwa majina yao gazetini, walikiri kuwapo uhaba wa dawa aina ya
Ciprofloxacin Caps, Paracetamol na Phenobarbital.
Akizungumzia hali hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk. Samweli
Lazaro, alisema katika mkoa wake kuna asilimia 72 ya upatikanaji wa dawa
na asilimia 28 ni upungufu.
ARUSHA
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti, amekiri kuwapo
upungufu wa baadhi ya dawa katika hospitali za mkoa huo alipoulizwa na
MTANZANIA kuhusu hali hiyo.
“Kuna dawa ambazo tunazo na nyingine hatuna. Lakini bosi wangu
ameshazungumzia suala hilo, mimi ni nani nizungumze tena?” alisema Dk.
Mokiti.
MBEYA
Taarifa kutoka mkoani Mbeya zinaeleza kuwa ukosefu wa dawa na vifaa
tiba umeutikisa mkoa huo na vituo vyake vya afya hali inayowafanya
wananchi kupata huduma hiyo kwa gharama kubwa.
Wakizungumza na MTANZANIA mapema wiki hii kwa nyakati tofauti, baadhi
ya wagonjwa waliokutwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini mkoani Mbeya, walisema upatikanaji wa dawa za magonjwa
mbalimbali ya binadamu ni mgumu, hivyo inawalazimu kwenda kuzitafuta
katika maduka ya watu binafsi.
“Nimeandikiwa dawa na daktari, lakini nimeenda dirishani naambiwa
dawa zimeisha, hivyo niende kununua nje katika maduka ya watu binafsi,
jambo ambalo kwangu ni gumu kutokana na kiasi cha fedha nilichokuwa
nacho,” alisema Joram Mwafwile mkazi wa Sae jijini Mbeya.
Alisema amekaa zaidi ya saa nne hospitalini hapo akisubiri kupata
huduma ya dawa, lakini jitihada hizo zinaonekana kushindwa hivyo kuamua
kurejea nyumbani kuangalia njia nyingine atakayoweza kutatua tatizo
hilo.
Nao Mariamu Nkinda, Atupele Asajile na Jimmy Mwakyusa, wakazi wa
maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya, wao walisema kuwa tatizo la dawa
limekuwa kubwa kwani ukiacha dawa za ugonjwa wa makaria ambazo angalau
zinapatikana, lakini za magonjwa mengine makubwa hazipatikani.
Mwakyusa alisema kuwa wanachofanyiwa hospitali kwa sasa ni kupata
huduma za vipimo na daktari kusoma, lakini wakienda kwenye madirisha ya
dawa huambiwa dawa hakuna na kulazimika kwenda kuzitafuta nje ya
hospitali ambako nako imekuwa adimu kuzipata.
“Kweli upatikanaji wa dawa kwa bei nafuu umekuwa ni mgumu, maisha
magumu, hela hakuna, hivyo kilichobaki kwetu sisi ni kumwomba Mungu tu
au tuingie kwenye matibabu ya miti shamba,” alisema.
Baadhi ya madaktari ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini,
walisema hali ya dawa ni mbaya na kwamba wao wanashindwa kuwasaidia
wagonjwa hasa wale ambao wanalazwa wodini.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk.
Yahaya Msuya, alikiri kwamba wanakabiliwa na changamoto hiyo kwa baadhi
ya dawa, lakini hawezi kulisemea kwa upana hadi ofisi yake
itakapojiridhisha kwa kupokea taarifa kutoka wilayani.
Akizungumzia hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja,
alikiri baadhi ya halmashauri kukabiliwa na madeni na kwamba MSD
ilishatoa waraka ambao ulibainisha vigezo na masharti ya utoaji wa dawa
hizo.
“Waraka huo uliainisha vigezo mbalimbali, lakini kikubwa kilikuwa ni
kwamba halmashauri ambazo zitashindwa kulipa madeni yake ya nyuma basi
zitasitishiwa huduma hiyo hadi zitakapomaliza deni, lakini ofisi
ilizitaka halmashauri kutekeleza waraka huo kwa vitendo ifikapo mwezi
huu,” alisema Mariam.
DODOMA
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Charles Kiologwe,
alisema katika mkoa wake kuna dawa za kutosha kutokana na Serikali
kutaka kuufanya kuwa mkoa wa kitiba.
Alisema hospitali zilizopo mkoani Dodoma; ya magonjwa ya akili
Mirembe, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Chuo Kikuu ya Dodoma (Udom), St.
Jemma na DMC pamoja na zile za wilaya zote zina dawa za kutosha.
Dk. Kiologwe alisema kilichopo sasa hivi ni kwamba hawaagizi dawa
mbili zinazotibu ugonjwa mmoja, bali wanaagiza kulingana na mahitaji ya
wagonjwa.
HOSPITALI MWANANYAMALA
Wakizungumza na MTANZANIA juzi, baadhi ya wagonjwa katika Hospitali
ya Mwananyamala, Dar es Salaam, walisema kuwa suala la ukosefu wa dawa
limekuwa likiwatesa na kushindwa la kufanya.
“Dawa hakuna, lakini viongozi wanafanya siasa na sisi maskini
tunakufa, Mungu wangu njoo utuokoe Watanzania sisi tunaojikongoja,”
alisema mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina moja la Alex.
TANGA
Hali katika Mkoa wa Tanga inaelezwa si ya kuridhisha huku baadhi ya
wagonjwa kulazimika kukimbilia katika Hospitali ya KCMC mkoani
Kilimanjaro baada ya kukosa huduma na baadhi ya vipimo.
“Nimekaa muda mrefu bila mafanikio na sasa nimeona ni vema kesho
(leo) niende KCMC maana hapa Bombo hali imekuwa mbaya na nikifanya
mchezo huu mguu ninaweza kuukosa. Maumivu ni makali sana, ninahisi dawa
za kueleweka hakuna, basi ni shida,” alisema mmoja wa wagonjwa
aliyezungumza na MTANZANIA.
RUVUMA
Katika Mkoa wa Ruvuma hali ya upatikaji wa dawa pia si ya kuridhisha,
huku wagonjwa wakilazimika kutafuta maduka ya dawa nje ya hospitali.
Monica Mapunda, alisema wiki ya pili sasa analazimika kwenda kununua
dawa nje ya hospitali ili mgonjwa wake aliyelazwa hospitali ya mkoa
aweze kuendelea na dozi.
“Hapa ndani hospitali hakuna dawa na sasa tumelazimika kama familia
kuchangishana fedha ili kuweza kumudu gharama za kununua dawa katika
maduka ya nje ya hospitali,” alisema.
MGANGA MKUU WA SERIKALI
MTANZANIA ilimtafuta Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Bakari
Kambi, ambaye alisema suala hilo hawezi kulizungumzia kwa kuwa bosi
wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu, tayari amelitolea ufafanuzi.
“Mimi siwezi kuzungumzia masuala ambayo tayari bosi wangu ameyaongelea na kuyatolea ufafanuzi,’’ alisema kwa ufupi.
MSD
MTANZANIA ilipomtafuta Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD),
Laurian Bwanakunu, simu zake hazikupatikana hadi tunakwenda mtamboni, na
alipotafutwa Ofisa Habari, Etty Kusuluka, alisema mkurugenzi ndiye
msemaji na yeye anaweza kuzungumza kwa ruhusa yake.
“Naomba umtafute Mkurugenzi ndiye msemaji mkuu akikuruhusu unitafute mimi ndiyo nitazungumza,” alisema Etty.
MAT YAJIVUA
MTANZANIA ilipomtafuta Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk.
Meshack Shimwela, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na kwamba
watafutwe Baraza la Famasia Tanzania.
“Mimi nazungumzia mambo ya ‘professional’ (taaluma), siwezi
kuzungumzia upungufu wa dawa, labda uwatafute watu wa Baraza la Famasia
ndio wanaohusika na suala hilo,” alisema.
SIKIKA YAISIKILIZIA SERIKALI
MTANZANIA ilipomtafuta Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la
Sikika, Irenei Kiria, alisema Serikali imekwishaahidi kushughulikia
suala hilo baada ya utafiti wao, hivyo wanasubiri kuona inavyotekeleza
suala hilo.
“Sisi baada ya utafiti wetu, tunasubiri kuona Serikali inavyotatua
suala hilo kama ambavyo imekuwa ikiahidi katika vyombo vya habari, kwa
sasa hatuwezi kuongezea zaidi.
“Suala la kununua na kusambaza dawa linafanyika kwa mchakato, si la
kufanya kwa siku moja kama kwenda kununua dawa dukani, hivyo lazima
tusubiri tuone,” alisema Kiria.
Katika ripoti yake ya utafiti iliyoitoa hivi karibuni, Sikika
ilieleza kuwa katika kipindi cha Machi hadi Septemba mwaka huu, mwenendo
wa dawa muhimu ulikuwa kati ya sifuri na kwa viwango ambavyo
havitoshelezi mahitaji.
Sikika ilieleza kuwa kwa mujibu wa takwimu hizo katika kipindi hicho
kulikuwa na akiba ya makopo 173 ya vidonge vya Panadol kwa nchi nzima
huku vifaa vya kujifungulia wanawake wajawazito navyo vimekosekana kwa
miezi miwili mfululizo.
Taarifa za ndani zilieleza kwamba hali hiyo imetokana na Serikali kushindwa kupeleka fedha za bajeti ya dawa MSD kwa wakati.
WAGANGA WAJIVUA
Oktoba 17, mwaka huu waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini
walijivua lawama kwa kumlilia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
wakidai kuwa tatizo la ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya
afya nchini limekuwa likisababisha malalamiko kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa wataalamu wa sekta ya afya,
Mwenyekiti wa waganga hao, Dk. Sudi Leonard, alisema tatizo la ukosefu
wa dawa na vifaa tiba limekuwa likizua manung’uniko kutoka kwa wananchi
pindi wanapokuwa wanahitaji huduma za tiba.
“Mheshimiwa makamu wa rais, pamoja na mambo yote, lakini tuna
changamoto ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba. Hali hii imekuwa
ikisababisha malalamiko kwa wananchi.
“Upatikanaji wa dawa pia umekuwa ukichukua mchakato mrefu kutoka MSD
mpaka kufika sehemu husika, pia kuna hili kundi la watu maalumu na wao
wanapokosa hulalamika,’’ alisema Dk. Leonard.
SERIKALI
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais Samia alikiri
kuwapo uhaba wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za Serikali nchini.
Alisema hata hivyo uhaba wa dawa nchini ni changamoto ya muda mfupi
kwani Serikali inatafuta ufumbuzi wa haraka kuwahudumia wananchi.
Samia alitoa kauli hiyo siku chache baada ya Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kusema hakuna
uhaba wa dawa nchini.
“Tumetenga bilioni 70/- kwa ajili ya kumaliza tatizo la dawa nchini,
pia tumetenga jumla ya Sh bilioni 85 kwa ajili ya kupunguza deni MSD.
Nia yetu ni kutaka huduma za afya ziwe zenye ubora,’’ alisema.
Samia alisema Serikali ina mpango wa kujenga kiwanda cha dawa katika
Mkoa wa Simiyu ili kuweza kukabiliana na tatizo la dawa hapa nchini.
Alisema kuwa changamoto hiyo ni ya mpito huku akizitaka hospitali nchini kukusanya mapato yao ambayo yatasaidia ununuzi wa dawa.
Habari hii imendaliwa na Eliud Ngondo (Songwe), Eliya Mbonea
(Arusha), Pendo Fundisha (Mbeya), Ramadhan Hassan (Dodoma), Susazan
Uhinga (Tanga), Amon Mtega (Ruvuma), Jonas Mushi na Veronica Romwald
(Dar es Salaam).
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment