SHIRIKA la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) limejipanga kufanya
mageuzi makubwa ya uwekezaji katika sekta ya viwanda utakaoinua viwango
vya ajira na kuboresha maisha ya wanachama.
Mikakati hiyo imelenga kuitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli wa
kuijenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama suluhisho la kuwakwamua
Watanzania kwa kuongeza ajira.
Hayo yalielezwa jana kwenye mkutano wa sita wa wadau wa NSSF uliofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Akifungua mkutano huo mjini hapa jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
alisema Serikali inataka kuleta maendeleo kwa kuhakikisha unakuwapo
uchumi wa kati wenye kujengwa na viwanda.
Waziri Mkuu alisema anafarijika kuona NSSF ikiwa imedhamiria kwenda
na mwelekeo huo kwa kupanua wigo wa uwekezaji na kuelekea katika viwanda
hatua itakayoongeza ajira na kukuza uzalishaji nchini.
“Uamuzi huu utawawezesha NSSF na mifuko mingine kupata wanachama
wapya na kukusanya michango zaidi na kuiwekeza kutimiza lengo la
msingi la hifadhi ya jamii.
“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana kukabiliana na
tatizo la sukari nchini kwa kuamua kujenga kiwanda cha sukari eneo la
Mkulazi mkoani Morogoro kitakachotoa tani 200,000 kwa mwaka.
“Lakini, pia kiwanda hicho kitatoa ajira zaidi ya 100,000 kwa
Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mifuko hiyo. Huu ni moyo
wa uzalendo unaofaa kuigwa na kila mtu, taasisi na kampuni mbalimbali,”
alisema na kuongeza:
“Kazi ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kufanywa kwa namna mbili,
kwanza ni kwa kuvifufua vilivyopo na pili ni kwa kuanzisha viwanda vipya
na kwa NSSF wao wameweza kutekeleza yote mawili.
“Mbali na ujenzi wa kiwanda hicho cha sukari, NSSF pia imeanza kazi
ya uwekezaji wa kutoa mikopo kwa viwanda nchini kwa dhamira hiyo hiyo ya
kuijenga Tanzania yenye viwanda.
“Nimeelezwa hapa kwamba NSSF imetoa mkopo wa Sh bilioni 3.1 za kukuza
uzalishaji wa viuatilifu katika kiwanda kilichopo Kibaha, lengo likiwa
ni kuongeza uzalishaji.
“Natoa rai kwa taasisi zilizonufaika au zitakazonufaika na mikopo hii
kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na pia kurejesha kwa wakati kwa
mujibu wa mikataba wengine nao wanufaike,”
Kuhusu suala la baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati na
kusababisha usumbufu kwa wanachama, Majaliwa alisema suala hilo
halikubaliki hivyo aliwataka waajiri wote nchini kuheshimu sheria na
kuwasilisha michango hiyo kwa wakati.
Kwa waajiri wanaodaiwa na NSSF, alimuagiza mkurugenzi mkuu
kuwaandikia barua za kutaka wawasilishe fedha wanazodaiwa mara moja na
wale ambao hawatalipa ndani ya muda watakaopangiwa, wafikishwe
mahakamani.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliwajulisha wadau wa NSSF kuwa
Serikali imelipa Sh bilioni 722.7 kati ya madeni ya michango ya Sh
bilioni 964.2.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Professa Godius Kahyarara, alisema NSSF
imejipanga kuona viwanda vya ndani vikizalisha bidhaa za matumizi ya
ndani na kuziuza katika soko la nje kupata fedha za kigeni.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment