SIMBA jana ilizidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada
ya kuifunga Mbao FC bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Uhuru Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 26 katika mechi 10
ilizocheza, ikiongoza kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Stand United
iliyo nafasi ya pili na pointi 20.
Hata hivyo Simba ililazimika kupata bao hilo ‘jioni’ mwa mchezo huo
kwani Mbao waliwabana kuanzia mwanzo wa mchezo na kama washambuliaji
wake wangekuwa makini, wangevunja mwiko kwa kuwafunga vinara hao. Jana
hakuwa Shizza Kichuya tena wala Ibrahim Ajib waliozoeleka kuipa Simba
mabao, bali kazi hiyo ilifanywa na Mzamiru Yassin katika dakika ya 88.
Mzamiru alifunga bao hilo baada ya kuunganisha pasi ya Fredrick
Blagnon na kuzusha shangwe kwa mashabiki wa Simba ambao walionekana
walikwishakata tamaa ya kupata pointi zote tatu. Kwa ujumla Mbao
iliisumbua Simba katika mechi hiyo ikionekana kuwashambulia huku ikiwa
imekamilika kila idara.
Dakika ya 17 ya mchezo huo Simba ilikosa mabao kupitia kwa
washambuliaji wake Laudit Mavugo, Kichuya na Ajib ambao mabeki wa Mbao
walihakikisha hawachezi nao mbali ili wasilete madhara langoni mwao.
Mzamiru nusura aiandikie Simba bao katika dakika ya 21 lakini mpira
aliopiga ulipaa juu ya goli. Dakika moja baadaye Hussein Swedi wa Mbao
akatengeneza nafasi ya kwanza ya bao lakini akashindwa kujiamini na
mabeki wa Simba wakaunasa mpira na kuuondoa kwenye eneo la hatari.
Kwa matokeo hayo, Mbao inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza imebaki
katika nafasi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi 12 katika mechi 11
ilizocheza.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment