MOJA ya dosari kubwa zinazotishia amani,utulivu na mshikamano wa
Watanzania ni pamoja na migogoro na mapigano kati ya wafugaji na
wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
Mambo hayo mawili huishia kusababisha vifo vya binadamu na mifugo
lakini pia uharibifu wa mali mbalimbali yakiwemo mazao na uchomaji
nyumba.
Akizungumza na wananchi eneo la Masamvu, mkoani Morogoro akiwa njiani
kuelekea Dodoma mwishoni mwa wiki, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
alitamka wazi kwamba serikali haipendi kuona mauaji ya wakulima na
wafugaji yakiendelea kutokea nchini na hasa katika mkoa wa Morogoro.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo aliwakumbusha wafugaji kutii
sheria namba 12 ya mwaka 2010 iliyotungwa na Bunge kwa mifugo yao
kutambuliwa na kupigwa chapa kwa mujibu wa sheria.
Lengo la sheria hiyo pamoja na mambo mengine ni kusaidia katika utatuzi wa migogoro pindi inapotokea.
Sisi tunaunga mkono mwito wa Makamu wa Rais Samia wa kuwataka
wafugaji na wakulima wapendane na kuheshimiana bila kusahau kwamba pale
panapotokea kutoelewana basi masuala yao yashughulikiwe kwa njia ya
busara bila kugombana kiasi cha kusababisha madhara makubwa kama vifo na
uharibifu wa mali.
Hapa tungependa kutoa msisitizo maalumu kwa viongozi wetu wa serikali
katika ngazi za vijiji,vitongoji,kata, wilaya na halmashauri kuchukua
majukumu yao katika uhalisia na stahiki zinazotakiwa bila kupendelea
upande wowote ili kudhibiti migogoro hiyo kama siyo kuimaliza kabisa.
Kwa wafugaji na wakulima pia kwa upande wao nao wawe tayari kwa
makusudi kushirikiana na viongozi hao wa serikali na siasa ili
kukabiliana na changamoto hiyo katika uhalisia wake badala ya kutumia
mbinu ambazo kwa muda mrefu sasa hakuna aliyeibuka mshindi nje ya
kuendelea kuathirika kwa kupoteza wapendwa wetu na mali zetu.
Serikali ya Awamu ya Tano ina lengo kulifikisha taifa letu katika
uchumi wa kati ikiwa ni pamoja na kukuza na kujenga viwanda zaidi ili
watu wetu waweze kujipatia ajira na bidhaa kwa lengo la kujiletea
maendeleo endelevu katika nyanja zote za kiuchumi,kisiasa,kijamii na
kiutamaduni.
Hakuna ubishi kwamba malengo hayo muhimu katika sekta hizo mbili za
kilimo na mifugo hayataweza kufikiwa na kutuletea tija na matunda
tunayokusudia kama hakutakuwepo amani, utulivu na mshikamano. Hapa
tungependa kuwakumbusha wenzetu wakulima na wafugaji wawe na dhamira ya
dhati ya kudhibiti kama sio kumaliza kabisha migogoro baina yao.
Pande zote mbili, tunarudia kuwakumbusha kwamba waketi pamoja kwa
kushirikiana na viongozi wao ili kuweka mikakati ya uhakika ya
kulikabili tatizo hilo ambalo ni kero kwa pande zote mbili na uwezo wa
kulidhibiti limo katika mikono yao kwa kufanya majadiliano hadi kufikia
muafaka kuondoa tofauti zao ili kujiletea maendeleo endelevu.
Wakumbuke kwamba penye vurugu, mapigano na migogoro hapana maendeleo.
Tulikatae hili kwa vitendo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment