Image
Image

Rais Magufuli aongoza waombolezaji kuaga Mwili wa Masaburi jijini Dar es Salaam.

RAIS John Magufuli akiwa miongoni mwa watu walioshiriki kuuaga mwili wa Dk. Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam (2010-2015), amezua jambo.
Akishiriki kuaga mwili huo leo asubuhi katika Viwanja vya Karimjee, Rais Magufuli amesema ingawa wasifu wa marehemu umemtaja Janeth Masaburi pekee kama mke lakini yeye anawafahamu wake wengi wa marehemu.
“Katika wasifiu ametajwa mke wa marehemu mmoja lakini mimi nawafahamu wake wa marehemu wengi sana. Na katika tabia zetu za kiafrika hilo suala la wake wengi ni kawaida tu. Hata vitabu vitakatifu vinasema Mtume Suleiman alikuwa na wake zaidi ya elfu moja.
“Nilikuwa naongea pale na Mheshimiwa Kikwete nikasema na sisi tungefurahi sana kama tungekuwa na wake wengi kama hawa,” amesema na kusababisha vicheko na miguno kutoka kwa waombolezaji.
Rais Magufuli ameeleza kuwa, historia ya Masaburi haiwezi kufutika katika Jiji la Dar es Salaam ushahidi wa hili ni watu wengi waliojitokeza katika msiba wake.
“Tunazungumza hapa kuwa watoto wa marehemu ni 20 lakini wanaweza kuwa hata zaidi ya 20.
“Niwaombe sana nyie watoto msifarakane, mshikamane na mtoto wa kwanza akawe kiongozi wa familia, palipo na umoja Mungu atawatangulia, sisi sote tu njia moja na kila mmoja ataionja mauti na si mimi, Kikwete wala Lowassa atakeyekwepa mauti,” amesisitiza.
Baada ya mwili huo kuagwa Karimjee, msafara wa waombolezaji umeelekea eneo la Chanika kwa ajili ya mazishi.
Viongozi mbalimbali walijitokeza kuuaga mwili huo pamoja na wananchi mbali na Rais Magufuli ni Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu; Rais Mstaafu Kikwete; Spika Mstaafu, Anne Makinda na Gharib Bilal, Makamu Mstaafu wa rais.
Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam; Charles Kuyeko, Meya wa Manispaa ya Ilala; Abdallah Bulembo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM; mawaziri, wabunge mbalimbali pamoja na Wakuu wa Wilaya za Dar.
Ramadhani Madabida, Mwenyekiti wa CCM amesema kifo cha Masaburi ni pigo si tu kwa familia yake bali pia Chama Cha Mapinduzi.
Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo pia alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliojitokeza kuuaga mwili wa Masaburi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana Masaburi alichuana vikali na Kubenea katika kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Ubungo ambapo (Masaburi) alishindwa alishindwa kwa tofauti ya kura 28,000.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment