KATIKA gazeti letu la jana, Mwinjilisti Jacob Foda wa kanisa la
Waadventista Wasabato alikaririwa akisema ni jambo la kusikitisha sana
kuona binadamu anatoa hukumu kwa mwenzake bila ya kumsikiliza.
Alisema hayo akizungumzia tukio la mauaji ya watafiti wawili na
dereva katika kijiji cha Iringa Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Mwinjilisti huyo ni sehemu ya kielelezo cha watu wenye ustaarabu,
wanaofuata maadili na wenye kuheshimu uhai ambao wamekuwa hawaelewi kwa
nini binadamu anaweza kutoa agizo la kuuawa kwa binadamu mwingine pamoja
na kwamba amejieleza yeye ni nani na yupo hapo kwa sababu gani.
Aidha, maneno ya mwinjilisti huyo ni kielelezo cha ‘uungu’ wa
binadamu katika sura sahihi ya Mungu mwenye upendo na anayejali maisha.
Pamoja na mwinjilisti huyo kutuonesha nini maana ya upendo na
ufuataji wa ubinadamu, watunza sheria nao wamesema wazi kuwa kitendo
hicho cha mauaji hayo hakikubaliki kwa namna yoyote ile na hata kwa
sababu yoyote ile.
Kiukweli hapakuwapo na haja ya wananchi hawa kuwaua watu wale, kwani
tayari walijisalimisha na walitaka wapelekwe kituo cha polisi kama
walikuwa na shaka nao, lakini wananchi hao walihakikisha kwa jeuri
waliyopewa na wakubwa wao wa imani wanatekeleza azma yao.
Huwezi kuacha kuamini kwamba hiyo ni jeuri ya kutoka kwa wakubwa kwa
kuwa watu hawakutaka hata kutii hata risasi zilizopigwa na polisi
walipofanya juhudi za kuwaokoa watafiti hao.
Tunaamini kwamba mauaji hayo yasingelikuwepo kama kusingelitokea watu
wanaohimiza wenzao kufanya uhalifu kwa kuchukua hatua mikononi na hapa
ndipo tuna kila sababu ya kulitaka jeshi la polisi kukamata na
kuwafungulia mashtaka wanaohusika wote.
Na hii tunaona lazima ianze kwa mchungaji wa kanisa la Christian
Family ambaye kwa makusudi akiwa na dhamira potofu kabisa, aliwatangazia
watu wakafanye kosa la mauaji kwa kauli zake. Tulitarajia watu wa Mungu
hawa kuwa na subira na roho za watu kwa kuwashawishi watu wao kutenda
mema na kufuata sheria, lakini si jinsi alivyopiga unyende uliosababisha
mauaji ya kutisha.
Iwe watu hawa wamekurupuka, au wamefanya wakiwa wanajua wanafanya
nini, tunalishauri Jeshi la Polisi kuwapambanua watu hawa, hata kama
wamekimbilia porini kuwakamata ili wakaonje sheria; ili pamoja na wao
kujutia kila mmoja atakayefikiria kurudia kitendo hicho aone ‘moto’ wa
sheria unavyounguza.
Pamoja na kumuomba Mungu awalaze pema peponi waja wake, Nicas
Magazine aliyekuwa dereva pamoja na watafiti wawili, Teddy Lumanga na
Jafari Mafuru, tunawataka wananchi kutambua kwamba hakuna sifa katika
kutoa uhai wa mtu na wanaofanya kitendo hicho sheria itaona fahari
wakikamatwa na kufikishwa kwake, hasa inapoonekana dhahiri kwamba
kitendo hicho wamekifanya kwa makusudi kwa lengo lenye hila ovu dhidi ya
ubinadamu.
Tunasema hata kama watakimbia mwaka mzima, watu hawa lazima wasakwe
na wapelekwe mbele ya sheria kujibu hoja za mauaji, tena ya kukusudia
huku wakiondoa nguvu kazi kubwa yenye kuwezesha maendeleo kwa kuwapa
wananchi taarifa sahihi baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu namna ya
kusonga mbele katika shughuli zao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment