Image
Image

Yanga na Azam kufa kiume leo.

BAADA ya Yanga na Azam kupata sare tasa mchezo uliopita. Leo zina kazi nyingine ngumu ya kutafuta pointi tatu katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania bara itakayochezwa viwanja tofauti. Yanga itakaribishwa na Toto Africans kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Azam FC itakuwa na mchezo mgumu utakaochezwa kuanzia saa moja jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Timu zote hazina matokeo mazuri yaliyopita, kila mmoja ni lazima itacheza mchezo wa kumaliza hasira ilimradi kupata pointi ambazo zitawasogeza karibu na kinara wa ligi, Simba inayoongoza kileleni mwa msimamo kwa pointi 23.
Bila shaka kupona kwa mshambuliaji Amis Tambwe aliyekuwa majeruhi na kurudi kwa kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima aliyekuwa na matatizo ya kifamilia, huenda kukaendelea kuleta matumaini mapya ya kupata ushindi katika mchezo huo.
Wachezaji watakaokosekana katika mechi ya leo ni Juma Abdul aliyeumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam FC, Malimi Busungu aliyedaiwa kuwa ana matatizo ya kifamilia wakati Ali Mustafa anauguza jeraha.
Yanga na Toto ni timu ambazo zimekuwa zikihusishwa kuwa na uhusiano wa karibu na hasa kwa vile viongozi wa Toto kudaiwa kuwa na mapenzi na timu hiyo ya Jangwani. Mechi ya msimu uliopita baadhi yao walijiweka pembeni mpaka baada ya mechi hiyo wakidai kuwa Yanga damu, hali iliyosababisha baadhi yao kusimamishwa uanachama.
Lakini mchezo wao hautakuwa rahisi kwa kila mmoja, hasa kwa Toto Africans ambayo imetoka kufungwa na Majimaji mabao 2-1. Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo, ikiwa na pointi 15, kukiwa na tofauti ya pointi nane dhidi ya vinara wa ligi hiyo Simba hivyo, kwa vyovyote wanahitaji ushindi kama kweli wanataka kuwa katika mbio za kutetea taji lao.
Toto, msimu huu umekuwa mbaya kwao, baada ya kucheza michezo 10, ikishika nafasi ya pili kutoka mwisho kwa pointi nane, baada ya kushinda michezo miwili, sare mbili na kupoteza sita. Mechi nyingine itakayochezwa leo ni Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar.
Timu hiyo ya Chamazi imetoka kufanya vibaya katika michezo mitatu iliyopita, ikilazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Yanga, ikifungwa na Stand United bao 1-0 na sare dhidi ya Ruvu Shooting 2-2. Bila shaka kutokana na kiwango bora katika mechi yao iliyopita, huenda wakaendeleza mapambano na kuhakikisha wanashinda.
Azam FC inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 12 katika michezo tisa. Inakutana na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15 katika michezo 10. Hautakuwa mchezo rahisi kwa kila mmoja, kutokana na ubora wa kila timu. Ruvu Shooting inaikaribisha Mwadui kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Maafande hao hawako vibaya sana wanashika nafasi ya sita wakiwa na pointi 13 katika michezo tisa waliyocheza. Mwadui inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho kwa pointi tisa baada ya kushinda michezo miwili kati ya tisa, mitatu ikitoka sare na kupoteza minne. Pia, Ndanda inaikaribisha Mbeya City kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Timu hii mara nyingi huwa haikubali kufungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, iko radhi ishinde au kutoka sare, Mbeya City itakuwa na kazi nzito. Timu zote zimecheza michezo 10, zikivuna jumla ya pointi 12 kila mmoja, City ikishika nafasi ya tisa na Ndanda ya 10 kwenye msimamo.
Stand United inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ikikimbizana na Simba, kwa tofauti ya pointi tatu, wao wakiwa na pointi 20. Leo itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya kumenyana na Prisons inayoshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 1. Mechi ya wawili hawa huwa haitabiriki na leo kila mmoja anahitaji matokeo.
African Lyon itakuwa mwenyeji wa Majimaji. Licha ya Majimaji kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Toto bado inaendelea kushika mkia ikiwa na pointi sita. Bila shaka kama inataka kujikomboa ni lazima ipambane kujiokoa ilipo kwa kushinda mechi zake. Lyon inahitaji kushinda bado ipo na pointi 10 katika nafasi ya 12.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment