Image
Image

Mikopo bilioni 80/- elimu ya juu yatua vyuoni

SERIKALI imetoa Sh bilioni 80 kwa ajili ya malipo ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaoanza na wanaoendelea na masomo na wameanza kulipwa jana. Aidha, imewataka wakuu wa vyuo ambao hawajawasilisha matokeo ya wanafunzi wao wanaoendelea na masomo kufanya hivyo haraka ili wakamilishe uchakataji wa mgawo wa mikopo. Katika mwaka huu wa fedha, serikali imetenga Sh bilioni 427 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akielezea mchakato wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kueleza kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya wanaoanza na wanaoendelea katika robo mwaka.
Manyanya alisema serikali imetoa fedha zinazotakiwa kukamilisha mchakato wa malipo unaofanyika kuanzia jana baada ya kumalizika kwa uchambuzi kulingana na vigezo.
Alisema kwa mujibu wa ulipaji mikopo, inazingatiwa vigezo vya kisheria vya kutoa mikopo kulingana na uhitaji kwa kuangalia anayepewa, kweli ana uhitaji na siyo kwa kila mtu kwani lengo la serikali kusaidia na siyo kuondoa majukumu ya mzazi.
Alisema pia wanaangalia bajeti iliyopo kwa wakati huo, kwani kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 na matamko ya Rais John Magufuli amedhamiria kuendelea kutoa mikopo kwa wahitaji wote pamoja na kuboresha elimu kwa namna mbalimbali.
Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa sambamba na kutoa mikopo ni ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Mloganzila kwa Sh bilioni 100 pamoja na kukamilisha ukarabati wa vyuo vya ualimu ambapo tayari vyuo 10 vimekamilika.
Alisema pia baada ya Rais kutembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuona adha ya wanafunzi kukabiliwa na kukaa mbali na chuo, Sh bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 20 katika ghorofa tatu zitakazochukua wanafunzi 3,800.
Manyanya alisema pia serikali imelipia ada moja kwa moja vyuoni kwa wanufaika wa mikopo ya Sh bilioni 40 katika vyuo vya serikali na binafsi nchini.
Aliwataka wanafunzi wanaolalamika kutopata mikopo kukamilisha kupeleka viambatanisho vyote stahili huku wakihakikisha wanakuwa na vigezo vya ufaulu kwani sasa ufaulu umepanda wengi wamepata daraja la kwanza na pili, hivyo kuchukua hao kwanza na wale wa daraja la tatu wachache.
Naibu Waziri alisema kwa yatima wapo wasiopewa mikopo baada ya uchambuzi kubaini kuwa na uwezo wa kujilipia kutoka kwa ndugu au mali zilizoachwa na wazazi hivyo kuna utofauti wa yatima, kwani wapo wahitaji na wasio wahitaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdul Razaq Badru alisema bodi hiyo hutoa mikopo kwa kuzingatia kozi za vipaumbele kama udaktari au uhandisi kwa ajili ya ujenzi wa wataalamu katika Tanzania ya viwanda.
Alisema pia mikopo hutolewa kwa ulinganifu wa uhitaji kwa asilimia huku wakifanya uchambuzi wa kina ili kuwafikia wahitaji wengi na wanufaika kuongezeka kama anavyotaka rais.
Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso) imesema kuwa muongozo mpya wa utoaji mikopo uliotolewa kwa mwaka huu wa masomo 2016/17 utawahusu wadahiliwa wapya tu wanaoanza masomo.
Taarifa iliyotolewa jana na Tahliso kwenda kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu, ilieleza kuwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ambao wanaendelea na masomo, wao wataendelea na utaratibu kama ulivyokuwa tangu awali walivyoingia makubaliano na utaratibu mpya hautawaathiri.
Mwenyekiti wa Tahliso, Stanslaus Kadugalize ambaye amesaini taarifa hiyo, alifafanua kuwa msimamo huo umetolewa baada ya jumuiya hiyo kuingilia kati baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kutoa mwongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Kadugalize alisema baada ya kutolewa kwa mwongozo huo walienda kufanya majadiliano na Waziri, Profesa Joyce Ndalichako ili kumwomba wabadili msimamo wa mwongozo huo kwa kuwa utawaathiri wanafunzi wengi ambao ni watoto wa maskini.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia walitangaza vigezo vya utoaji mikopo kuwa kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo wapya na wanaoendelea na masomo watakopeshwa kulingana na uwezo wao (means tested) katika vipengele vyote vya mikopo.
Tahliso ilieleza kuwa kutokana na maelezo hayo ni dhahiri mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea hasa kwa wale wenye wazazi bila kujali ana uwezo ama hana uwezo, mikopo yao ingepungua kutoka kwenye asilimia walizopangiwa awali.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa muongozo huo ungepelekea fedha inayotolewa kwa ajili ya chakula na malazi kupungua, jambo ambalo lingesababisha wanafunzi wengi kushindwa kuendelea na masomo, kutokana na uwezo wa wafamilia wanazotoka hasa watoto wa maskini ambao hutegemea fedha hizo hizo za boom kulipia sehemu ya ada iliyobakia na huku wakiendelea kuishi maisha ya shida vyuoni.
Katika vigezo hivyo, Serikali ilisema itatoa kipaumbele kwanza kwa wanafunzi wanaoenda kusomea fani za Sayansi za Tiba na Afya, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi na wale watakaosomea Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.
Kwenye vigezo hivyo pia serikali ilisisitiza kuwa kipaumbele kingine kitakuwa ni kwa waombaji hususani wenye mahitaji maalumu kama vile ulemavu na yatima.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment