KAMPUNI ya Songoro Marine Transport Boatyard imeihakikishia Serikali
kuwa meli mpya mbili za mizigo zinazoendelea kujengwa katika Bandari ya
Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya zitakuwa zimekamilika ifikapo
mwishoni mwa mwezi huu.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Salehe Songoro amesema ifikapo Oktoba 30,
mwaka huu kampuni hiyo itaziingiza meli hizo mbili za mizigo ndani ya
ziwa Nyasa tayari kwa safari za majaribio.
Alitoa uhakika huo juzi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla
kufanya ziara ya kushitukiza bandarini Itungi akilenga kufuatilia ujenzi
huo wa meli mpya.
Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa ujenzi wa meli mbili za mizigo
umefikia zaidi ya asilimia 80, hivyo kazi zilizosalia ni za umaliziaji
ikiwemo upakaji rangi na tayari meli hizo zimepewa majina ya Mv Ruvuma
na Mv Njombe.
Alisema meli ya abiria ambayo ujenzi wake utakamilika Februari
mwakani itapewa jina la Mv Mbeya II kwa kuwa jina la Mv Mbeya liliwahi
kutumika miaka ya nyuma katika meli iliyozama ndani ya Ziwa Nyasa miaka
mingi iliyopita.
“Mv Mbeya II tayari ujenzi umeanza kwa vipande vipande lakini
tunataraji baada ya hizi meli mbili za mizigo kuingizwa ziwani ndipo
tutapata nafasi ya kutosha kwaajili ya kuanza ujenzi mkubwa wa meli hiyo
ya abiria itakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria miambili na tani
miambili za mizigo kwa wakati mmoja,” alisema Songoro.
Akitoa tathmini yake baada ya ziara hiyo, Makalla alisema
ameridhishwa na hatua za ujenzi huo na kuwa ana imani kuwa ahadi ya
kuziingiza ziwani meli mbili za mizigo mwishoni mwa mwezi huu
itatimizwa.
"Nimejionea kila kitu tayari kimefungwa. Injini, vyumba vya kuongozea
vyote viko tayari. Kazi zilizosalia ni kidogo ambazo kama kasi
itaendelea hivi ifikapo mwisho wa mwezi huu zitakuwa zimekwisha na mimi
nitakuja kushiriki siku ya majaribio,” alisema Makalla.
Alisema tayari wadau mbalimbali wa kibiashara wameanza kuonesha nia ya kutumia usafiri huo mara tu utakapoanza kutoa huduma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment