SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imeanza kuchukuwa hatua
kurudisha huduma za usafirishaji wa abiria katika bandari ya Wete, Pemba
na kutumia Sh milioni 200 kwa ajili ya kufanya ukarabati katika hatua
ya awali.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji,
Mohamed Ahmada alisema hayo wakati akijibu swali la mwakilishi wa Gando,
Mariamu Thani aliyetaka kujua mipango ya kuifanyia ukarabati bandari ya
Wete imefikia hatua gani hadi sasa.
Akifafanua Ahmada alisema, lengo
la Serikali ni kuona bandari hiyo inafanya kazi zake kama ilivyokuwa
zamani na kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaoishi mkoa wa Kaskazini
Pemba wenye idadi kubwa ya watu.
Alisema juhudi zimechukuliwa ikiwamo
ya kuzungumza na wahisani mbali mbali kufanya ukarabati bandari hiyo
kwa kuongeza kina cha maji kwa ajili ya kuziwezesha meli kufunga gati
hapo bila ya matatizo.
Hata hivyo, Ahmada hakuitaja kampuni gani au
mfadhili yupi anayeifanyia ukarabati bandari hiyo, ambayo kwa sasa
haitumiki kwa ajili ya kufunga gati meli zinazotoa huduma katika kisiwa
hicho.
Huduma za usafiri wa abiria katika bandari ya Wete zimekwama
kwa muda mrefu ambapo kwa sasa huduma za meli zipo katika bandari ya
Mkoani Pemba.
Kitendo cha kuwa na huduma duni za usafiri wa abiria
katika bandari ya Wete, kinalalamikiwa na wananchi wa mkoa wa Kaskazini
Pemba ambapo abiria wanaokwenda huko hulazimika kushuka bandari ya
Mkoani na kuanza safari kwenda katika mkoa wa Kaskazini Pemba.
Bandari
hiyo kwa sasa inatoa huduma za majahazi yanayoleta bidhaa mbali mbali
kutoka katika mikoa ya Tanzania Bara ikiwamo Tanga.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment