Samuel
John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 huko wilayani Urambo Mkoa wa
Tabora. Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 – 1953,
kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957 na kuendelea na
masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle School”.
Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana
Tabora yaani “Tabora Boys” kidato cha I – IV na cha V – VI.
Mara
tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta alijiunga Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria (L LB) mwaka 1964 na
kuhitimu mwaka 1971.
Sitta
amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu mwaka 1966, wakati yuko
mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi UDSM, wanafunzi waligoma na
kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa
mishahara yao baada ya JKT. Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa,
kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono
na marupurupu makubwa?
Baada
ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu Julius Nyerere alikubali
kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya
mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. Miezi miwili baadaye akatangaza
Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi
hao.
Watukutu
wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo (Wote sasa marehemu) na wengine
kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile walichokiita haki zao, (haki
za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu Mwalimu Nyerere kwa maneno
makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu”.
Mwalimu
Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa kile
alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao”. Miezi kumi baadaye,
baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia akaamua kuwarudisha
chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo; Sitta na wenzake 7 walitiliwa
ngumu, hawakurejeshwa chuoni.
Busara
za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu aliliwe zaidi na kuandikiwa barua
mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na. C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13
ya 9/07/1967. Mwalimu alikubali kilio hicho na kuwaruhusu vijana hao
wanane warudi kwa sharti kwamba wale watukutu wawili (Sitta na
Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu Nyerere” mwenyewe. Hii ndiyo
ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM na kuendelea na masomo kwa
miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971.
Wakati
Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya
“CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975
aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa
Utawala.
Baadaye
mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya
Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu
Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976.
Chini
ya mfumo wa chama kimoja, Sitta alikuwa kiongozi wa juu wa CCM na
serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na Waziri katika nyakati tofauti na
ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo wa vyama vingi.
Sitta alimuoa Margareth Simwanza Sitta
Mbio za ubunge
Enzi
za chama kimoja 1975 - 1995 Sitta alikuwa mbunge wa Jimbo la Urambo
(kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia
alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi
cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.
Mwaka
1995 Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na
kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR.
Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda kwa
kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta.
Sitta
alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu na
aliwashinda wapinzani wake wakuu Lumatiliza Yotamu Lubungila wa NCCR na
Wilson George Ntakamulenga wa CUF. Sitta alipata kura 28,660 (72.3%) na
kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki. Kurudi kwa nguvu
kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge
la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa aliloliita bunge la Viwango Na
Kasi "Speed and Standards" kwa mafanikio na changamoto nyingi.
Mwaka
2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda
wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (CHADEMA) na Zombwe
Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 (70.47%). Baada ya ushindi
huo, Sitta alijaribu tena kuwania uspika bila mafanikio; utendaji wake
wa kuiuma serikali na wakati mwingine kuipuliza kwenye Bunge la Tisa
ulimfanya achukiwe na serikali.
Ilipoonekana
ana nguvu akatengenezewa “chui wa karatasi” (mshindani), Andrew Chenge.
Chenge naye akachukua fomu ya uspika ghafla, likatengenezwa ‘zengwe’
kuwa wagombea wote wana nguvu, hapo CCM ikapata mwanya wa kutamka kuwa
haiwataki wote ili kuondoa mvutano. Sitta akapoteza ndoto za uspika na
ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda.
Rais
Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010 alimpa Sitta
Wizara ya Afrika Mashariki kama Waziri,vilevile alihamishiwa Wizara ya
Mawasiliano na Uchukuzi.
Mbio za urais
Samuel
John Sitta alianza mbio za urais “kimyakimya” tangu alipokuwa Spika wa
Bunge la Tisa (2005 – 2010). Kuna nyakati alikuwa akitoa kauli
zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti huku
akionyesha kuwa nchi ina viongozi thabiti na hawajapewa uongozi mkuu wa
nchi, akiwemo yeye.
Hata
alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka 2014, mara nyingi Sitta alionekana
kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na alipohojiwa, mara kwa mara, juu
ya urais alionyesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa, alilalamika kuwa wala
rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi.
Katika
Uchaguzi wa 2015, Sitta alitangaza nia ya kuwania Urais na alichukua
fomu ya kugombea urais kupita chama cha Mapinduzi ambapo baada ya
uchaguzi wa ndani chama, John Magufuli ndo jina lililofanikiwa kupenya
na kuteuliwa na chama kugombea Urais wa Tanzania.
Mungu Ailaze Roho Ya Marehemu Mahali Pema Peponi Amen.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment