KATIKA kuendelea kujenga dhana ya kubana matumizi ya fedha za
serikali, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesafiri kwa ndege ya
abiria ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda
Mwanza na kuokoa zaidi ya Sh milioni 33.
Kabla ya kuanza safari hiyo jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais
akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwa kupanda ndege hiyo
ameokoa fedha za serikali na kodi za wananchi.
Alisema ameona ashirikiane na Watanzania kuonesha uzalendo kwa
kutumia huduma ambazo zinatolewa na serikali na kuwataka Watanzania wote
kutumia ndege hizo.
“Ningepanda ndege ya kukodi ningetumia shilingi milioni 40 kwa safari
hii, lakini nikaona hapana nikaamua mimi pamoja na msafara wangu
tutumie ndege hii ya Shirika la Ndege Tanzania ambapo tumetumia Shilingi
milioni 7.6 pekee,” alisema Makamu wa Rais aliyeambatana na watu 16
katika safari hiyo.
Makamu wa Rais ambaye alipanda ndege hiyo pamoja na abiria wengine wa
kawaida, aliwataka viongozi wengine pia kufuata mfano huo kusafiri kwa
kutumia ndege za shirika hilo.
Alisema ameona kwenye televisheni watu wakitoa maoni yao juu ya
kampuni hiyo ya ndege kuwa ni nzuri kwa sasa na yeye akaamua kusafiri na
ndege hiyo.
“Niliona kwenye televisheni watu wakitoa maoni mazuri tu juu ya
shirika hili na mimi nikaona nitumie nafasi hiyo,” alifafanua Makamu wa
Rais.
Hivi karibuni, serikali imenunua ndege mbili aina ya Bombardier Q400
na kuzikabidhiwa kwa ATCL na zimeanza kufanya kazi katika mikoa
mbalimbali nchini huku zikiwa na gharama nafuu, lakini pia zikiwa na
gharama nafuu ya uendeshaji.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
ambaye alikuwepo uwanjani akimsindikiza Makamu wa Rais, alisema
Watanzania waelewe kwa sasa kampuni hiyo iko kwa ajili ya kufanya
biashara.
Alimpongeza Makamu wa Rais kwa kuonesha ushirikiano mkubwa na pia
uzalendo kwa kusafiri na ndege ya ATCL, kwani angeweza kutumia ndege
nyingine yoyote.
“Leo hii kwa kutumia ndege ya Tanzania yeye pamoja na wasaidizi wake
ni jambo jema sana alilolifanya na pia ni jambo la kizalendo
tunampongeza sana, kwani angeweza kutumia ndege nyingine yoyote
anayoitaka,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ndege za ATCL gharama zake ni nafuu na pia huduma zao
zimeboreshwa zaidi, na kwamba ifikapo mwaka 2018 serikali itanunua ndege
nyingine moja na pia mwaka 2019 inatarajia kununua ndege nyingine.
Profesa Mbarawa alitembelea pia karakana iliyopo katika uwanja huo wa
ndege na baadaye alitembelea chuo cha mafunzo kwa wafanyakazi wa ndani
ya ndege ambako alizungumza na wanafunzi waliokuwepo.
Aliwataka kufanya kazi kwa bidii kwani serikali inajenga ATCL mpya ambayo inatoa huduma bora kwa wateja wake.
“Mmekuja hapa mnaijua ATCL? Hapa tunataka watu wanaotoa huduma nzuri,
ile culture (utamaduni) iliyokuwepo nyuma kama mmekuja nayo mjue mlango
uko wazi hautachukua miezi sita mtaondoka. Mkifanya kazi hapa mfanye
kwa bidii, mkahudumie watu kwa ukarimu kwa sababu tunataka kujenga ATCL
mpya ambayo inaongoza ndege zote na hatutamvumilia mtu ambaye
anaturudisha nyuma,” alieleza Profesa Mbarawa.
Aliwataka wafanyakazi hao wa ACTL kuachana na mfumo uliopita badala yake kufanya kazi kwa bidii kuijenga ATCL mpya.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema kampuni hiyo
inaboresha huduma zake ambako kwa sasa wanaboresha huduma za mtandaoni
kwa ajili ya watu kushika nafasi ya safari na hata kulipia kupitia
mitandao ya simu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment