SERIKALI ya Shirikisho la Ujerumani na watu wa Ujerumani wametoa
msaada wa fedha Euro milioni 11 sawa na Sh bilioni 26.4 kwa ajili ya
kusaidia uendeshaji wa shughuli za wakimbizi nchini.
Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke alisema fedha hizo
zitasimamiwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa
(UNHCR) pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Balozi Kochanke alisema UNHCR watatumia fedha hizo kwa ajili ya kutoa
huduma mbalimbali ambazo zinahitajika kwa wakimbizi waliopo nchini na
baadhi ya fedha zitatumika kusaidia mahitaji ya chakula cha wakimbizi
hao.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),
Michael Danford alisema hali ya chakula kwa wakimbizi inategemea
wahisani kama Ujerumani, hivyo misaada hiyo itawawezesha kuishi na
kupata mahitaji ya chakula.
“Kama mnavyojua wakimbizi wanakuja wakiwa hawana kitu chochote,
wanaacha makazi yao hivyo wanahitaji msaada huo kwa kiasi kikubwa ili
waweze kuendelea kuishi,” alisema Danford.
Akishukuru kwa msaada huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi, Balozi Hasan Simba Yahya alisema wamekuwa wakiwakumbusha
kuzingatia hali za wananchi wanaopokea wakimbizi kwa sababu hali
zinakuwa si za kuridhisha na hivyo kufanya watoto kudumaa na hivyo
kuathiri watoto.
“Kama serikali tutaendelea kubeba jukumu la kuhudumia wakimbizi kadri
wanavyokuja kwa kuwa ni jukumu la kimataifa hivyo kubwa ni kuwakumbusha
wahisani wakihudumia wakimbizi wasiishie hapo bali wakumbuke na jamii
inayowapokea wakimbizi,” alisema Balozi Yahya.
Aliongeza, “wanaopokea wakimbizi watazamwe badala ya kuachwa kwa kuwa
wanaathirika na uharibifu wa mazingira kwenye maeneo yao na pia hali ni
mbaya ya usalama katika maeneo yao kutokana na kuja kwa wakimbizi wengi
kwa wakati mmoja.
“Mtu anakuja anaingia hana chochote na ana watoto wana njaa, hivyo
ataingia kwenye shamba lenye muhogo na hapo ndipo vurugu zinaanza, hivyo
ili hayo yote yasitokee nguvu zielekezwe kwa watu wanaopokea wakimbizi
katika maeneo hayo.”
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment