WAKATI dirisha dogo la usajili likifunguliwa leo, vigogo vya soka
nchini vya Yanga, Simba na Azam FC vimeanza mchakato wa kuwatafuta
wachezaji ili kuboresha vikosi vyao.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hiyo ni nafasi muhimu
ya kujiimarisha kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo kwa ajili ya duru la
pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga, Simba na Azam FC zinaonekana kuendelea kutazama kimataifa kwa
kutafuta wachezaji wa kigeni katika nafasi tofauti katika kuhakikisha
timu zao zinaendelea kutikisa ndani na nje ya nchi.
Wachezaji wanaotajwa hadi sasa kusajiliwa ni kiungo mkabaji Meshack
Chaila wa Zesco United ambaye huenda akaingia mkataba wa miaka miwili
ndani ya wiki hii.
Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga jana, Chaila ameshamalizana na timu hiyo na yuko tayari kujiunga nao wakati wowote.
Ujio wa mchezaji huyo huenda ukawatimua baadhi ya waliopo, ambapo
hadi sasa Yanga ina idadi ya wachezaji saba wa kigeni, isipokuwa bado
hawajawekwa hadharani ni akina nani watakaotemwa.
Mchezaji mwingine anayetajwa ni Kipre Tchetche ingawa tovuti ya Yanga
inasema mfuko wao usajili unasuasua, hivyo kuna uwezekano wa kumsubiri
Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji aliyeko Marekani ili kuokoa jahazi.
Wachezaji waliopo hadi sasa ni Mzambia Obrey Chirwa, Wazimbabwe
Donald Ngoma na Thaban Kamusoko, Mrwanda Haruna Niyonzima, Mrundi Mbuyu
Twite na Amis Tambwe na Mtogo Vicent Bossou.
Pia, kuna wachezaji wazawa kama Malimi Busungu ambaye kwa muda mrefu
amekuwa akikosa namba huenda akabaki au kupelekwa kwa mkopo katika timu
nyingine zilizoonesha nia ya kumhitaji ikiwemo Tanzania Prisons au
Majimaji.
Kwa upande wa Simba ilianza mchakato wa kutaka kumrejesha mchezaji
wao Emmanuel Okwi anayecheza soka la kulipwa Denmark. Mchezaji huyu
anadaiwa kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza huko aliko hivyo, huenda
akarejeshwa.
Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
alisema Okwi atarudi kwenye dirisha dogo. Tayari Simba ilianza kampeni
za kumrejesha Okwi kwa kusaka maoni ya wadau kwenye mitandao ya kijamii
kama ni sahihi kumrejesha mchezaji huyo wa Uganda.
Pia, licha ya Kipa wao namba moja Vicent Angban kuwapa mafanikio hadi
sasa, kumekuwa na maoni ya wadau kutoridhishwa na kiwango chake. Lakini
bado haijawekwa wazi kama ni miongoni mwa wachezaji watakaotemwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema
hivi karibuni kuwa kuna wachezaji watakaotemwa, lakini hakuwataja.
Tetesi zimewataja wachezaji wengine kama Shomari Kapombe na Kipre
Bolou kuwemo katika mpango wa kusajiliwa na timu hiyo. Wachezaji hao kwa
sasa wanatumikia Azam FC.
Simba ina wachezaji wa kigeni akiwemo Angban, Laudit Mavugo, Juuko
Murshid, Fredrick Blagnon, Method Mwanjale na Janvier Bokungu.
Na Azam FC inaonekana kutoridhishwa na wachezaji wake wa kigeni
waliokuwepo, kwani tayari imeanza majaribio kwa wengine waliomiminika
kusaka nafasi ya kucheza katika timu hiyo.
Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Ruvu juzi, kulikuwa na
wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo mabeki wa kati Nkot Mandeng
Eric (Coton Sport De Garoua, Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Asec
Mimosa, Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Coton Sport
Garoua, Cameroon).
Washambuliaji ni Yaya Anaba Joel (Coton Sport Garoua, Cameroon),
Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Bernard Ofori (Medeama, Ghana)
na Konan Oussou (Tala’ea El-Gaish SC, Misri).
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment