WASOMI, wadau
wa elimu na wananchi wa kawaida wamekosoa tamko la Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakisema kwamba
halijafanyiwa utafiti na halitekelezeki kisheria.
Mwishoni mwa
wiki, akiwa kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),
Profesa Ndalichako alisema kuanzia mwakani mwanafunzi yeyote hatajiunga
na masomo ya Shahada bila kupitia kidato cha sita.
Alisema mfumo wa elimu huria umechangia kuzalisha wasomi butu kwa kupokea wanafunzi dhaifu kitaaluma.
Wakizungumzia
tamko hilo kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi
ya wasomi walisema kabla ya waziri kuanza kutoa amri na matamko,
alitakiwa kufanya utafiti kujiridhisha juu ya agizo lake hilo.
“Profesa
Ndalichako hajasema ametoa wapi ujasiri wa tamko lake, ni kwa utafiti
upi aliofanya yeye au hata kukasimu taasisi kwa niaba yake ili ifanye
utafiti na kuja na majibu kuwa kidato cha sita ndicho kiwango bora cha
kumpitisha mtu kusoma shahada ya kwanza?
“Binafsi naona haya ni
matamko ya kisiasa yasiyoweza kutekelezwa kisheria, arekebishe sheria
kwanza ndio aje kutoa tamko la kurekebisha mfumo wa elimu, vinginevyo
anaweza kuharibu kuliko waliomtangulia,” alisema mkuu wa chuo kikuu
maarufu mkoani Arusha ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Naye
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Tawi la Makumira, Mchungaji Profesa
Josef Parsalao, alisema pamoja na lengo zuri la kurekebisha mfumo wa
elimu, badala ya kuanza na amri na matamko, Serikali ilitakiwa
kurekebisha kasoro zilizopo hatua kwa hatua.
“Sijui yeye
Ndalichako alipitia hatua zipi za elimu, lakini upo ushahidi wa kuwapo
kwa wasomi wengi wakiwamo wale wanaofundisha vyuo mbalimbali nchini,
kupitia ngazi ya chini kabisa ya cheti na sasa ni maprofesa na
walifundisha hawa wanaobeza ngazi hizo.
“Wapo majaji ambao
walianza kazi ya ukarani mahakamani, wakajiendeleza kwa kusoma Chuo cha
Mahakama Lushoto ngazi ya cheti, sasa ni madaktari na maprofesa wa
sheria tunawategemea,” alisema Profesa Parsalao.
BANA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, yeye alisema haamini
kama alichosema Waziri Ndalichako ni tamko na uamuzi wa Serikali, kwani
suala hilo haliko kwenye sera ya elimu na kuonya kuwa alifute haraka
kwani hiyo si njia sahihi ya kuboresha elimu nchini.
Dk. Bana
alikwenda mbali zaidi kwa kutoa mfano wa jinsi yeye alivyosoma kupitia
mfumo huo unaopingwa na Ndalichako hadi hapo alipofikia.
“Kama
kachukua uamuzi huo, nafikiri amekurupuka, kama anafikiria kidato cha
sita ndiyo njia pekee, ameshauriwa vibaya na huo uamuzi aufute haraka
sana na ni kinyume na utaratibu wa elimu kote duniani… utakuwa ni uamuzi
wa dhambi ya asili na dhambi ya ubaguzi. Kama anataka njia ya kuboresha
elimu aje tumfundishe.
“Mimi binafsi sikupitia kidato cha sita
na kuna maprofesa zaidi ya 20 au 40 ninaowafahamu, yupo Profesa Baregu
(Mwesiga Baregu) hakusoma kidato cha sita, kuna Profesa Mathew Luhanga
ambaye alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa
miaka 14, yupo pia Profesa Cuthbert Kimambo ambaye alikuwa Mkuu wa
Taaluma UDSM na wengine wengi, ni watu wanaoheshimika kote duniani,”
alisema.
PROFESA BAREGU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, hakutofautiana na
Dk. Bana. Yeye alisema mfumo uliopo unakubalika duniani kote na ndio
ulioleta msemo wa ‘elimu haina mwisho’.
“Kauli ya waziri
imeonyesha umuhimu wa kuwa na tume ya kitaifa ya kushughulikia suala la
elimu, kwa sababu kweli kuna tatizo la ubora wa elimu yetu na halipaswi
kunyamaziwa, lakini hii si njia sahihi ya kulitatua.
“Sijamwelewa
waziri kwanini ameona diploma kwenda chuo kikuu ndiyo tatizo na kusema
kuwa watu wote wana haki ya kujengewa mazingira ya kujiendeleza
kielimu,” alisema Profesa Baregu.
PROFESA MPANGALA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa (RUCO), Profesa Gaudence
Mpangala, alisema anapinga uamuzi huo wa Profesa Ndachako kwani
utawanyima watu uhuru wa kujiendeleza.
Profesa Mpangala naye
aliwataja baadhi ya maprofesa anaowafahamu ambao hawakupitia kidato cha
sita na akasema wamekuwa msaada mkubwa kwa taifa.
“Profesa
Kimambo alikuwa mwalimu wangu wa Kiswahili, yeye alikuwa na elimu ya
ualimu ‘Grade’ C wa shule ya msingi lakini amejiendeleza hadi amekuwa
Profesa yupo pia Profesa Ndunguru na wengine wengi na waliopitia mfumo
wa Cheti-Stashahada wanakuwa na uzoefu mkubwa kuliko wa kidato cha sita
na wanafanya vizuri wakifika chuo kikuu,” alisema Profesa Mpangala.
TAMONGSCO
Akizungumzia
kauli hiyo ya Profesa Ndalichako, Katibu Mkuu wa Vyuo na Shule Binafsi
Tanzania, Benjamini Nkonya, alisema hawaelewi waziri huyo kutoa tangazo
kama hilo ni kwa sababu watu wengi wamekuwa watumishi bora sana na wengi
hawajasoma kidato cha sita au vinginevyo.
“Wito wetu kwa
Serikali ikamilishe mchakato kwa kupeleka rasimu ya sheria mpya ya elimu
bungeni, ili pawepo na Baraza la Taifa la Elimu ambalo litakuwa na
wawakilishi kutoka sekta ya umma, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) na sekta binafsi kama TAMONGSCO, ambayo itaandaa nyaraka
(regulations) zote kabla hazijawekewa sahihi na kamishna wa elimu,”
alisema Nkonya.
PROFESA MLAMA
Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama, yeye alikubaliana
na mawazo ya Waziri Ndalichako, akisema mfumo huo ni wa zamani na
uliruhusiwa ili kutoa fursa kwa watu kusoma kwa kuwa nchi ilikuwa na
wasomi wachache.
“Sasa hivi kuna wanafunzi wengi wa kidato cha
sita na fursa nyingi za kusoma kidato cha tano na sita zipo, tofauti na
kipindi cha miaka ya nyuma, hakuna ulazima sana wa watu kutegemea njia
yingine wakati wanaweza kusoma kidato cha sita na kuwa sawa na wengine
darasani,” alisema.
LALTAIKA
Kaimu Mkuu wa Idara ya
Ubunifu, Usimamizi wa Teknolojia na Ujasiriamali katika Taasisi ya
Sayansi ya Nelson Mandela, Dk. Amani Laltaika, alipongeza hatua ya
Profesa Ndalichako, huku akisema amegundua tatizo katika elimu na
amethubutu kuchukua hatua ya kurekebisha kuliko waliomtangulia ambao
hawakuchukua hatua yoyote.
“Sifa ya kwanza ya kiongozi ni ubunifu
na kutatua matatizo yaliyopo, nampongeza waziri kwa kugundua upungufu
katika elimu yetu, kwa sababu walikuwapo mawaziri wengi katika nafasi
aliyopo sasa, lakini hawakugundua,” alisema Dk. Laltaika.
SIFA ZA TCU KUJIUNGA NA VYUO
Mwezi
Juni mwaka huu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ilitangaza utaratibu
mpya kwa watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016 na 2017 wanaochukua
shahada.
Utaratibu huo mpya ulikuja baada ya miezi miwili tangu
kutumbuliwa kwa watendaji wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi
wasio na sifa na kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu.
Pamoja na sifa hizo ambazo ziliwahusu
waliomaliza kidato cha sita, pia sifa hizo zilieleza kuwa wale
watakaodahiliwa kujiunga na vyuo ni pamoja na watakaokuwa na utambulisho
wa sifa za kielimu za kidato cha nne kuanzia alama nne ambazo ni D na
kupanda juu katika mchanganuo wa alama za ufaulu wa B+, ikiwa A=75-100,
B+=65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39 na F=0-38.
Sifa nyingine
zinazotajwa ni wenye vyeti vya NVA daraja la tatu, wenye ufaulu si chini
ya alama nne au sifa nyingine zinazokaribiana na hizo, ikiwa ni pamoja
na zinazotambuliwa na Baraza ka Taifa la Mitihani (NECTA) na Elimu ya
Mafunzo ya Ufundi (VETA).
Watahiniwa hao watatakiwa kuwa na
angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada ‘NTA’ daraja la sita au wastani wa B
kwa cheti cha ufundi ‘FTC’ katika mchanganuo wa alama A=5, B=4, C=3 na
D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa wenye stashahada za ualimu au wastani
wa daraja B+ kwa kitengo cha afya kama tabibu wa magonjwa ya binadamu
na nyingine au cheti na stashahada nyinginezo.
Sifa nyingine
zinazoangaliwa katika udahili huo ni pamoja na kuwa na ufaulu wa daraja
la pili kwa wenye Stashahada zisizokuwa za NTA.
Imeandaliwa na Abraham Gwandu (Arusha), Jonas Mushi na Mauli Muyenjwa (Dar)
Chanzo: Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment