Image
Image

Lwenge amesema sekta ya maji nchini ina upungufu wa wataalamu.

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amesema sekta ya maji nchini ina upungufu wa wataalamu wa fani ya maji, hususani katika ngazi ya mafundi sanifu na ndani ya Wizara.
Lwenge amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Chuo cha Maji uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema pamoja na juhudi za serikali za kutaka kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma ya maji, tatizo la wataalamu limeifanya wizara kwa kushirikiana na ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kubadili chuo hicho kuwa Wakala wa Serikali ili kuongeza uhuru katika uendeshaji wa mafunzo.
Lwenge amesema ni imani yake kuwa Bodi hiyo itatoa mchango chanya kwenye chuo hicho ili kisaidie kuongeza wataalamu ili kukabiliana na upungufu huo, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo bora ili kupata wataalamu bora.
“Suala la kuwa na wataalamu bora ni nyeti katika jamii inayotaka maendeleo ya dhati na programu ya maendeleo katika sekta ya maji, haiwezi kuwa endelevu endapo hatutakuwa na wataalamu wa kutosha,” alisema na kuongeza kuwa tathimini iliyofanywa na Wizara mwaka 2014/2015 ilionesha mahitaji ya mafundi sanifu yameongezeka na hadi 6,200.
Lwenge ametoa rai kwa wanafunzi kuwa na maadili na nidhamu wanapokuwa chuoni na mara watakapoanza kufanya kazi katika sekta ya maji na umwagiliaji.
Bodo hiyo inaundwa na Mwenyekiti wake, Profesa Felix Mtalo, Dk Shija Kazumba, Dk Ethel Kasembe, Dk Joyce Nyoni, Amina Mafuru na Dk Lunogelo Bohera.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, iliyoteuliwa Mei 17 mwaka huu, Profesa Mtalo amesema chuo kinakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na mabweni, tatizo lililojitokeza baada ya kuongezeka kwa udahili.
Amesema kabla ya kubadili chuo kuwa wakala 2008, kulikuwa na wanafunzi 200, lakini sasa kuna wanafunzi 1,922 wakati uwezo wa mabweni ni kuchukua wanafunzi 700, jambo linalofanya zaidi ya wanafunzi 1,000 kuishi nje ya chuo.
Amesema changamoto nyingine ni upungufu wa maabara kwa kozi za uchimbaji visima, haidrolojia na uhandisi wa umwagiliaji, jambo ambalo linafanya chuo kutumia gharama kubwa kuwapeleka wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo kwa wakala wa uchimbaji visima Taasisi ya Utafiti ya Mlingano iliyopo Tanga.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment