Ndege iliyobeba watu 81, wakiwemo wachezaji wa klabu moja ya soka ya Brazil, imeanguka eneo la Medellin nchini Colombia.
Taarifa zinasema watu 25 wamethibitishwa kufariki na sita wamenusurika..
Ndege hiyo inadaiwa kupata hitilafu za mfumo wake wa umeme.
Ndege
hiyo ilikuwa safariki kutoka Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji wa
timu ya Chapecoense, ambao walikuwa wamepangiwa kucheza mechi ya fainali
ya Copa Sudamericana, dhidi ya timu ya Medellin, Atletico Nacional.
Mechi
ya awamu ya kwanza ya kombe hilo, la pili kwa umuhimu Amerika Kusini,
ilikuwa imepangiwa kuchezwa Jumatano lakini sasa imesitishwa.
Timu
hito inayotoka mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil, ilipandishwa kucheza
ligi ya daraja ya kwanza nchini Brazil mwaka 2014 na ilifika fainali ya
kombe hilo la Sudamericana kwa kulaza San Lorenzo ya Argentina.
Taarifa
zinasema ndege hiyo muundo wa British Aerospace 146 ambayo imekuwa
ikitumiwa na shirika la ndege la Lamia la Bolivia ilikuwa na abiria 72
na wahudumu tisa.
Maafisa wa klabu hiyo ya Chapecoense wametoa
taarifa wakisema: "Tunamuomba Mungu awe na wachezaji, maafisa,
wanahabari na wageni wengine watu ambao walikuwa wameandamana na ujumbe
wetu."
Wamesema hawatatoa taarifa nyingine hadi ibainike kiwango kamili cha mkasa huo.
Taarifa zinasema watu wawili kutoka kwa timu hiyo - Alan Ruschel na Danilo - huenda wamenusurika.
Telemundo
Deportes wameandika kwenye Twitter kwamba Ruschel ameathiriwa na
mshtuko lakini ana fahamu na anazungumza. Aidha, ameomba aruhusiwe kukaa
na pete yake ya harusi na awaombe jamaa zake.
Ilianguka eneo la
milimani nje kidogo mwa mji wa Medellin majira ya saa sita usiku saa za
huko (saa mbili asubuhi Afrika Mashariki).
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka kwa maafisa wa uwanja wa ndege, marubani walisema ndege hiyo
ilikuwa imepata matatizo katika mfumo wake wa umeme.
Meya wa mji ulio karibu wa La Ceja amethibitisha kwamba mchezaji mmoja wa miaka 25 ni miongoni mwa manusura.
Meya wa Medellin Mayor Federico Gutierrez amesema ajali hiyo ni "janga kubwa".
Maafisa wa uwanja wa ndege wa Jose Maria Cordova de Rionegro uliopo Medellin, wamesema juhudi zote zinafanywa kuwaokoa manusura.
Hali mbaya ya hewa inazuia maafisa kufikia eneo la mkasa kwa urahisi.
Hakukutokea moto baada ya ndege hiyo kuanguka, jambo ambalo linaibua matumaini ya kupatikana kwa manusura.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment