Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukarabati kituo cha afya
cha Laela kilichopo mkoani Rukwa ili kikidhi vigezo vya kuwa Hospitali
ya Wilaya ikiwa ni moja ya jitihada za kupunguza adha ya wananchi
kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya zilipo.
Hayo yamesemwa
leo mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe.
Suleimani Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kwela Mhe. Ignas
Malocha aliyehitaji kujua ni lini kituo hicho cha afya kitapewa hadhi ya
kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mhe. Jafo amesema kuwa ni uamuzi wa muda
mrefu wa Serikali kuiweka Hospitali hiyo kuwa ya Wilaya na ndiyo sababu
ya kufanya jitihada za kukiongezea uwezo kituo hicho kwa kujenga wodi
nyingi pamoja na kutoa kibali cha kuajiri watumishi wapya kwani kwa sasa
kituo hicho kina upungufu wa watumishi .
Amefafanua kuwa hadi sasa
kuna baadhi ya majengo ambayo tayari yameshakamilika ambayo ni jengo la
upasuaji wa dharura, wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji pamoja na
wodi ya mama wajawazito.
“Kwa sasa kituo cha afya cha Laela hakina
miundombinu inayokidhi sifa za kuwa Hospitali ya Wilaya ila kutokana na
kupanuka kwa Mji huo na kuongezeka kwa watu wanaohitaji huduma katika
kituo hicho tumeamua kukiboresha ili kifikie hadhi ya kuwa Hospitali ya
Wilaya”, amesema Jafo.
Ameongeza kuwa kwa sasa huduma za rufaa kwa
wagonjwa wanaohudumiwa katika kituo hicho zinatolewa kupitia magari ya
kawaida ya Halmashauri kutokana na ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa
lakini Wizara ina matarajio ya kutenga fedha ya kununulia gari hilo
katika Bajeti ya mwaka 2017/2018.
Aidha, Mhe. Jafo amethibitisha kuwa
kituo hicho kimetengewa jumla ya shilingi 9,358,100 katika Bajeti ya
fedha ya mwaka huu ambayo itagharamia kununua dawa na vifaa tiba
vitakavyorahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Dkt Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea
kuipitia mikataba ya makampuni binafsi ili kuangalia namna ya
kushirikiana nao katika kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba katika
Hospitali na vituo vya afya nchini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment